WIMBI la joto kali limeikumba sehemu kubwa ya bara la Ulaya, likisababisha shule nyingi kufungwa na vifo vya watu kuripotiwa katika nchi za Uhispania, Ufaransa na Ureno.

Katika baadhi ya maeneo ya Uhispania na Ureno, viwango vya joto vimeripotiwa kuvuka nyuzi joto 45 katika kipimo cha Celsius, hali iliyopelekea watu wanne kupoteza maisha kutokana na madhara ya joto hilo.

Nchini Ufaransa, zaidi ya watu 300 wamepelekwa hospitalini kwa huduma za dharura kutokana na matatizo yanayohusishwa na joto kali, huku watu wengine wawili wakifariki dunia.

Waziri wa Ikolojia wa Ufaransa, Agnes Pannier-Runacher, amesema mwezi Juni 2025 umeweka rekodi mpya kama mwezi wenye joto kali zaidi haiajwahi kutokea nchini humo tangu mwaka 1900.

Wataalamu wa hali ya hewa nchini Ujerumani na Ufaransa wametoa tahadhari kuwa wimbi hilo la joto litaendelea kwa siku chache zijazo kabla ya kushuka mwishoni mwa wiki.