url-4Ndugu Rais, kwa unyenyekevu mkubwa tunakuja mbele yako kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyekuongoza vema mpaka ukatuletea Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wetu!

Kwa hili baba ubarikiwe sana! Umakini wake mtu huyu umeyarudisha matumaini ya Watanzania wengi waliokuwa wameanza kuichoka awamu ya tano ikingali changa. Wakati yeye anajifunza kutoka kwako, baba, huyu mtu ana kitu kikubwa ambacho nawe yakulazimu ujifunze kutoka kwake!

Alipozungumza na wafanyakazi wa chama cha wafanyakazi Tanzania alilitafakarisha sana Taifa kuhusu utawala wa sheria ambao ndiyo nguzo ya utawala bora. Anawaonya viongozi wenzake kutojichukulia sheria mkononi. Wameibuka baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakitenda au kutoa amri ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria au hazizingatii sheria na haki walizonazo raia katika nchi hii.

Amewataka viongozi wenzake kuacha mara moja tabia ya kutumbua majipu kwa kuwaachisha kazi wafanyakazi au kuwaweka ndani au kuwawajibisha wafanyakazi kwa namna yoyote ile bila kufuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.

Tunamwomba Waziri Mkuu afahamu kuwa kwa hili hayuko peke yake. Mama yetu Samia, Makamu wa Rais naye ametahadharisha mara kadhaa. Viongozi wetu hawa wakuu wametoa kauli hii baada ya kutoridhika na yanayoendelea nchini. Dhana ya utawala wa sheria na kujali utawala bora vimepuuzwa kwa kiasi kikubwa.

Hivi karibuni Watanzania wamepatwa na hali ya mfadhaiko wa kule Taifa linakopelekwa, baada ya baadhi ya viongozi kujaa kiburi ghafla na kuwa na jeuri kiasi cha kujifananisha na Mungu mwenyewe! Kiongozi anasema hadharani bila woga kuwa, “Huna wa kukutetea, mimi nikisimama mahala hapa, Mungu amesimama!” Kwa umri nilionao nimezisikia kauli nyingi kutoka kwa viongozi wetu, lakini kauli za kiongozi mpofu kama hii nilikuwa sijawahi kuisikia ikitolewa na kiongozi yeyote katika nchi hii! Yesu Kristu wakati wa mafundisho yake aliwajibu watu wake kwa maneno mawili tu, “Mjinga, wewe!”

Ndugu Rais, walisema Mwenyezi Mungu akikupa mkate mgumu hukupa na meno magumu ili uweze kuutafuna. Kassim Majaliwa ametokea wakati alipohitajika zaidi. Na hivi ndivyo ilivyoandikwa katika ukurasa wa 86 wa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu kuwa; “Ni desturi ya maisha kuwaficha watu wake bora mpaka tokeo kubwa litokee!”

Tumesoma katika maandiko matakatifu kuwa, wenye busara na hekima wakinyamaza, wajinga na wapumbavu huongezeka katika nchi; nayo nchi huangamia! Waziri Mkuu wetu hajanyamaza! Amesema atawashughulikia viongozi wote walio chini yake ambao kazi yao ni kulalamika tu na hasa wanapoona wameshindwa kutekeleza majukumu yao.

Kwa umakini mkubwa kabisa alisema; “Acha kulalamika unapoona umeshindwa kutekeleza majukumu yako…Nitaanza na wewe!”

Ndugu Rais, kiongozi mwenye upeo mdogo wa kufikiri hawezi kujua kuwa anapowachongea watumishi wenzake au kuwaumbua watendaji walio chini yake hadharani ndipo anapoonyesha jinsi alivyo dhaifu kiuongozi na kwamba amepwaya, hatoshi! Hawa wameiporomosha heshima ya kiongozi.

Baadhi yao wamekuwa kama vibarua tu!

Zamani tulifundishwa kuwa, ukimkaba baba yako au anayefanana naye unatenda dhambi kubwa! Na kwa dhambi hiyo Mwenyezi Mungu mwenyewe anakuandikia laana. Laana hiyo hata ungeoga vipi, utasuswa na kuwa chukizo hata kwa watu wako mwenyewe. Kumrudia Mungu ni kufanya kitubio. Hakuna njia za panya. 

Uliyemkaba naye akiendelea kunung’unika kimoyomoyo anakutengenezea laana ya ziada itakayosimama juu ya kichwa chako mpaka siku ya hukumu yako! Ole wake mtu yule atakayeweka matumaini yake katika mtu huyu! Ole wake kwa maana maandiko katika Biblia Takatifu yanasema, “Amtumaye mpumbavu, hujikata miguu na kunywa hasara!”

Ndugu Rais, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa uhai wake aliitembelea nchi ya Burundi. Huko baada ya kuulizwa swali, alinukuriwa akijibu kuwa; “Msidhani kuwa viongozi wapumbavu wako hapa Burundi peke yake, hata kwetu Tanzania viongozi wapumbavu wapo!”

Mwalimu Nyerere hakututajia hao viongozi wetu aliowaita wapumbavu, lakini sasa imekuwa ni kawaida kusikia maagizo na amri za baadhi ya viongozi wetu zinazoashiria utimilifu wa maneno hayo ya Baba wa Taifa.

Muda si mrefu wananchi watawabaini. Wako watendaji kadhaa wa Serikali ambao wamewekwa ndani bila utaratibu unaostahiki bali kwa amri tu ya ama mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa. Tumesikia mwalimu amelazimishwa na mkuu wa wilaya kupiga deki darasa zima mbele ya wanafunzi. Huyu angeweza hata kuwekwa ndani, nani angebisha? Watakapotokea watu wakasema huu ni wendawazimu tutakuwa na sababu zipi za kupinga tuhuma hizo?

Ndugu Rais, ziko kauli ambazo zinatolewa na baadhi ya viongozi wetu ambazo ukizitafakari unashindwa kujizuia kumkumbuka marehemu Didas Masaburi! Ah! Ukalale pema peponi Masaburi! Alisema wakati wake kuna baadhi ya viongozi walifikiri kwa kutumia makalio yao! 

Leo tunasikia kiongozi anasema; “Hawa ndiyo vichaa tunaohangaika nao;…ondoka hapa!” Bila kupewa nafasi ya kujitetea ambayo ni haki yake kama raia huru katika nchi huru yenye viongozi wenye heshima kubwa; masikini alimtii mungu-mtu akaondoka huku Taifa zima likiishuhudia ile aibu kubwa!

Baba, Kassim Majaliwa, Mzee Mwinyi aliuliza, yupo wapi kiongozi wa kukemea ujinga unaofanyika katika nchi? Mzee Mwinyi analia nchi kukatika usukani! Baba Majaliwa tumaini pekee ni wewe!

Ndugu Rais, nilisoma elimu ya jamii. Kitu ambacho kimewashinda wabobezi na wazamivu wa elimu ya jamii ni kuieleza jamii, ni kwanini vichaa wote huwaona wengine ambao si vichaa kuwa ndiyo vichaa? Jipitishe tu kwenye vilabu vya pombe; kila mlevi atakuona ni mlevi mwenzake!

Kumwita mtu kichaa hakumfanyi aliyeitwa kuwa kichaa, vinginevyo Kubenea atuambie, alipomwita mgomvi wake kibaka aliwahi kumwona akiiba chochote hata simu tu?

Baba Kassim Majaliwa na Mama Samia Suluhu Hassan tunawapenda viongozi wetu wote. Waelimisheni hawa kuwa jamii haimkatai kijana kwa ujana wake, bali kwa utoto au upuuzi wake! Msinyamaze! Mkinyamaza maandiko matakatifu yanasema; “Wenye busara na wenye hekima wakinyamaza wajinga na wapumbavu huongezeka katika nchi na Taifa huangamia!”

2298 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!