Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

Watu tisa wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na lori la mizigo, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema ajali hiyo ilitokea Machi 10, 2024, majira ya saa 11:15 jioni, eneo la Kilomo, Wilaya ya Bagamoyo katika Barabara Kuu ya Bagamoyo Dar es Salam.

Amesema gari lenye nambari za usajili T. 503 DRP lenye tela namba T733DUQ, lori aina ya Howo likiendeshwa na Dereva Apolo, Isdor Mgomela (52) liligonga uso kwa uso gari ya abiria aina ya Coaster yenye namba za usajili T. 676 DSM likiendeshwa na dereva Juma Mackey na kusababisha vifo hivyo na majeruhi.

“Watu Tisa wamefariki ikiwemo madereva wa magari yote mawili, gari aina ya Coaster ilikuwa ikitokea Bagamoyo kuelekea Dar es Salam na Lori lilikuwa likitokea Dar es Salam kwenda Bagamoyo,” amesema Kamanda Lutumo.

Aidha amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori kuyapita magari mengine pasipo kuchukua tahadhari jambo lililosababisha kwenda kugonga gari ya abiria uso kwa uso na kusababisha vifo hivyo.

By Jamhuri