Mahakama ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga imemhukumu jela kifungo cha maisha, Ramadhani Bakari Iddi (46) mkazi wa Kilapula, Kata ya Ngomeni kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 13.

Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Geofrey Haule amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kujiridhisha pasi na shaka kuwa ametenda kosa hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Haule alisema Novemba 8, 2023 mshtakiwa alitenda kosa hilo la kumlawiti mtoto huyo baada ya kumrubuni kisha kwenda naye makaburini kwa lengo la kumtoa mashetani ndipo akafanya kitendo hicho cha kinyama kwa dhamira ovu.

Amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo mahakama imejiridhisha kuwa ametenda kosa hilo na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa jamii.

Aidha, Hakimu Haule amesema adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kifungu cha sheria 154 (1) (a) na 2 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 RE.2022.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa wakizungumza kwa nyakati tofauti waendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilayani Muheza, Joseph Njama na Michael Msangawale waliishukuru mahakama kwa kutoa adhabu hiyo kali kwa mtuhumiwa huyo.

Kwa mujibu wao adhabu hiyo ni fundisho kwa wale wote wenye nia ovu ya kutenda makosa hayo katika jamii na taifa kwa ujumla.

By Jamhuri