Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetakiwa kutumia ipasavyo fursa ya Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ili kuwaelimisha na kuwafikia kwa karibu watumishi wa umma kuhusu huduma mbalimbali inazotoa, hususan katika sekta ya makazi na ujenzi wa ofisi.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Selemani Mkomi, wakati wa ziara yake katika banda la TBA lililopo viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambako maonesho hayo yanaendelea kufanyika.

“Mmekuja hapa kuonesha huduma zenu ambazo ni muhimu kwa watumishi wa umma. Hawa ndio wahitaji wakuu wa nyumba za makazi, ofisi na miundombinu mingine ya matumizi. Hakikisheni mnatumia nafasi hii kutoa elimu ya kutosha ili huduma zenu zijulikane vizuri zaidi,” amesema Mkomi.
Aidha, amesema bado kuna changamoto ya uelewa kwa baadhi ya watumishi wa umma kuhusu mahali pa kupata huduma za makazi, hivyo amesisitiza TBA kuongeza juhudi za kuhamasisha na kutoa taarifa sahihi kwa umma, hususan walengwa wa moja kwa moja wa huduma hizo.

Kwa upande wake, mmoja wa watumishi wa umma waliotembelea banda hilo, Hussein Mzee Mussa, amepongeza jitihada zinazofanywa na TBA katika utekelezaji wa miradi ya makazi, akitaja mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 3,500 katika eneo la Nzuguni, jijini Dodoma kama kielelezo cha mafanikio.
“Mradi huu unatoa matumaini makubwa kwa watumishi wa umma na ukikamilika utapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la makazi hapa Dodoma,” amesema Bw. Mussa.
Kupitia maonesho hayo, TBA inaendelea kutoa elimu na maelezo kuhusu miradi mbalimbali ya ujenzi inayoitekeleza, ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi kwa watumishi wa umma, ujenzi wa ofisi za serikali, pamoja na kushiriki katika ujenzi wa mji wa serikali jijini Dodoma.
