Hapa nchini Tanzania nadhani hata huko ughaibuni kwenye nchi zinazojulikana kama za ulimwengu wa kwanza, wananchi wanazungumzia uwepo wa vyama vya siasa na demokrasia.

Vyama vyenyewe kwa asili yake vilianza wapi na vilianza namna gani katika nchi zile, haijaelezwa wazi. Wale wenzetu walioendelea kule Magharibi bado wanaamini wana wajibu wa kuviangalia vyama vya siasa katika nchi huru za Afrika.

Ndiyo sababu kukiwa na uchaguzi mkuu katika nchi huru zote za Afrika, utasikia kuwa tume za uangalizi kutoka Umoja wa Mataifa (UN) au Umoja wa Ulaya (EU), wanaoitwa “international observers” wanatumwa kuja kuangalia namna demokrasia wanaoijua wao imekua kwa kiasi gani.

Kwa nchi zetu za Kiafrika ndiyo hasa hivyo vikundi vinakuwa vingi. Mathalani kule Zimbabwe; Julai 30, mwaka huu kulikuwa na waangalizi (observers) kutoka nchi huru za Afrika (AU), Umoja wa Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADAC), EU na UN.

Loo! “Observers” wote hawa wa nini? La msingi, demokrasia katika nchi zinazoendelea haiaminiki! Hivyo, waliobobea katika suala la demokrasia lazima waje wathibitishe. Basi, wanajiona kama vile wana wajibu wa kuja kuangalia sisi tusioendelea tunafanyaje.

Mbona ulipotokea uchaguzi mkuu kule Marekani, kati ya Bibi Clinton na tajiri Trump suala hili la “International Observers” halikuwapo? Kumekuwa na uchaguzi Ufaransa (2017) na kule Urusi (2018) au Ujerumani (2018) na Italia (2017) mbona haikusikika wametumwa waangalizi kutoka AU, au EU au UN? Ndiyo kusema huko kwa wenzetu waangalizi hawahitajiki? Kama hivyo ndivyo, tujiulize kwanini hawa “International Observers” hawahitajiki kule, lakini wanahitajika huku kwetu Bara la Afrika?

 

Basi hiki ni kisasili (myth) tu kimejengeka miongoni mwa wakubwa- Wazungu hawa. Kuwa demokrasia kwao haina dosari maana imeanza huko, sisi tuliletewa tu na wakoloni na hivyo lazima waisimamie wao. Nasi kwa unyonge wetu “inferiority complex” tukaipokea hali ile mpaka leo hii.

Azimio la Arusha linasema, “…Tumeonewa kiasi cha kutosha, Tumenyonywa kiasi cha kutosha na Tumepuuzwa kiasi chakutosha…”

“…unyonge wetu (inferiority complex) ndiyo uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa…Si ndio hayo tunayoyaona sasa toka kwa Wazungu?

Lakini kule nchi za Ulaya na Marekani hii democrasia, na mambo ya vyama vya siasa viliibukaje? Nani aliwapa hawa Wazungu hati miliki ya demokrasia ambayo kwao wanaamini lazima watufundishe sisi na kutusimamia?

Hili Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliita “Jeuri ya Kikoloni”. Hebu jaribu kusoma tena ile hotuba ya Mwalimu Nyerere aliyotoa Dar es Salaam Siku ya Kumbukumbu ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 09 Desemba, 1978 wakati tukiwa katika maandalizi ya vita ya kumng’oa nd