Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia kijana aitwaye Paschal Msindo (21), mkazi wa Kijiji cha Kalepula Wilaya ya Kalambo kwa tuhuma za kumuua baba yake kwa kumkata shoka shingoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 1, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Shadrack Masija, amesema kuwa lilitokea Oktoba 29, majira ya saa 7, mchana ambapo kijana huyo alimkata na shoka shingoni baba yake mzazi aitwaye January Msindo (83) na kumuua papo hapo.

Amesema kuwa kabla ya tukio hilo mzee Msindo alikuwa amechota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ambayo aliyafuata umbali mrefu kutokana na changamoto ya ukame kwani visima vingi vimekauka kijijini hapo.

Kamanda Masija amesema kuwa baada ya mzee huyo kuchota maji ndipo kijana wake alitaka kuchukua maji hayo kwa ajili ya matumizi yake ndipo baba yake alipo mkatalia na kumtaka akachote maji yake jambo lililomkasirish kijana huyo.

Kijana huyo aliingia ndani na kuchukua shoka kisha kumvamia baba yake na kumkata mara mbili shingoni na kumsababishia jeraha kubwa lililomsababishia damu nyingi kutoka na kufariki muda mfupi kabla ya kupatiwa matibabu.

Kamanda huyo amesema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kufanya mauaji hayo alikimbilia porini lakini Polisi walianza msako kwa kushirikiana na wananchi na walifanikiwa kumkamata akiwa amejificha porini.

Amesema kuwa kijana anashikiliwa na Polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji hayo mara tu baada ya upelelezi wa awali kukamilika.