Shule ya Sekondari ya Scolastica iliyopo Himo, Moshi mkoani Kilimanjaro inatuhumiwa kuajiri mwalimu raia wa Kenya asiyekuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini.

Mwalimu Laban Nabiswa, ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika Shule hiyo ya Scolastica.

Laban amekiri mahakamani kuishi na kufanya kazi nchini isivyo halali wakati kesi ya mauaji inayowakabili yeye na wenzake watatu ikiendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi.

Kibali cha miezi mitatu cha kuishi nchini kilimalizika muda wake mwezi mmoja kabla ya tukio la mauaji la Novemba 6, 2017.

Washtakiwa wengine katika shauri hilo la jinai namba 48/2018 ni Mkurugenzi wa Shule hiyo, Edward Shayo (mshtakiwa wa pili) na aliyekuwa mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha (mshtakiwa wa kwanza).

Siri ya mshtakiwa huyo kuishi nchini isivyo halali ilifichuliwa na wakili upande wa mashtaka, Abdallah Chavulla, wakati akimdodosa mshtakiwa huyo muda mfupi baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Firmin Matogolo.

Mshtakiwa huyo ambaye pia ni shahidi wa tatu upande wa utetezi, alidai kuwa aliingia nchini Julai 10, 2017 na kibali chake kilikuwa kinamalizika Oktoba 10, mwaka huo.

Mbali na muda wake wa kuishi nchini kuwa ulimalizika, pia ilibainika mahakamani hapo kuwa kibali cha mshtakiwa huyo hakikumruhusu kufanya kazi ya ujira.

Sehemu ya mahojiano ya Wakili Gwakisa Sambo na mshtakiwa huyo ni kama ifuatavyo:

Wakili: Shahidi hebu iambie mahakama, Novemba 2017 ulikuwa unaishi wapi?

Shahidi: Nilikuwa naishi Himo Mheshimiwa Jaji.

Wakili: Hapo Himo ulikuwa unaishi na nani?

Shahidi: Nilikuwa naishi na mke wangu na watoto Mheshimiwa Jaji.

Wakili: Mke wako anaitwa nani?

Shahidi: Anaitwa Suzan.

Wakili: Mwaka 2017 ulikuwa unafanya kazi gani?

Shahidi: Nilikuwa nafanya kazi ya ualimu, nilikuwa nafundisha darasani, pia nilikuwa mwalimu wa nidhamu Mheshimiwa Jaji.

Wakili: Shahidi hebu iambie mahakama, tarehe 6/11/2017 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa shuleni Scolastica na saa 9 jioni nilirudi nyumbani kwa mapumziko mafupi kwa ajili ya kujiandaa kurudi shuleni jioni.

JAMHURI limemtafuta Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Albert Rwelamira, kutaka kujua kama ofisi yake inazo taarifa za mshtakiwa huyo kuwa nchini kinyume cha sheria.

Rwelamira amesema hawakuwa na taarifa hizo na kuahidi kulifanyia kazi, ikiwamo kufuatilia mwenendo wa kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi.

Humphrey Makundi aliripotiwa kutoweka shuleni hapo Novemba 6, 2017 na mwili wake ulipatikana Novemba 10, mwaka huo katika Mto Ghona – mita 300 kutoka shuleni hapo.

Polisi waliopoa mwili na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi kabla ya kuzikwa Novemba 11 katika makaburi ya Karanga baada ya kutotambuliwa.

Hata hivyo, baada ya mwili huo kuzikwa, polisi kwa kushirikiana na baba wa marehemu, Jackson Makundi, waliendelea na uchunguzi na Novemba 17 mwili huo ulifukuliwa kwa kibali cha Mahakama.

Baada ya tukio hilo, polisi waliwakamata washtakiwa. Katika maelezo ya mshtakiwa wa kwanza, Chacha, amekiri kumpiga mwanafunzi huyo kwa ubapa wa panga.

Chacha katika maelezo yake anadai kuwa siku ya tukio alisikia kishindo cha mtu akiruka ukuta wa shule na baada ya kufuatilia aliona mtu akikimbia na ndipo alipomkimbiza.

Anadai kuwa alimfikia mtu huyo na kumpiga kwa ubapa wa panga na baadaye aliendelea kumshambulia kwa kutumia panga lake hadi akapoteza fahamu.

Kulingana na maelezo yaliyosomwa mahakamani hapo, Chacha anadai kuwa baadaye alimjulisha mshtakiwa wa pili na wa tatu na wakafika eneo la tukio.

Akaendelea kueleza kuwa baada washtakiwa hao kufika alishauri Makundi apelekwe hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini mshtakiwa wa pili ambaye pia ni mmiliki wa shule hiyo alikataa ushauri huo.

Chacha anadai kuwa mshtakiwa wa pili alishauri mwili huo ukatupwe katika Mto Ghona kwa kile alichodai italeta shida. Washtakiwa hao wa kwanza na wa tatu walitii agizo hilo na kwenda kuutupa mwili huo mtoni.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili David Shilatu, Elikunda Kipoko, Gwakisa Sambo na Patrick Paul. Upande wa mashtaka unaongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande, akisaidiwa na mawakili Abdallah Chavulla, Omari Kibwana na Lucy Kyusa.

Tayari kesi hiyo kwa sasa ipo katika hatua ya kutolewa kwa tarehe ya hukumu baada ya Jamhuri na upande wa utetezi kufunga ushahidi pamoja na wazee wa baraza kutoa maoni yao.

Upande wa Jamhuri uliita mashahidi 19 wakiwamo madaktari bingwa wawili kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC walioufanyia uchunguzi mwili wa marehemu – Dk. Alex Mlemi na Dk. Samwel Mwita; pia Hadija Mwema kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mashahidi wengine ni baba mzazi wa marehemu, Jackson Makundi; mhudumu katika chumba cha kuhifadhia maiti Mawenzi; Mlinzi wa Amani na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Moshi Mjini; na mtaalamu kutoka Kampuni ya simu ya Vodacom.

Upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo vya nyaraka yakiwamo maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza, Chacha aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani na panga linalodaiwa kutumiwa na mshtakiwa huyo.

Vielelezo vingine ni ripoti ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), ripoti ya uchunguzi wa kifo na ripoti ya mawasiliano ya simu ya washtakiwa ambayo yanaonyesha waliwasiliana siku ya tukio pamoja na simu saba na nguo za marehemu alizokuwa amezivaa siku ya tukio.

By Jamhuri