Na Lilian Lundo na Veronica Simba, JamhuriMedia, Kagera

Vijiji 512 kati ya Vijiji 662 vya Mkoa wa Kagera ambayo ni sawa na asilimia 77.3 ya vijiji vya mkoa huo vimepata huduma ya umeme kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikiwemo Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, REA Awamu ya Pili na REA Awamu ya Kwanza.

Vijiji 150 ambavyo bado havijaunganishwa na umeme mkoani humo, vitaunganishwa na umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, ambapo tayari mkandarasi anaendelea na kazi za mradi huo.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema jumla ya shilingi bilioni 80 imetolewa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa umeme vijijini mkoani humo.

“Kupitia Wakala wa Nishati Vijijini ndani ya Mkoa wa Kagera imewekeza shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini, na hivi ninavyoongea ndani ya mkoa huu kuna miradi mitano inatekelezwa,” amesema Mhandisi Saidy wakati wa hafla wa uwashaji wa umeme Kijiji cha Mubaba, wilayani Biharamulo.

Aidha, viongozi na wananchi wa mkoa huo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Hassan kwa kuwawezesha kupata umeme wa uhakikia, ambao utafungua fursa mbalimbali katika maeneo yao.

“Tangu umeme wa REA umeingia kijijini, tayari watu wameshanunua ‘fridge’, watu wameshaanza kutafuta mashine za umeme kwa ajili ya kusaga, hata mashine za kutoa ‘photocopy’ tumeanza kupata,” amesema Diwani wa Kata Murusagamba iliyopo Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, Mhe. Sudi Mkubira

“Umeme wa REA umetusaidia kupata mashine za kukoboa mpunga za umeme, kabla ya kuja umeme huu tulikuwa tukikoboa mpunga kwa kutumia mashine za mafuta ambazo zilikuwa zinasababisha mchele kuwa mweusi hivyo tulikuwa tukikosa wateja,” amesema Mfanyabiashara wa Mchele, Kalebo John kutoka Kijiji cha Mubaba kilichopo Kata ya Kaniha, Wilaya ya Biharamulo, mkoani Kagera.

Katika kuhakikisha kila kijiji mkoani humo kinapata umeme, kwa sasa REA inatekeleza miradi mitano mkoani humo, ambayo ni Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mradi wa Kupeleka umeme Pembezoni mwa Miji, Mradi wa ujazilizi, Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo, na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji. 

Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko yupo kwenye ziara ya kuwasha umeme katika vijiji vya mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora na Singida, ziara hiyo imeanza Septemba 26, 2023 mpaka Octoba 8, 2023.

By Jamhuri