url-3Ulimwengu umeshtushwa na kifo cha Fidel Castro Ruz, aliyeongoza mapinduzi ya Cuba. Hata hivyo, wachache walishangazwa, kwani Aprili, mwaka huu Castro aliuambia Mkutano Mkuu wa Chama cha Kikomunisti kuwa wakati wake umefika, hasa kwa vile alikaribia umri wa miaka 90 na “kama ilivyo kawaida ya watu wote” naye hatakuwapo tena.

Huyu ni Kamanda Mkuu wa Mapinduzi ya Cuba ambaye wananchi walimuita “El Comandante Fidel.” Rais Raul Castro alitangaza kifo chake Novemba 26 na kwa mujibu wa usia aliouacha, mwili wake ulichomwa na majivu yake yakatembezwa nchini kote kabla ya kuzikwa katika makaburi ya Santiago de Cuba.

Kwa siku nne mamilioni ya wananchi wakajipanga nchini  kote na kutoa heshima zao za mwisho. Desemba 4 akazikwa mahali ambako alizikwa José Martí, shujaa wa Mapinduzi ya Cuba mnamo karne ya 19.

Kabla ya mapinduzi yaliyoongozwa na Castro mwaka 1959, Cuba ilikuwa ikitawaliwa na Jenerali Fulgencio Batista aliyekuwa dikteta na kibaraka wa Marekani. Cuba ilikuwa kisiwa cha kamari (casino), madanguro na vilabu vya matajiri kutoka Marekani. 

Ndipo Castro na vijana wenzake wakaanzisha vita ya msituni. Wakafanikiwa kuteka kambi ya kijeshi ya Moncada, lakini baadaye wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika mahakama, Castro alijitetea (yeye alikuwa mwanasheria) kwa kutoa hotuba ndefu akimlaani Batista na kusema ni yeye ndiye alipaswa kushtakiwa kwa udikteta wake na ukandamizaji wa wananchi. Mwishowe akasema “Sijali mkinifunga, kwani historia itanisafisha.”

Castro akatumikia kifungo. Baada ya kuachiliwa akapanga tena mapinduzi akishirikiana na wenzake kina Che Guevara. Wakampindua Batista Januari 1, 1959. Wafuasi wa Batista wakakimbilia Marekani na kuanzisha kikundi cha wapinga mapinduzi mjini Miami.

Tangu wakati huo Marekani ikafanya kila mbinu za kuishambulia Cuba na kuipindua serikali ya Castro. Wakavunja uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Cuba. Castro akalazimika kuomba msaada kutoka Umoja wa Kisovieti (USSR).

Mwaka 1961 Marekani ilitumia mamluki wakisaidiwa na manowari, mizinga na ndege vita kuishambulia Cuba, lakini njama hizo zikazimwa na wanamgambo wa Cuba. Hayo ni mashambulizi yanayojulikana kama Ghuba ya Nguruwe (Bay of Pigs).

Marekani ilifanya mipango ya kumuua Castro mara 634; na mara zote hizo wakashindwa. Njama hizi zilipangwa na shirika la kijasusi la CIA likisaidiana na kikundi cha Miami. Walitumia njia tofauti kama vile kumwekea sumu katika dawa, kumwekea sumu katika sigara (sigar), kuweka sumu katika nguo zake za kuogelea na hata kumwekea mabomu chini ya jukwaa alikokuwa akihutubia. Walijaribu hata kumwekea sumu katika kahawa.

Alipofika New York kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) alipewa sigar ambayo kama angeiwasha, basi ingemripukia na kumuua. Wakajaribu kumpulizia dawa ili ndevu zake zidondoke. Ni kwa sababu tangu alipokuwa msituni amekuwa akifuga ndevu na kuvaa kombati za kijeshi.

Mwaka 1976 Marekani ilitumia magaidi kuiripua ndege ya abiria ya Cuba na kuwaua wasafiri 78. Hawa ni raia wasio na hatia na wengi wao wala si raia wa Cuba. Magaidi wakakimbilia Marekani ambako wakapewa hifadhi.

Castro ni kamanda wa mapinduzi aliyekwepa majaribio zaidi ya 600 ya kumuua. Ameishi kiasi cha kuona marais tisa wa Marekani wakiingia na kutoka Ikulu (White House), kila mmoja akifanya bidii ya kumwondoa duniani bila ya mafanikio. Ni kuanzia Dwight Eisenhower, John F Kennedy, Lyndon Johnson, hadi Richard Nixon. Huyu Nixon peke yake alijaribu mara 184.

Inaelekea wakati Marekani wanajishughulisha na kumuua Castro walisahau kuwalinda marais wao. Mwaka 1963 siku Rais Kennedy alipouliwa, wakati huo huo jasusi wa CIA alipewa sindano yenye sumu ili kwenda kumuua Castro.

Mashambulizi ya Marekani dhidi ya Cuba yakaendelea kwa muda wa miaka 54 hadi Julai 2015 ndipo Rais Barack Obama wa Marekani akaamua kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Cuba. Hata hivyo, vikwazo vya kiuchumi vingali vinaendelea hadi leo.

Mazungumzo baina ya Cuba na Marekani yaliwezeshwa na Papa Francis kwa kuzikutanisha kisirisiri pande mbili. Machi 2015 Obama akazuru Cuba.

 

Castro atakumbukwa kwa mengi na wananchi wa Cuba. Kwa mfano, alianzisha mfumo wa matibabu bure kwa wote pamoja na elimu bure. Ni matibabu na elimu ya ngazi zote. Hii ni haki ya kila raia iliyoainishwa katika katiba ya nchi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliipongeza Cuba kwa kufuta ujinga. Hii ilifanyika kupitia kampeni kabambe ya kuwafundisha wananchi wote kujua kusoma na kuandika. Castro alikuwa na msemo: “Kama hujui basi jifunze;  kama unajua, fundisha”.

Lakini urithi mkubwa zaidi wa Castro ni jinsi alivyosaidia nchi za ulimwengu wa tatu, pamoja na Afrika. Mchango wake katika ukombozi wa Afrika utakumbukwa daima katika historia ya Bara hili.

Mapema mnamo miaka ya 1960 Cuba iliunga mkono vita ya ukombozi ya Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa. Si tu Cuba ilituma wanajeshi huko Algeria, bali pamoja na madaktari.

Tangu wakati huo Castro pia amesaidia nchi nyingine za Kiafrika kama Msumbiji,  Angola,  Zaire (leo DRC), Guinea-Bissau, Guinea, Equatorial Guinea, Sierra Leone na Libya. Cuba ilituma maelfu ya madaktari katika nchi za Kiafrika. 

Nje ya Afrika Castro pia alizisaidia nchi kama Yemen, Vietnam, Laos, Jamaica na Guyana.

Angola ndiko majeshi ya Cuba yalipigana kwa nguvu na kwa muda mrefu. Ni kwa sababu baada ya Ureno kujitoa kutoka Angola mnamo 1975, nchi hiyo ikaingiliwa na makaburu wa Afrika Kusini na dikteta Mobutu Sese Seko ambaye alikuwa kibaraka wa Marekani.

Oktoba 1975 majeshi ya makaburu wa Afrika Kusini yakaingia Angola yakisaidiwa na Marekani.  Nia yao ilikuwa ni kuuteka Mji Mkuu, Luanda na kuipindua serikali ya MPLA iliyokuwa ikiongozwa na RaisAugustino Neto na kuwatawaza vibara wao kina Holden Roberto na Jonas Savimbi.

Kwa kufanya hivyo walitaka kulinda na kueneza himaya ya makaburu na ubeberu katika Afrika. Vibaraka wao (kama Kamuzu Banda wa Malawi) wangetawala nchi kama Namibia, Angola, Zimbabwe, Zambia na Msumbiji.

Hizo ni njama zilizokuwa zikisukwa chini ya uongozi wa Henry Kissinger, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.

Nchini Angola, Rais Neto alikabiliwa na wapinzani wawili- Holden Roberto aliyesaidiwa na Mobutu, na Jonas Savimbi aliyesaidiwa na makaburu. Marekani ilikuwa msaidizi wao mkuu. Neto akaomba msaada kwa Castro, naye mara moja akatuma wanajeshi 4,000 kuilinda Angola.

Inakisiwa kuwa makaburu, wakisaidiwa na Marekani,  walikuwa na askari 60,000 ndani ya Angola, Cuba nayo ilituma wapiganaji 36,000.

Majeshi ya Angola yakisaidiwa na ya Cuba yalipambana na askari wa kikaburu kwenye daraja la Ebo. Walijificha msituni na kuwaachia makaburu wavuke. Katikati ya daraja wakawashtukizia na kuwashambulia. Askari wao 90 waliuawa na vifaru vyao saba viliteketezwa.

Machi 1988 mapambano makali yaliendelea maeneo ya Cuito Canavale nchini Angola. Majeshi ya makaburu yalilazimika kurudi nyuma.

Baada ya makaburu kuchapwa, wakasalimu amri. Wakalazimika kujitoa kutoka Angola na hata Namibia. Huo ukawa ni mwanzo wa kuporomoka kwa utawala wa makaburu.

Wapiganaji wa Cuba wakarudi kwao wakiwa wamewashinda makaburu na kusaidia ukombozi wa Angola, Namibia na Afrika Kusini.

Baada ya Afrika Kusini kujikomboa, Rais Nelson Mandela alitembelea Cuba na kutoa shukrani zake. Castro pia alialikwa kuhutubia Bunge la Afrika Kusini.

Mandela alisema wakati wa kutawaliwa na makaburu nchi ya kwanza kuombwa msaada ilikuwa Marekani. Siyo tu walikataa kuwasaidia wananchi wa Afrika Kusini, lakini hata hawakujali kujibu ombi lao.

Mandela alisema ndipo wakawasiliana na Cuba ambayo mara moja ikakubali. “Sasa nchi za magharibi wanatuambia eti tusiwe na urafiki na Casto. Huu ni upuuzi. Kama wamekasirika wakajinyonge,” alitamka Mandela.

Wakati wa mazishi ya Nelson Mandela, kati ya waalikwa wachache waliopewa fursa ya kuzungumza ni Raul Castro aliyemwakilisha Fidel.

Wakati makaburu walipoishambulia Angola, Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha azimio la kuwalaani. Marekani ikawalinda makaburu kama kawaida yao. Pia mwaka 1971 Mahakama ya Kimataifa (ICJ) ikatoa hukumu kuwa makaburu wanaitawala Namibia kinyume cha sheria za kimataifa.

Ikasema utawala huo ni haramu na hivyo wanapaswa waondoke haraka. Marekani ikawapa makaburu kiburi cha kupuuza hukumu hiyo. Baada ya hapo Baraza la Usalama la UN likapitisha tena Azimio Na. 435 la kuwalaani makaburu na kuwataka wajitoe Namibia. Kama kawaida, Marekani ikawaunga mkono makaburu.

Mwaka 1978 makaburu walifanya mauaji ya wakimbizi zaidi ya 600 katika kambi ya Cassinga nchini Namibia. Baraza la Usalama la UN liliwasilisha azimio la kuiwekea Afrika Kusini vikwazo. Marekani ilitumia kura yake ya turufu na ikazuia azimio hilo. Wakati huo Rais wa Marekani alikuwa Jimmy Carter.

Mwaka 1985 majeshi ya makaburu yalishambulia bomba la mafuta la Gulf Oil ndani ya Angola. Majeshi ya Angola yalifanikiwa kuzuia, lakini kama makaburu wangefanikiwa, basi wangekufa wengi, pamoja na raia wa Marekani waliokuwa wakifanya kazi hapo. Kwa mara nyingine Marekani iliwakingia kifua makaburu.

Majeshi ya Cuba na Angola yalifanikiwa kuwafurusha makaburu na vibaraka wao Savimbi na Roberto. Marekani ikapatwa na aibu kubwa. Ndipo wakaitisha mkutano wa amani jijini New York. Mnamo Desemba 1988 makubaliano yakatiwa saini. Makaburu wakakubali kujitoa siyo tu kutoka Angola, bali na Namibia.

Na huko Afrika Kusini nako kaburu P. W. Botha akalazimika kujiuzulu. Nafasi yake ikachukuliwa na De Klerk ambaye akaruhusu vyama vya siasa na akamfungua Nelson Mandela kutoka kifungo cha miaka 27 gerezani.

Julai 1991 Mandela akatembelea Cuba wakati wa sherehe ya mapinduzi. Alitoa shukrani zake kwa Cuba.

Alisema Cuba itakuwa na nafasi ya pekee katika mioyo ya Waafrika, kutokana na mchango wake katika kupigania ukombozi.

“Katika historia ya bara letu tumekuwa daima tukidhalilishwa na wageni. Ni mara ya kwanza tumeona wageni kutoka Cuba wakija kutusaidia kupigania ukombozi wetu”, akaongeza Mandela. 

Ndipo hivi majuzi, mjini Havana (Cuba) mamilioni ya wananchi walitoa heshima zao za mwisho kwa Castro huku wakitokwa machozi. Kutoka Afrika walifika marais wawili tu, nao ni Zuma (Afrika Kusini) na Mugabe (Zimbabwe).

Kutoka Algeria, Rais Abdelaziz Bouteflika alituma ujumbe akisema yeye binafsi amempoteza rafiki wa zaidi ya miaka 50. Alisema wananchi wa Algeria pia wamempoteza El Commandante. Marais wa Angola na Namibia nao hawakuhudhuria.

By Jamhuri