Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa wito kwa vyombo vya habari na vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuhakikisha vinatoa nafasi ya haki na usawa kwa wagombea wote kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano uliowakutanisha wadau wa sekta ya habari, Dkt. Biteko alisema kuwa uchaguzi ni kipindi nyeti kinachopaswa kuwa na umoja wa kitaifa, kwa kuwa taarifa nyingi husambaa na kuwa msingi wa maamuzi ya wananchi kuhusu nani wa kumchagua.
“Katika kipindi hiki cha uchaguzi ni kawaida hata watu wa familia moja kutofautiana kimawazo. Mkutano huu ni sehemu ya kuwaleta pamoja wadau ili pamoja na tofauti zetu, tusalie wamoja. Sisi ni Watanzania wenye nia ya kuijenga nchi yetu na kuifanya istawi zaidi,” alisema.

Dkt. Biteko alisisitiza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, kwa kufuatilia na kuripoti matukio mbalimbali kabla, wakati na baada ya uchaguzi, na kuvitaka vyombo hivyo kuwa waaminifu kwa jamii kwa kusambaza taarifa sahihi na za kuaminika.
“Katika zama hizi ambapo nguvu ya mhariri imepungua na taarifa huweza kusambazwa bila kupitia mchakato rasmi wa uhariri, ni muhimu sana kwa wanahabari kutumia weledi wao na kulinda tasnia hii kwa wivu mkubwa. Tukikosa uangalizi, tunaweza kugawanyika kama taifa,” alisema.
Alibainisha kuwa kwa sasa Tanzania ina vyombo vingi vya habari ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ikiwa ni matokeo ya mazingira bora yaliyowekwa na serikali. Alisema kuna magazeti 375, vituo vya redio 247, vyombo vya habari mtandaoni 355, blogu 72, na vituo vya televisheni 68 ambavyo vimeajiri idadi kubwa ya vijana na kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
“Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa kipaumbele kikubwa kwa sekta ya habari. Moja ya hatua za mwanzo kabisa alizochukua ni kufungua baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na kurejesha leseni vilivyonyang’anywa,” alisema.

BODI YA ITHIBATI
Akizungumzia hatua nyingine za serikali, alisema serikali imeanzisha Bodi ya Ithibati kwa waandishi wa habari ili kuhakikisha kuwa huduma za habari na utangazaji zinazingatia viwango vya weledi na maadili.
“Waandishi wa habari mnapaswa kuwa walinzi wa kweli, wajenzi wa amani na waoneeni wivu taaluma yenu. Katika mazingira haya ya teknolojia na taarifa potofu, mnapaswa kuwa waangalifu sana na kuhakikisha jamii inapata habari sahihi,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wanahabari kutumia lugha ya staha, kuepuka uchochezi, na kuripoti kwa usawa bila upendeleo wakati wa kampeni, uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.

Alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi, vyombo vya habari vinapaswa kuhimiza siasa za maelewano na uvumilivu, kuheshimu tofauti za maoni, na kutambua kuwa kutofautiana si dhambi wala kosa, bali ni sehemu ya demokrasia.
ULINZI NA USALAMA
Kwa upande wa vyombo vya ulinzi na usalama, Dkt. Biteko alieleza kuwa serikali imejipanga kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi zao katika mazingira salama, huru na rafiki, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kulinda usalama wa wanahabari na mali zao wakati wote wa uchaguzi.
“Tutahakikisha kuwa kila mwanahabari anarudi nyumbani kwake akiwa salama. Tutaendelea kulisimamia hili kwa nguvu zote kupitia vyombo vyetu vya dola,” alisema.
Alimaliza kwa kutoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kushirikiana kwa karibu na Tume Huru ya Uchaguzi ili kupata taarifa sahihi na kwa wakati. Pia alizitaka taasisi za habari kujitathmini mara kwa mara kwa lengo la kulinda maslahi mapana ya tasnia hiyo.
