*Walimuuzia mteja vocha ‘feki’ ya Sh 5,000
*Mahakama yaamuru wamlipe Sh milioni 10

Na Mwandishi Wetu

Mtanzania Simon Mkindi, ambaye ni mkazi
wa Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam,
mwezi uliopita ameweka historia isiyofutika
nchini baada ya kuishtaki Kampuni ya simu
ya Airtel kwa kumuuzia vocha ‘feki’ ya Sh
5,000 akashinda kesi, na sasa anapaswa
kulipwa Sh milioni 10.
Kesi hii ya kihistoria ambayo inaweza
kuwaamsha Watanzania wengi kudai haki
zao mahakamani pale kampuni za simu
zinapowakata muda wa maongezi visivyo
au kuwauzia vocha zinazokataa kuingia
kwenye simu zao ilianza kunguruma mwaka
2014 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Dar es Salaam.
Mwaka 2014 Simon Mkindi alifungua kesi
Na. 379 dhidi ya Airtel (T) Ltd akidai fidia ya

Sh milioni 10 kutokana na hasara aliyopata
iliyotokana na makosa ya Airtel ambao ni
wamiliki wa mtandao aliokuwa anautumia
na vocha aliyoinunua afanye mazungumzo.
Mkindi aliiambia mahakama kuwa Julai 30,
mwaka 2014 alinunua vocha ya simu ya
Airtel ya Sh 5,000 Na. 1041405582666 kwa
nia ya kupata muda wa maongezi na kupiga
simu. Alipanga kujaza muda wa maongezi
katika simu yake Na. 0784 317995. Alijaribu
mara kadhaa kuingiza vocha hiyo bila
mafanikio.
Hata baada ya kupiga simu kwa namba ya
huduma kwa wateja Na. 100 kati ya mara
25 na 30 hakupata msaada huku
akishindwa kupiga simu zake za kibiashara.
Alieleza kuwa alipiga simu tena huduma
kwa wateja Agosti 11, 2014, Agosti 12,
2014 na Agosti 18, 2014, lakini mara zote
hizo alipuuzwa. Alikwenda ofisi za Airtel,
akaambiwa tatizo lingefumbuliwa, lakini
haikuwa hivyo.
Aliendelea kuwasiliana na Airtel kwa
kwenda ofisini kwao na kupiga simu bila
kupata ufumbuzi ndipo akaamua kwenda
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kutafuta haki yake. TCRA walimshauri
Mkindi kuwaandikia barua ya malalamiko

Airtel. Agosti 29, 2014 zikiwa ni siku karibu
30 tangu anunue vocha hiyo, aliwaandikia
barua ya malalamiko Airtel kama
alivyoshauriwa.
Septemba 2, 2014 Airtel walimwandikia
barua wakimtaka awasilishe vocha
aliyonunua. Septemba 4, 2014 aliwajibu
Airtel kwa barua aliyoitoa kama kielelezo
mahakamani na kuwapatia nakala
iliyothibitishwa ya vocha. Septemba 9, 2014
Airtel walimwandikia barua Mkindi
kumwomba radhi kwa usumbufu alioupata
na Septemba 10, 2014 vocha ikafunguliwa
na kuanza kutumika.
Baada ya mzunguko huo, Mkindi aliiomba
mahakama kuiamuru Airtel imlipe fidia kwa
usumbufu alioupata wakati anafuatilia vocha
hiyo na kuacha kazi za kumwingizia kipato.
Wakati shauri hilo linaendelea, Airtel
ilimtuma Isaac Nditi aliyejitambulisha
mahakamani kama ofisa aliyeshughulikia
tatizo la Mkindi. Nditi alikuwa na uzoefu wa
miaka saba kazini, hivyo aliiambia
mahakama kuwa: “Kuna nyakati inatokea
ambapo mteja anataka kuweka muda wa
maongezi (kwenye simu yake)
inashindikana kutokana na makosa ya
kiufundi.”

Katika kuitetea Airtel, akasema kampuni
hiyo huuza vocha milioni 3.5 (hakusema
kwa muda gani), na wastani wa asilimia 1,
huwa zinagoma kuingia kwenye simu.
Akaongeza kuwa mteja anapoweka vocha
ikagoma anapaswa kupeleka vielelezo Airtel
au kutoa namba za vocha. “Tatizo
linapotolewa taarifa hutatuliwa ndani ya saa
72,
” Nditi aliiambia mahakama.
Kutokana na maelezo ya Nditi na ushahidi
wa maandishi aliouwasilisha Mkindi,
Mahakama ya Kisutu iliitia hatiani Airtel
kuwa ingawa utaratibu wao ni kumaliza
tatizo ndani ya saa 72, vocha ya Mkindi
iligoma Julai 30, 2014 na tatizo lilifumbuliwa
Septemba 10, 2014.
Akitoa hukumu Aprili 27, 2017, Hakimu
Mkazi G. A. Mwambapa, baada ya kusikiliza
pande zote alisema: “Mahakama imeridhika
kuwa mlalamikiwa (Airtel) walichangia
ucheleweshaji katika kujaza muda wa
maongezi. Mlalamikaji ameiambia
mahakama kuwa ni mfanyabiashara.
Alitumia muda wake muhimu kumsukuma
mlalamikiwa kufanya kazi yake kwa karibu
mwezi mmoja na nusu, wakati hakustahili
kufanya hivyo kama mlalamikiwa
angetimiza wajibu wake kwa wakati.

“Mahakama hii inafahamu kuwa katika
dunia ya kisasa ya mawasiliano na
matumizi ya ‘data’

, nguvu ya mawasiliano ni
kubwa mno. Kumzuia mteja kutumia muda
alioulipia kunaweza kusababisha hasara
kubwa na kwa kiasi fulani mteja anaweza
kujikuta anapata hasara au anapoteza
jambo kwenye biashara yake.
“Kwa maana hiyo, mlalamikiwa anapaswa
kutambua hatari inayotokana na uzembe
wake kwa gharama ya mteja. Kwa hiyo
natoa fidia ya jumla ya Sh milioni 10 kwa
mlalamikaji na gharama za kesi.”
Baada ya hukumu hiyo Airtel walikata rufaa
Mahakama Kuu kwa kufungua kesi Na. 129
ya mwaka 2017. Mahakama Kuu baada ya
kupitia hukumu na kuzisikiliza pande zote
mbili kwa maandishi, iliithibitisha hukumu ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji W. P. Dyansobera katika hukumu
aliyoitoa Agosti 1, 2018 amesema mrufani
ameshindwa kuthibitisha makosa
yaliyotendwa na Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu katika kufikia uamuzi wa
kumpa tuzo ya Sh milioni 10 ndugu Mkindi,
hivyo akaifukuza rufaa hiyo na kuongeza
kuwa mrufani anapaswa kumlipa Mkindi
gharama za kesi alizoingia wakati

anashughulikia rufaa.
JAMHURI limeutafuta uongozi wa Airtel
kuzungumzia kesi hii bila mafanikio, ila
taarifa za uhakika lilizonazo ni kuwa
mwishoni mwa mwezi uliopita Airtel
wameingia makubaliano ya kumlipa Mkindi
hizo Sh 10,000,000 na gharama za kesi.
Uamuzi huu umethibitisha kuwa wananchi
wanaokatiwa mawasiliano ya simu au
kuuziwa vocha zikashindikana kuingia
wanayo haki ya kudai fidia kwa hasara
wanayopata kwa kukosa mawasiliano katika
kipindi ambacho vocha inakuwa haiingii.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share