Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia Dodoma

Biashara ya kaboni (hewa ukaa) imekuwa chanzo kipya chenye tija kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Katavi, hususan Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kwa kufungua fursa mpya na kuchochea ustawi wa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza Julai 3, 2025 jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko amesema kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu, mkoa umepokea zaidi ya shilingi bilioni 25 kutokana na biashara hiyo, fedha ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya elimu, afya, miundombinu, ajira, kilimo na huduma za kijamii.

Amesema kupitia mapato hayo, mkoa umefanikiwa kujenga madarasa zaidi ya 50, kukarabati madarasa 20 na kujenga nyumba sita za walimu kwa mifumo tofauti. Katika sekta ya afya, vichomea taka na mashimo ya kondo la mama yamejengwa katika vituo mbalimbali, sambamba na ujenzi wa matundu ya vyoo, madawati karibu 1,500, masoko mapya ya vijijini na ofisi za vijiji.

Aidha, amesema vijana zaidi ya 100 wamepata ajira za kulinda misitu, kaya elfu nne zimepatiwa bima ya afya, walimu wa mkataba wameajiriwa na chakula kimeendelea kutolewa kwa shule 16. Wanawake wajasiriamali pia wamenufaika kwa mikopo inayozidi milioni 100.

Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2 zilizopokelewa Aprili mwaka huu, zinatarajiwa kutumika kuboresha shule za msingi na sekondari, kutoa ajira mpya kwa walimu na wahudumu wa afya vijijini pamoja na kuimarisha uhifadhi wa misitu.

Kwa upande wa kilimo, ameeleza kuwa ukarabati wa skimu kubwa za umwagiliaji za Mwamkulu na Kabage unaendelea kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 55, na tayari utekelezaji wake umefikia hatua ya robo. Kukamilika kwake kutasaidia kuongeza eneo la umwagiliaji mara zaidi ya mbili, na kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa kiwango kikubwa. Vilevile, vijana zaidi ya mia saba wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa, huku vyama vya ushirika vikiendelea kuongezeka kwa kasi.

Katika sekta ya miundombinu, barabara kuu kama Mpanda–Tabora, Mpanda–Vikonge na Mpanda–Sitalike zimekamilika na zinatumika, huku nyingine kama Vikonge–Luhafwe na Kibaoni–Sitalike zikiendelea kujengwa. Daraja kubwa la Kavuu linaendelea kujengwa na lile la Msadya tayari limekamilika.

Sekta ya elimu pia imenufaika ambapo shule mpya 129 zimejengwa kupitia programu mbalimbali za Serikali ikiwemo BOOST, UVIKO na SEQUIP. Shule ya wavulana ya kanda imepokea zaidi ya shilingi bilioni 4, sawa na shule maalumu ya wasichana katika Halmashauri ya Nsimbo. Vilevile, Mradi wa Maji wa Miji 28 unaendelea kutekelezwa ndani ya Manispaa ya Mpanda.

Katika afya, miradi 22 mipya inatekelezwa ikiwa ni pamoja na hospitali mpya za wilaya, vituo vya afya na zahanati. Kwa upande wa nishati, vijiji vyote 172 vya mkoa tayari vina huduma ya umeme kupitia Mradi wa REA, huku vitongoji zaidi ya 500 kati ya 912 vikiwa tayari vimeunganishwa.

Mhe. Mrindoko ameeleza kuwa miradi mingine mikubwa ni pamoja na kukamilika kwa Bandari ya Karema, miradi ya umwagiliaji, ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya za Tanganyika na Mlele, ujenzi wa vihenge na ofisi za kuhifadhi mazao ya NFRA pamoja na ukarabati wa reli ya Kaliuwa–Mpanda yenye urefu wa zaidi ya kilomita 200.

Amesisitiza kuwa mafanikio haya makubwa yanatokana na matumizi sahihi ya mapato ya kaboni, ushirikiano wa wananchi na uongozi makini wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya kweli na endelevu kwa Watanzania.