“Mara nyingi ninapoendesha gari katika mitaa ya Jiji la Arusha, nalazimika kutumia akili nyingi. Hadi naondoka mjini huwa ninahisi uchovu wa kufanya kazi nzito ya kutumia akili.”

 

Hayo ni maneno ya dereva wa gari kutoka mjini Moshi. Maneno haya yananishawishi kufanya utafiti mdogo kujua jinsi wanavyomudu kazi hiyo wakiwa jijini Arusha.

Ninafanikiwa kubaini jinsi baadhi ya madereva wanavyoendesha magari jijini Arusha bila kufuata sheria za barabarani.

 

Kama ilivyo katika miji na majiji mengi, Jiji la Arusha lina taa za kuongoza magari katika makutano ya barabara maeneo ya Sanawari, Mianzini, Stendi Kuu, Friends Coner na Kona ya Esso.  Katika maeneo haya baadhi ya madereva wanapokuta taa nyekundu zinazotaka wasubiri, wao huzipuuza kwa kulazimisha kuyapita magari yanayosubiri kuruhusiwa na taa za kijani.

 

Baadhi ya madereva hupita kwa mwendo kasi katika maeneo zilipo taa hizo, kiasi cha kuhatarisha maisha ya watumiaji wengine wa barabara wakiwamo waendesha pikipiki na watembea kwa miguu.

 

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa Mkoa wa Arusha, Marison Mwakyoma, anakiri kuwapo kwa tatizo hilo, lakini anasema kwamba tayari dawa yake imeshaiva na ofisi yake itaanza kuifanyia kazi siku chache zijazo.

 

Akitolea ufafanuzi tatizo la madereva wasiotii sheria za barabarani, Kamanda Mwakyoma anawataka madereva wa vyombo vyote vya moto na watembea kwa miguu kufuata na kutii sheria bila shuruti na alama za barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima.

 

Anasema kumekuwapo na tatizo la baadhi ya madereva wanaokaidi sheria na alama za barabarani na kusababisha ajali ambazo zingeepukika.

 

“Madereva wengi wanafanya makusudi, ama wanakuwa walevi wakati wanaendesha magari, au hawataki kuelewa. Kwa kuwa tumewaelimisha vya kutosha na hawataki kuelewa, basi kinachofuata ni kuwachukulia hatua kali za kisheria,” anasema Kamanda Mwakyoma.

 

Anafafanua kuwa Kikosi cha Usalama Barabarani kimejipanga kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva wanaokiuka sheria za barabarani katika maeneo ya taa za kuongoza magari.

 

“Kwa sasa dereva atakayekutwa na kosa la kupita kimakosa kwenye taa za kuongozea magari atatozwa faini ya Sh. 30,000, na akirudia  makosa hayo zaidi ya mara tatu atafutiwa leseni yake ya kuendesha gari,” anasema Kamanda Mwakyoma.

 

Adhabu hiyo, kwa mujibu wa Kamanda Mwakyoma, itafuatana na mkakati wa kuweka doria maeneo husika na kuwakamata madereva wanaokokaidi kutii taa za kuongoza magari.

 

“Tukikukamata tutakupeleka sehemu husika na utachukuliwa hatua kali za kisheria. Hata hivyo, tangu taa zifungwe ufanisi mkubwa umeonekana kutokana kupungua kwa ajali nyingi.

 

“Lakini pia kwa wanafunzi wanaovuka barabara kwa miguu wamewekewa mradi wa kuvuka kwa kutumia vibao vyenye alama ya barabarani,” anasema.

 

Kwa upande mwingine, madereva wanasema baadhi yao wanaoendesha magari jijini Arusha hawajahudhuria mafunzo ya udereva.

 

Dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya Njiro na katikati Jiji la Arusha, aliyejitambulisha kwa jina la Alfred Kibwereza, anasema madereva wengi ni ambao wamejifunza magari katika mazingira tatanishi.

 

“Madereva wengi unaowaona hawajapata mafunzo ya udereva wala elimu ya udereva, hawa wamejifunzia mitaani ndiyo maana hawatii sheria na alama za barabarani,” anasema Kibwereza.

 

Dereva huyo anatoa wito kwa Serikali kuangalia uwezekano wa kuandaa mafunzo kwa madereva wa magari, hususan kuhusu uelewa na matumizi ya taa za barabani.  Tatizo la baadhi ya madereva wa magari na pikipiki kutojua matumizi ya usalama lipo pia kwa watembea kwa miguu.

 

Mkazi wa jijini Arusha aliyejitambulisha kwa jina la Maria John (Ntilie), anasema amekuwa na mazoea ya kuvuka barabara kabla taa hazijaruhusu kutokana na taa hizo kuchukua muda mrefu kuruhusu, lakini pia baada ya kuona baadhi ya madereva wa magari na pikipiki wakifanya hivyo.

 

“Hizi taa zinachelewa sana kuwaka, sasa unakuta wakati mwingine baadhi ya watu tunakuwa na haraka, hivyo tunalazimika kupishana na magari na pikipiki wakati wa kuvuka.

 

“Sijawahi kufundishwa na wala sijui matumizi ya taa za barabarani, hivyo nimekuwa nikijivukia tu, na hili si kwangu pekee, watembea kwa miguu wengi hatujui jambo hilo.  Naomba maofisa wa usalama barabarani watupatie elimu sisi watembea kwa miguu ili kuepuka ajali za mara kwa mara,” anasema Maria.

 

Hata hivyo, Kamanda Mwakyoma anasema Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani linaendelea kuweka mikakati itakayowezesha watu wengi wakiwamo madereva na watembea kwa miguu, kuelimishwa sheria na matumizi ya taa na alama za barabarani.

 

Please follow and like us:
Pin Share