Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jabarhila, iliyopo Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza, Mwatanda Omari (37), amehukumiwa kwenda jela miezi 12 kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono.

Mwalimu Omari alitenda kosa hilo Machi 9, 2017 kwa kumuomba rushwa hiyo mzazi wa mwanafunzi katika shule hiyo. Jina la mzazi limehifadhiwa.
Mzazi alikuwa anaomba uhamisho wa mtoto kutoka shuleni hapo kwenda Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilikuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mbele ya Hakimu Abesizya Kalegeya.
Kaimu Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, amesema mwalimu huyo alinaswa kwenye mtego aliowekewa.

“Mwalimu Mkuu huyo ndiye mwenye mamlaka ya kujaza fomu ya uhamisho. Alitaka apewe ngono ndipo aweze kujaza fomu hiyo,” amesema Stenga.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwanasheria wa Takukuru, Placidia Rugalema, uliomba mwalimu huyo apewe adhabu kali kwa kuwa rushwa ya ngono imeshamiri.
Baada ya kusomewa hukumu, mshtakiwa aliiomba mahakama imsamehe kwa kuwa hakutenda kosa hilo kwa kukusudia.
Hata hivyo, mahakama ilimwadhibu kwa kumpeleka jela miezi 12 au kulipa faini ya Sh milioni 2.5.  Alikosa kiasi hicho cha fedha na kupelekwa gerezani.

Wakati huo huo, mfanyabiashara wa mazao ya kilimo, Benjamin Rweyemamu (50) amehukumiwa kwenda jela miaka mitatu.
Rweyemamu amepatikana na hatia ya kushawishi na kutoa rushwa, kinyume cha Kifungu cha 15 (I) (b) cha Sheria ya Takukuru, Na. 11 ya Mwaka 2007.
Mfanyabiashara huyo alimshawishi Ofisa wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili ampitishie mkopo wa Sh milioni 235.378.

“Alimwahidi kumpatia Sh milioni tano iwapo atafanikisha kupatikana kwa mkopo huo. Alitanguliza hongo ya Sh 100,000 kwa ofisa huyo wa benki. Amefanya hivyo ili kumshawishi akamilishe mchakato wa maombi yake,” amesema Stenga.

Kesi hiyo ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza mbele ya Hakimu Bonaventure Lema, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru alikuwa Wakili Maximilian
Yabona.
Mtuhumiwa alikiri makosa yake hivyo mahakama ikamhukumu kwenda jela miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh 500,000. Alilipa faini hiyo na kuachiwa.

Katika tukio jingine, shaka imeibuka kwenye fedha za ujenzi wa Shule ya Msingi Buhingo, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Shule hiyo ni miongoni mwa miradi 20 ya kimaedeleo yenye jumla ya Sh 23,225,199,261.09 inayojengwa katika halmashauri zote mkoani Mwanza.

Habari za kichunguzi zinasema Sh milioni 86.6 zinazotiliwa shaka matumizi yake zilielekezwa na serikali kujenga vyumba vitatu vya madarasa, matundu sita ya vyoo na kuchimba kisima kirefu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Anthony Bahebe, amekiri kuwapo dosari kadhaa katika matumizi ya fedha za ujenzi wa mradi huo.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Stenga, amesema wameshaanza uchunguzi wa suala hilo.

Please follow and like us:
Pin Share