Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Kazi nzuri na miradi tele ya maendeleo iliyotekelezwa katika Jimbo la Tanga Mjini imetengeneza deni kwa wananchi wa Tanga Mjini dhidi ya Rais Dk. Samia Suluhu ambaye pia ni Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2025.
Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini (CCM), Ummy Mwalimu, Juni 16, 2025, alipokuwa akitoa hotuba fupi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Tanga Mjini katika Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Tanga. Katika hotuba yake, Ummy Mwalimu amesema Jimbo la Tanga Mjini limepata miradi mingi na mikubwa ya maendeleo ambayo imetatua kero za wananchi.
Kwa msingi huo, Ummy Mwalimu amemuhakikishia Rais Dk. Samia kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, asiwe na wasiwasi wa kura kwani wananchi wa Tanga Mjini watampa asante yao kwa njia ya kumpigia kura nyingi za kishindo ili aendelee kukaa Ikulu awatumikie Watanzania.
“Kwa kazi nzuri zilizofanyika, sisi watu wa Tanga kwakweli hatuna deni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Oktoba 2025, watu wa Tanga tutamlipa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumrejesha Ikulu,” amesema Ummy Mwalimu.
Mwenge wa Uhuru wilayani Tanga umezindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikijumuisha miradi ya afya, maji, elimu, viwanda na utawala ambapo wananchi wamepongeza miradi hiyo iliyozinduliwa kwani imegusa ustawi na maendeleo yao.
