Waandamanaji wanaoipinga Serikali nchini Kenya walirejea barabarani wakiongeza madai ya kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu licha ya mabadiliko yake ya hivi majuzi.
Mwanamume mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama viungani mwa mji mkuu, mwandishi wa BBC katika eneo hilo anasema.
Katikati ya jiji la Nairobi, maduka yalisalia kufungwa huku polisi wakifyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya waandamanaji.
Maandamano hayo yalianza mwezi uliopita kupinga mswada wa ushuru ambao haukupendwa na watu wengi, na kutoka wakati huo umeondolewa na rais.
Lakini yamekuwa yakiendelea kutokana na hasira zaidi juu ya utawala mbaya, rushwa na uwajibikaji wa polisi kutokana na vifo vya makumi ya waandamanaji katika maandamano ya hivi karibuni.
Wiki iliyopita, Rais Ruto alitoa wito wa “mazungumzo” huku akifuta baraza lake lote la mawaziri na mkuu wa jeshi la polisi kujiuzulu.
Harakati za maandamano hayo kwa kiasi kikubwa zinaratibiwa mtandaoni na vijana wa Kenya, ambao wengi wao wamekataa mazungumzo na wanamtaka Bw Ruto “aondoke” madarakani.
Umati wa watu ulibeba mwili wa muandamanaji aliyeuawa Jumanne huko Kitengela, kusini mwa Nairobi, hadi kituo cha polisi kilicho karibu. Jeshi la polisi halijazungumzia kifo cha mtu huyo.
Waandamanaji hao waliimba “Ruto lazima aende”, waliwasha moto barabarani na kurusha mawe walipokuwa wakipambana na polisi, mwandishi wa BBC katika eneo la tukio anasema.
Ghasia pia zilishuhudiwa katika maeneo mengine ya nchi, yakiwemo Mombasa, Kisumu, Nakuru na Nyeri.
Makumi ya watu wameuawa hadi sasa tangu kuanza kwa maandamano hayo, huku shirika linalofadhiliwa na serikali likisema idadi ya vifo vilivyotokea kutokana na maandamano hayo si chini ya watu 50 huku wengine 413 wakijeruhiwa.
Mapema Jumanne, kaimu mkuu wa polisi alisema kulikuwa na “intelijensia ya kuaminika” kwamba “makundi fulani ya wahalifu waliopangwa” yalikuwa yamepanga “kupenya, kuvuruga na kuhatarisha” maandamano hayo.