Azam FC italazimia kuifunga Simba leo ili kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake baada ya jana kufungwa na URA bao 1-0

Mabingwa watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi leo wameonja joto ya michuano hiyo baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0, kutoka kwa URA ya Uganda katika mchezo mkali wa kundi A, uliopigwa majira ya 10, kwenye uwanja wa Amaan Zanzibar.

Kipigo hicho kwa Azam kimeifanya URA kuongoza kundi hilo wakifikisha pointi saba na kuwashusha Azam kwenye nafasi ya pili wakibakiwa na pointi zao sita huku kesho wakitarajia kupambana na Simba.

Mshambuliaji Kagaba Nicholas, ndiyo alifunga bao hilo pekee dakika ya 3e baada ya kuachia shuti kali lilimshinda kipa wa Azam FC Benedict Haule na mpira kutinga wavuni.

Azam inayonolewa na kocha Mromania Aristic Cioaba, ilipambana kusawazisha bao hilo ambapo mara kadhaa washambuliaji wake Enock Atta, Idd Kipagwile na Paul Peter walishindwa kuzitumia vizuri nafasi walizozipata kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Azam walianza kwa kufanya mabadiliko ya kumtoa Kipwagile na kumuingiza Bernald Authur, ambaye alikwenda kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la URA, lakini timu hiyo ilionyesha kujipanga vuema na kuwadhibiti ipasavyo Azam.

URA mabingwa wa mwaka 2015 wa michuano hiyo walionekana kucheza vizuri na kuutawala mchezo huku wakiwasumbua vilivyo wapinzani wao Azam ambao walibadilisha mfumo na kutumia mipira mirefu lakini haikuwa rahisi kwao kuweza kusawazisha bao hilo la Kagaba.

Katika dakika za nyongeza Azam FC ilipata pigo kwa mshambuliaji wake Atta Agyei kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kwa makusudi mshambuliaji wa URA Lwasa Peter.

Baada ya kadi hiyo Azam walionekana kupoteza mwelekeo na URA kuendelea kuutawala mchezo na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Azam lakini hawakuweza kufunga bao la pili hadi dakika 90 za mpambano huo zinakamilika.

By Jamhuri