Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishauri Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) kuhakikisha maazimio na matamko yanayopitishwa katika mikutano yake yanatafsiriwa kuwa programu zinazotekelezeka na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa nchi wanachama na wananchi wao

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 23 Julai 2026, alipokutana na Katibu Mkuu wa OACPS, Mhe. Moussa Saleh Batraki, aliyefika Ikulu Zanzibar akiwa na ujumbe wake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi nchini Tanzania.

Amesema maamuzi ya Mkutano wa Nane wa Mawaziri wenye dhamana ya masuala ya bahari, mito, maziwa makuu na uvuvi, uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2024, pamoja na yale ya Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa OACPS, uliofanyika Malabo mwaka 2026, yanapaswa kutafsiriwa kuwa programu zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Azimio la Dar es Salaam limeweka msingi wa pamoja wa kuimarisha usimamizi endelevu wa bahari, uvuvi, ufugaji wa mazao ya baharini, uhifadhi wa mazingira ya bahari na maendeleo mapana ya Uchumi wa Buluu katika nchi wanachama wa OACPS.

Ameeleza kuwa Zanzibar imeendelea kunufaika na programu mbalimbali zinazotekelezwa kupitia ushirikiano baina ya OACPS na Umoja wa Ulaya.

Ameitaja Programu ya Fit for Market inayohusu viwango vya afya ya mimea na usalama wa mazao kuwa miongoni mwa mifano ya ushirikiano huo, ambapo Jumuiya ya Wakulima wa Matunda na Mboga Zanzibar (UWAMWIMA), inayowakilisha wakulima wadogo zaidi ya 2,000, imenufaika na mafunzo ya usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu, viwango vya masoko na usalama wa chakula.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar imeuweka Uchumi wa Buluu katika kiini cha ajenda yake ya maendeleo kutokana na umuhimu wa bahari katika uchumi, ajira, usalama wa chakula, utamaduni na uhifadhi wa mazingira.

Amezitaja sekta za kipaumbele kuwa ni uvuvi, ufugaji wa mazao ya baharini, uzalishaji na uongezaji thamani wa mwani, utalii wa fukwe, usafiri wa majini, uhifadhi wa mazingira ya bahari na usarifu wa bidhaa zinazotokana na rasilimali za bahari.

Ameitaka Sekretarieti ya OACPS kuimarisha ushirikiano wa moja kwa moja baina ya nchi wanachama, hususan Mataifa Madogo ya Visiwa, nchi za mwambao na mataifa yenye maeneo makubwa ya bahari, ili ziweze kubadilishana uzoefu, maarifa na suluhisho za changamoto zinazofanana.

Rais Dkt. Mwinyi amesema ushirikiano huo utaipa Zanzibar fursa ya kunufaika na uzoefu wa nchi nyingine wanachama, sambamba na kushirikisha mataifa hayo uzoefu wake katika utekelezaji wa ajenda ya Uchumi wa Buluu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OACPS, Mhe. Moussa Saleh Batraki, ameishukuru Tanzania kwa mchango wake wa kifedha, ushiriki wake katika mikutano ya Jumuiya hiyo na mchango wake katika masuala ya bahari, uvuvi na Uchumi wa Buluu. Pia, amemweleza Rais Dkt. Mwinyi kuhusu mageuzi yanayoendelea ndani ya OACPS na kuomba ushauri kuhusu changamoto zinazozikabili nchi ndogo za visiwa katika kutekeleza ajenda ya Uchumi wa Buluu.

Ujumbe huo wa OACPS umeambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Said Shaib Mussa, pamoja na viongozi na maafisa kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), Mhe. Moussa Saleh Batraki, pamoja na ujumbe wake, walipofika Ikulu Zanzibar, leo tarehe 23 Julai 2026.