Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania limepitisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa fedha wa 2023/2024,ya Shilingi Trilioni 44.39 kwa kura 354 kati ya kura 374 zilizopigwa ambapo kura 20 ni za wabunge ambao hawakuwa na uamuzi na hakukuwa na kura ya hapana.

Idadi hiyo ya kura za ndio ni sawa na asilimia 95 ambapo Miongoni mwa wabunge waliounga mkono bajeti hiyo ni wabunge watatu wa vyama vya upinzani ambao ni wabunge wa viti maalum Nusrat Hanje na Salome Makamba kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),na mbunge wa Mtambile Seif Salim Seif wa Chama Cha ACT Wazalendo na

Akihitimisha hoja Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba amesema katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, fedha zinazokwenda katika wizara,mikoa, wilaya na majimbo ni fedha nyingi ambazo hazijawahi kutokea tangu Uhuru na kusisitiza kuwa hakuna wizi serikalini.

Katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge wengi walihoji kuhusu tozo ya Shilingi 100 kwenye mafuta ya Petroli na Dizeli ambapo Dokta Mwigulu amesema tozo hiyo ni jambo jema kwa sababu linakwenda kutunisha mfuko wa mapato kwa serikali na hivyo kuiwezesha kutekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii.

Katika hatua nyingine Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2023 ambao pamoja na mambo mengine una lenga kuzifanyia marekebisho sheria zipatazo 18 ili kufanikisha utekelezaj iwa bajeti hiyo.
Wabunge walianza kupiga kura saa 5:30 asubuhi baada ya hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba.

Kulingana na kanuni za Bunge zoezi hilo lililotanguliwa na mwongozo wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akinukuu ibara ya 90 (2) (b), wabunge walipiga kura ya wazi kwa kila mmoja kuitwa jina lake na kujibu ndiyo kwa wanaokubali na wengine wachache kuitikia ‘abstain’ (hawakubali wala hawakatai) akiwemo Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.

By Jamhuri