Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia

Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, mkoani Pwani, imetakiwa kuongeza juhudi katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi iliyosimama kwa muda mrefu.

Maagizo hayo yametolewa na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Pwani, Sehemu ya Mipango na Uratibu, Edna Katalaiya, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliolenga kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katalaiya alieleza kuwa usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato utaongeza pato la Halmashauri, ambalo litatumika kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

“Tunaelekezwa katika miongozo ya uandaaji wa bajeti za Serikali kuwa kabla ya kuanzisha miradi mipya, ni muhimu kuhakikisha miradi viporo imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi,” alisisitiza Katalaiya.

Aidha, Halmashauri hiyo imetakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuimarisha usimamizi wa vyanzo vilivyopo kwa kupanua wigo wa ukusanyaji, pamoja na kuanzisha miradi mikakati itakayoongeza mapato na kuchochea ajira kwa vijana.

Vilevile Katalaiya ,aliwakumbusha wakuu wa idara na vitengo kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo wa kujibu hoja, akisisitiza kuondokana na matumizi ya karatasi na kuhimiza mshikamano katika utendaji kazi ili kuepuka kuibuka kwa hoja mpya zisizohitajika.

Aliipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata Hati Safi kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 2020 hadi sasa, pamoja na kufanikisha ukusanyaji wa asilimia 96 ya mapato kufikia Juni 17, 2025.

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mhe. Juma Salum, aliipongeza Serikali kwa kuleta mabadiliko makubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza jitihada za kuvutia uwekezaji katika Kisiwa cha Mafia, hususan katika sekta ya utalii, pamoja na kuleta fedha za utekelezaji wa miradi ya elimu, afya, maji, umeme na barabara.

Kufikia Juni 15, 2025, Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ilikuwa imefanikiwa kufunga hoja 16 kati ya hoja 34 za mwaka wa fedha 2023/2024.