Uliokuwa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) kwa miaka minne umeshindwa kulipa mafao ya kustaafu ya askari polisi aliyelitumikia jeshi hilo kwa miaka 33, kisa kabambikizwa uanachama katika mfuko mwingine.

Thomas Njama, amestaafu Jeshi la Polisi mwaka 2015 akiwa Kituo cha Polisi cha Mto wa Mbu mkoani Arusha.

Amesema PSPF wanatakiwa kumlipa kiinua mgongo cha Sh 47,162,022 na pensheni ya kila mwezi ya Sh 253,559 kwa mujibu wa hesabu za utumishi wa jeshi hilo aliyopatiwa na mfuko huo.

Lakini mfuko huo wa PSPF unashindwa kumlipa mafao hayo kwa kigezo kwamba ni mwanachama wa mfuko mwingine wa pensheni kwa watumishi wa umma, GEPF.

GEPF, ambao wanadai kuwa amechangia mfuko wao kwa muda wa miaka 16, wamemlipa kiinua mgongo cha jumla ya Sh 6,813,931 ambacho alilipwa kwa mkupuo mmoja kupitia hundi namba 543 ya Desemba 28, mwaka 2015.

Malipo hayo yaliambatana na malipo ya mwezi Julai hadi Januari 2016, hivyo kufanya kiinua mgongo alichopokea kuwa jumla ya Sh 7,767,884.

Amedai kiinua mgongo hicho hakitambui kwa sababu amepunjwa na kwamba mfuko huo amebambikiziwa.

“Wanasema nimekuwa mwanachama wao kwa miaka 16, si kweli, uanachama wangu ulikuwa PSPF.

“Wakati napatwa na matatizo na kuwekwa mahabusu mwaka 2002 uanachama wangu wa PSPF ulifanyiwa uhuni ukahamishiwa GEPF,” amedai Njama.

Amehoji inawezekanaje mtuhumiwa aliyesimamishwa kazi na mshahara wake kurejeshwa hazina, ufunguliwe makato katika mfuko mwingine ambao hana uanachama nao?

“Unajua kwa mujibu wa sheria za jeshi, ukishtakiwa mahakamani unakuwa umefukuzwa kazi moja kwa moja, mimi nilifukuzwa na mshahara wangu ukasitishwa.

“Kinachonishangaza Mfuko wa PSPF ambako nilikuwa mwanachama tangu mwaka 1999 baada ya kuwekwa magereza mwaka 2002 walisitisha makato yangu lakini baadaye GEPF wakaanza makato kwenye mshahara wangu ambao uliamuliwa kurejeshwa hazina,” amesema Njama.

Amehoji inawezekana vipi jambo hilo likatendeka kwa kipindi kifupi baada ya yeye kwenda mahabusu na kwamba huo ni mchezo uliochezwa ukishirikisha baadhi ya watendaji.

“Kama PSPF walitambua kwamba mimi nimefukuzwa kazi wakasitisha makato yangu ya uanachama ni nani aliyewaambia GEPF waanze kunifanyia makato wakati mimi niko mahabusu ilhali sikuwa mwanachama wao?

“Baada ya kutuhumiwa kwamba tumefanya mauaji kwa mtu aliyekuwa mahabusu tulifukuzwa kazi na mishahara yetu kuamuliwa irudishwe hazina.

“Kwa nini haikurudishwa, badala yake walianza kuifanyia makato tena katika Mfuko wa GEPF. Ni nani alikuwa mnufaika wa mshahara wangu wakati mimi siko kazini?” amehoji Njama.

Hata hivyo mwaka 2007 baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kusikiliza shauri lao na kubaini hana kosa aliachiwa huru.

Baada ya hukumu hiyo Jeshi la Polisi likaelezwa kumrudisha kazini na kwamba stahiki zake zote zirejeshwe, na baada ya kurejeshwa kazini alibaini uanachama wake ulikuwa umehamishiwa mfuko mwingine.

Anaamini kuna wahusika wa mchezo huo kwani baada ya kukaa mahabusu kwa miaka mitano alipoachiwa alihoji kuhusu suala hilo maofisa wa Jeshi la Polisi wakamjibu kuwa alisaini mwenyewe kuwa mwanachama wa Mfuko wa GEPF.

Alipowahoji GEPF kuhusu uanachama wake, walimjibu kwamba wao wameletewa jina lake na kwamba walielezwa na maofisa wa polisi kuwekwa katika mfuko huo.

Amesema alivyowahoji maofisa wa jeshi hilo kwamba hajawahi kuwa mwanachama wa GEPF ni nani aliyeweka sahihi kwenye nyaraka za uanachama wake, walimtaka kuachana nalo kwani walimtishia kumfungulia tena kesi ya mauaji.

“Niliamua kukaa kimya, kwa sababu tayari nilikuwa nimekwisha kufanyiwa hujuma, isitoshe hata familia yangu ilikuwa imeyumba hivyo sikuona haja ya kuingia kwenye migogoro tena,” amesema Njama.

Hata hivyo anabainisha kuwa kipindi cha nyuma Mfuko wa GEPF ulikuwa unashawishi wakurugenzi wa taasisi mbalimbali kupeleka wanachama wao katika mfuko huo na kwamba kamisheni itakayopatikana watagawana na maofisa hao.

“Kuna kipindi Polisi walilazimishwa kujiunga na GEPF kisa mfuko huo ulitaka kufa, maofisa wa Polisi walilazimisha polisi kujiunga na mfuko huo,” amesema.

Anaeleza kuwa kutokana na sakata hilo, Jeshi la Polisi walimlazimisha kustaafu, na kwa mujibu wa cheo chake alitakiwa kustaafu akiwa na miaka 60 lakini badala yake akastaafu akiwa na miaka 50.

Mifuko hiyo ambayo kwa sasa imeunganishwa katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa PSSSF, anadai kwamba imemsababishia usumbufu mkubwa katika kufuatilia haki yake.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSF), Hosea Kashimba, amesema hilo ni suala la kawaida kutokea na mara nyingi linasababishwa na uelewa mdogo anaokuwa nao mwanachama katika kufuatilia haki yake.

“Hilo ni suala la uelewa tu, mwambie huyo askari mstaafu aende kwenye ofisi zetu la PSSSF za Ilala (Dar es Salaam) akaonane na meneja akamweleze tatizo lake,” amesema Kashimba.

Na kwamba haiwezekani pesa yake kupotea kama ana uhakika na hoja zake awaombe kukagua faili lake ili kubaini ni wapi lilipo tatizo na liweze kushughulikiwa.

Kashimba ameongeza kuwa huenda tatizo hilo likawepo kwani kipindi cha nyuma askari waliokuwa wakiingizwa katika mifuko hiyo walikuwa wakitazamwa katika madaraja na vyeo vyao.

“Sidhani kama kuna tatizo hapo, huenda suala hilo limetokana na makosa madogo yaliyojitokeza wakati wa kuwapanga kwa madaraja.

“Ili tatizo liweze kurekebishwa mwambie afuatilie ajue makosa hayo ni yapi na yanarekebishika, na mweleze hivi nimekuagiza aende ofisini kwa meneja Ilala wakague faili lake.

“Kama ana uhakika na stahiki zake uhakiki utafanyika na atalipwa tu hakuna wasiwasi wowote,” amesema Kashimba.

Ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini kwa hoja kwamba si msemaji wa jeshi hilo amesema: “Kujiunga na mifuko ni hiari ya mtu mwenyewe, ninachoshauri wanaoweza kulitolea ufafanuzi ni wahusika wa mifuko hiyo.

By Jamhuri