Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke(TRRH) imefanya upasuaji wa kuondoa uvimbe katika kizazi, maarufu kama myoma. Myoma ni uvimbe usio wa saratani unaojitokeza kwenye kizazi, na hutokea kwa wanawake waliopo katika umri wa kuzaa. Upasuaji huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa baada ya Vicky Malissa, ambaye alitembelea hospitali mbalimbali ndani na nje ya nchi, bila kupata matibabu.

Malissa alishauriwa kuondoa kizazi kutokana na ukubwa wa uvimbe huo, lakini baada ya kufika Tanzania, alipokelewa na madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke (TRRH) ambao walifanikiwa kumfanyia upasuaji wa kuondoa uvimbe bila kuondoa kizazi.

Kupitia changamoto alizopata katika kuhangaikia matibabu, Malissa amewashauri wananchi kuamini kuwa wataalamu na huduma bora za afya zipo nchini, na kuwataka kufika hospitalini hapo wanapokumbana na changamoto za kiafya kama yake.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joseph Kimaro, ameeleza kuhusu ugonjwa wa myoma na jinsi vipimo vilivyofanyika vilivyoonyesha uwepo wa uvimbe huo.

Amebainisha kuwa mgonjwa alipata shida kupata matibabu hadi kufikia hatua ya kushauriwa kuondoa kizazi. Dr. Kimaro ametoa shukrani kwa serikali kwa kuwekeza katika sekta ya afya, kuwezesha upatikanaji wa vifaa tiba na mabingwa, hivyo kufanikisha upasuaji huo.

Aidha, Daktari Bingwa wa Mionzi, Mawimbi Sauti na Sumaku, Dkt. Ikupa Mwasumbi amethibitisha maendeleo mazuri ya mgonjwa mara baada ya vipimo vya Mawimbi sauti(ultra sound) kuonyesha kutoweka kwa uvimbe wote. Amehimiza jamii kufika hospitalini mapema wanapokumbana na changamoto za kiafya, kwani matibabu yanaweza kufanyika kwa wakati na kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Malissa ameonyesha furaha yake na kuwashukuru madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke kwa mafanikio ya upasuaji wake, na kutoa wito kwa wanawake wengine kutafuta matibabu hapa nchini kwanza kabla ya kwenda nje ya nchi.