Na Mussa Augustine,JamhuriMedia

Chama Cha Wakulima (AAFP), kimeishauri serikali kudhibiti usafirishaji wa chakula nje ya nchi ili kuzuia mfumuko wa bei na uhaba wa vyakula nchini.

Rai hiyo imetolewa jiijini Dar es Salaam leo Februari 15,2023 na Mwenyekiti Taifa wa chama hicho Said Soud Said wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mustakabali wa mikutano ya hadhara ya chama hicho inayotarajiwa kuanza Machi 17, mwaka huu, jijini Dodoma kikiwa na sera ya” Siasa na Watu”

Aidha ameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili kunusuru hali ya kupanda kwa gharama za maisha kutokana na ongezeko la kupanda kwa bei ya vyakula nchini.

” Sisi kama AAFP tunamshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua za kuzuia usafirishaji wa chakula nje ya nchi,kwani kufanya hivyo inachangia kuwepo na uhaba wa chakula ndio maana hata bei imekua juu sana,Mtanzania mwenye kipato cha kawaida hawezi kumudu”amesema mwenyekiti huyo.

Aidha amesema kuwa chama hicho kinatumia sera ya “Siasa na Watu” wakati wa mikutano ya kisiasa ikiwa lengo ni kuieleza Serikali namna ya kuboresha maisha ya watu Wakulima ,wavuvi,wafugaji kwani nchi ya Tanzania inaendeshwa kwa misingi ya kikatiba.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa ni wajibu kwa Serikali kuwajali wananchi wake ktika nyanja mbalimbali ikiwemo kuwaondoa katika lindi la umasikini,maradhi na ujinga kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kuwanufaisha Wananchi wote.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amemuomba Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuyaendeleza mazuri aliyoyaacha mtangulizi wake hayati Rais Dkt. Jonh Magufuli ,kwa kuyajali makundi mbalimbali ikiwemo Wazee, wajane,na Watu wasio jiweza.

“Tunamuomba Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan afuate nyayo za mtangulizi wake Hayati Dkt Magufuli kwa kuwajali na kuwatetea wanyonge waliodhulumiwa haki zao,asikubali kupotoshwa na baadhi ya watendaji wake kwa kupelekewa taarifa zisizo sahihi hususani katika janga hili la kupanda kwa bei ya vyakula” amesisitiza.

Wakati huo huo, halmashauri kuu ya chama hicho imewateua Said Soud Said kuwa mwenyekiti Taifa,Nancey Mlikaria makamu mwenyekiti bara,Omary Juma makamu maenyekiti Zanzibar, huku nafasi ya katibu Mkuu Taifa ikichukuliwa na Rashid Mohamed Rai na Naibu katibu Mkuu Bara akiwa ni Mark Mhemela ,na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar akiwa ni Chumu Abdalah.

By Jamhuri