Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel,
amefanya ziara barani Afrika kwa
kuzitembelea nchi za Ghana, Mali, Niger,
Ethiopia, Misri na Senegal.
Ziara hiyo ilikuwa yenye kuzungumzia
changamoto ya uhamiaji haramu na
kuimarisha uhusiano wa kibiashara.
Akiwa nchini Ghana kiongozi huyo
amekutana na Rais Nana Akufo-Addo, jijini
Accra kujadili namna nzuri
itakayoziwezesha nchi hizo kuimarisha
maendeleo ya kiuchumi pamoja na
kupambana na uhamiaji haramu.
Kabla ya ziara hiyo Merkel amesema
kupitia ujumbe wake wa video kwamba ni
muhimu kwa viongozi wa Afrika na Ulaya
kuanza kutafakari na kujiuliza namna ya
kuimarisha mapambano dhidi ya uhamiaji
haramu.
Akiwa nchini Senegal alitarajiwa
kuzungumzia uwepo wa haja ya kukabiliana

na uhamiaji haramu na watu wanaofanya
biashara haramu na kuongeza kuwa nchi
yake haiwezi kuwa mshirika wa nchi
zinazowahifadhi wanaofanya biashara
haramu na kuvumilia bila kuchukua hatua.
Rais wa Senegal, Macky Sall, ameonyesha
kusikitishwa kwake na hatima ya wahamiaji
wanaopoteza maisha kila mara wakati wa
kuvuka Jangwa la Sahara na Bahari ya
Mediterranean na kutoa wito wa kutafutwa
suluhisho na kubuniwa fursa kwa vijana
barani Afrika.
Amesema iwapo mataifa ya Afrika
yataweza kuleta maji, umeme na kujenga
mazingira mazuri ya kuishi, vijana
hawatahitaji kuondoka kwenda kutafuta
maisha bora barani Ulaya na kuongeza
kuwa jawabu la kweli ni kwa Afrika kutafuta
suluhisho la changamoto zilizopo.
Katika ziara hiyo pia Merkel alitarajiwa
kukutana na Rais wa Jumuiya ya Kiuchumi
ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS),
Jean-Claude Broun na kufanya
mazungumzo na Rais Muhammadu Buhari
wa Nigeria kuhusu maendeleo ya kijamii na
kiuchumi nchini humo.
Katika siku za karibuni Kansela Merkel
amepoteza uungwaji mkono wa kisiasa
tangu alipochukua uamuzi wa
kuwakaribisha wahamiaji nchini Ujerumani,

huku Chama chake cha Christian
Democratic Union (CDU), kikipitia kipindi
kigumu kuliko wakati mwingine wowote.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share