Asema Serikali imeamua kuliinua zao hilo ili kukuza uchumi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Simiyu

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua viwanda viwili cha Pamba na Mabomba mkoani Simiyu huku akisisitiza kuwa, Serikali imedhamiria kufanya uwekezaji katika zao hilo na mabadiliko yake yataonekana taratibu kwa kukuza uchumi wa nchi, mkoa na watu.

Rais Dkt. Samia amesema hayo katika ziara yake Mkoani Simiyu wakati akizindua viwanda hivyo viwili ambavyo ni kiwanda cha kuchakata mabomba pamoja na kiwanda cha kuchakata pamba, wilayani Bariadi.

Dk. Samia amezindua viwanda hivyo katika eneo la Salunda ambapo, amekiri kuridhishwa na uchakataji wa zao la pamba katika kiwanda hicho.

Pia alisema, ameridhika na maelezo mazuri aliyoyatoa Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, mara baada ya kuwasili mkoani humo hivyo anatoa wito kwa wananchi kuwa tayari na mabadiliko yanayoendelea sekta ya Kilimo.

Rais Dkt. Samia alisema, mabadiliko hayaji mara moja ni hatua na yana maumivu lakini watakaoumia si wakulima bali wale waliozoea kuwalalia wakulima kwa kununua pamba kwa bei ya chini.

“Nawashukuru wananchi kwa mapokezi.
Nimefungua kiwanda hiki cha mabomba na kuchakata pamba, nimeona kazi inayofanywa na ubora wake nimejiridhisha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni katika zao la pamba,”alisema.

Alisisitiza kuwa, kama ambavyo nchi imefanya vizuri katika zao la korosho, kahawa, tumbaku, mbaazi ndivyo ambavyo kwa sasa serikali inaenda kuweka nguvu katika kulipandisha zao la pamba.

“Uzalishaji wa mabomba utatusaidia sana, tunayo miradi mingi sana ya usambazaji maji sasa mabomba haya yanayozalishwa yatatusaidia huko.

“Tukiwa na wazee jana jioni Waziri wa Kilimo alitueleza mengi mipango ya Serikali katika kuliwezesha zao hili la pamba, tumepandisha zao moja moja sasa tumegeukia pamba hatua tunazochukua ni kwa faida yetu, mabadiliko yanakuwa na maumivu kidogo watakaoumia ni wale ambao hawalimi wanaonunua mazao kwa kuwalalia wakulima na hao ndio wanakuwa na kelele,”alisema.

Aliongeza kuwa “Hatua tunazochukua ni kwa faida ya nchi na wakulima tumefanikiwa katika korosho, tumbaku, kahawa, mbaazi huko wamefaidika sasa huku kwenye pamba tukae mguu sawa, Simiyu zao kubwa ni pamba na lengo la serikali ni kuwafikia wakulima wote,”alisema.

Alisema, mwekezaji wa kiwanda hicho amewaza vyema na ataungana na Serikali kuhakikisha nchi inasitisha upelekaji malighafi za pamba na kuitengeneza hapa hapa nchini ili watu wapate ajira.

“Hicho ndicho tunachotaka, Watanzania wenye uwezo wawekeze hapa na kukuza uchumi wetu sisi wenyewe niwaombe wafanyabiashara wengine wafanye jitihada za uwekezaji.
Serikali imefanya kazi nzuri za maendeleo na zinaonekana wekezeni nyumbani,”alisema.

Viwanda hivyo vyenye thamani ya Sh. bilioni 8, vinamilikiwa na Kampuni ya Moli Oil mills company LTD, ambao pia ni wamiliki wa kampuni za Nsagali.

Aidha viwanda hivyo vimezalisha takribani ajira 850 za moja kwa moja, pamoja na ajira nyingine 400, huku vikitoa fursa kwa wajasiriamali wadogo wadogo kunufaika kwa kufanya biashara za mama lishe.

Rais Dkt. Samia yuko katika ziara ya kikazi mkoani Simiyu, hadi Juni 19, mwaka huu.