Afrika bara kubwa lenye changamoto nyingi

url-5Kijiografia Bara la Afrika ni miongoni mwa Mabara sita yanayo unda Ulimwengu huu likiwa ni la pili kwa ukubwa wa maili za mraba zipatazo 11,700,000 sawa na asilimia 22% za eneo lote la dunia.

Bara hili la Afrika linafahamika kama ‘Sleeping giant’ hadi kufikia mwaka 2005 uchumi wake umekuwa ukikua kwa takribani asilima tano na likiongoza kwa kutoa ajira nyingi kwa mataifa mengi toka ugaibuni.

Bara hili limekuwa likitoa karibia asilimia 8% ya nishati ya mafuta inayozalishwa duniani huku likitoa malighafi muhimu kama chuma na chakula.

Historia ya kale inaeleza kuwa bara hili limechangia kwa kiwango kikubwa sana maendeleo ya nchi nyingi za Ulaya, Marekani na nchi nyingine duniani.

Marehemu Profesa Ali Mazrui katika moja ya andiko lake linalofahamika kama (From slave ship to space ship Africa between Marginalization) anafafanua kwa kiwango gani mataifa ya Ulaya na Marekani yalivyo changia kuidhoofisha bara la afrika na jinsi lilivyo endelea kuwa shamba la bibi.

Anaenda mbali kwa kulifananisha bara hili na shamba la bibi ambalo mtu mweupe anaweza kutoka kwao akiwa na dola mia mbili lakini baada ya mikaka miwili au mitatu akarudi kwao akiwa ni bilionea.

Anasema kuwa kabla ya ukoloni uhusiano kati ya mataifa haya ya Ulaya na Marekani ulikuwa ni biashara ya watumwa ndio maana nguvu kazi kubwa toka Afrika ili safirishwa kwenda Ulaya na Marekani.

Matokeo ya nguvu kazi hiyo ndiyo maana leo miji kama New york, Paris, na miji mingine ya Ulaya na Marekani inaonekana vile ilivyo.

Anasema tangia kuanzishwa kwake Umoja wa Afrika moja ya majukumu yake ilikuwa ni kuhakikisha Bara hili lina anza kupiga hatua za kimaendeleo kwa kuhakikisha ustawi wa watu wake.

Kinyume chake ni kuwa Umoja huu ulikuwa ni dhaifu na umeshidwa kutekeleza majukumu yake na kushindwa kupambana na nguvu za mabeberu toka nje.

Katika ripoti iliyotoewa na Oxfarm mwaka 2007 ilitoa taarifa kuwa migogoro mingi inayo sababishwa na matataizo ya kivita katika bara yamekuwa yakisababisha bara hili kutumia dola bilioni 18 za Kimarekani kununua silaha.

Hizi ni pesa ambazo kama zingeelekezwa kwenye shuguli za kimaendeleo katika bara hili zingesaidia kunyanyua maisha ya wananchi wengi wanaoishi chini ya dola moja.

Anasema badala yake tumekuwa tukishuhudia jinsi silaha hizo zinavyotumika kuangamiza maelfu ya watu wengi wasio kuwa na hatia katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Anasema kila mmoja ameshuhudia yale yaliyo tokea katika nchi za Libya, Tunisia na Misri na sehemu nyingine katika bara hili huku Afrika ikishindwa kuwa na msimamo mmoja.

Matokeo ya kufeli huko ni kuzaliwa kwa matatizo ya ndani yasiyo isha, vyama vya kisiasa vimegeuka vimesahau majukumu yao yaliyopelekea kuasisiwa kwao.

Anasema Katika hali halisi ndani ya nchi nyingi za kiafrika leo ni ukweli usiopingika kuwa sera za ndani ya nchi nyingi hazikujengwa juu ya usawa, upendo na mshikamano bali imejengwa katika misingi ya kibepari.

Ndiyo maana hadi hii leo hakuna hata kiongozi hata mmoja katika bara hili la kiafrika anayeweza kusema ni kiasi gani bara hili linapata kutokana na raslimali zake kuendelea kuporwa na watu wa nje.

Kinachoweza kusemwa ni kuwa waafrika wachache walioko kwenye nafasi za juu ndio wanaopata nafasi ya kutupiwa makombo na wakubwa (wawekezaji) walio achiwa kumiliki raslimali.

Anasema kwa wale wanaolijua historia ya bara la Afrika  lilikotoka watakubaliana kuwa Afrika ya leo haina tofauli na ile ya miaka ya 1940 kwani imerudi enzi zile za zama za utumwa.

Historia ya bara hili inaeleza wazi kuwa wakati wa ukoloni ‘sisi’ kama watwana wa wakoloni tulikuwa mali ya wakoloni pamoja na raslimali zote.

Kitendo cha viongozi wa bara la Afrika kulaghaiwa na kujiingiza kwenye mikataba ya kinyonyaji na kubinafsisha kila kitu kwa wageni ni hali ya hatari katika ustawi wa bara hili.

Ni bora kama waafrika tukaelewa kuwa yote haya yanayo tokea katika bara hili yote ni matokeo ya sera mbovu za kupenda kuiga Uzungu kisha kuuhamishia Afrika toka Ulaya na Marekani.

Kama tunahitaji kuiacha Afrika mpya kwa kizazi kijacho viongozi wetu wa (AU)  wanatakiwa kujenga umoja wa bara hili ambao ni lazima utapatikana kutokana na utawala bora wenye kujali wanyonge.

Ni bora wakaelewa kuwa maendeleo ya bara hii yataletwa na waafrika wenyewe na si kwa kumtegemea mjomba toka Ulaya au Marekani pia ni lazima kuwa makini na sera hizi za mabeberu zinazopoteza nuru ya Afrika.