Balaa Magomeni Kota

Na Alex Kazenga,JamhuriMedia, Dar

Licha ya ahadi ya serikali ya kuwapa kipaumbele wakazi ‘asilia’ wa Magomeni Kota kupata makazi katika majengo ya kisasa, takriban familia 21 zimetoswa; JAMHURI limebaini.

Familia hizo ni miongoni mwa 644 zilizolazimika kulihama eneo la Magomeni Kota mwaka 2011 kupisha mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa.
Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wakazi waliokosa ‘nyumba mpya’, Paul Likule, anamsukumia lawama Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Majengo ya Magomeni Kota, George Abel, aliyechaguliwa na wakazi wa Magomeni kusimamia na kuratibu uhakiki wa majina ya wamiliki wa nyumba za awali (asili) za Magomeni Kota.

Likule anasema Abel kwa kushirikiana na mtandao ndani ya Wakala wa Majengo (TBA), wamemdhulumu haki yake, akidai kuwa mwaka 1979, shemeji yake, Hirtruda Kessy, alimmilikisha nyumba Na. 460.

Hayo yalitokea baada ya Hirtruda, aliyekuwa akifanya kazi NBC kustaafu utumishi wa umma na kuhamia Arusha.

“Ajabu leo TBA wananiambia iliyopaswa kuwa nyumba yangu (kwenye majengo mapya matano) wameichukua, hawawezi kunipa ufunguo kwa sababu wamebaini inamilikiwa na watu wawili.

“Mimi tangu nikabidhiwe hiyo nyumba sijawahi kubadilisha umiliki wake. Jina linalotambulika hadi TBA ni la shemeji (Hirtruda) ambaye katika suala hili halalamiki wala hajawahi kuweka zuio nisipewe funguo. Sasa huyo mmiliki wa pili ni nani hata kuzuiwa nisitendewe haki?” amehoji Likule.
Anasema mwaka 2011 wakati wa kuhakiki majina na kupewa fedha kupisha mradi, alikuwa mmoja wa wakazi waliopokea malipo kutoka serikalini kuwawezesha kutafuta makazi ya muda.

Lakini sasa hayumo katika orodha ya wanaopaswa kuishi kwenye maghorofa mapya na anasema: “Ninashangaa leo serikali ile ile iliyonipa fedha awali inanibagua!”

Hata hivyo, anasema amefuatilia suala hilo na kubaini kuwa Abel ndiye aliyepewa nyumba hiyo, akitumia nafasi yake (uenyekiti wa kamati) kupotosha taarifa nyingi za wamiliki wa nyumba za Magomeni Kota.

Bibi azushiwa kufariki dunia

Katika harakati za kuhakikisha na wao wanakuwa wamiliki wa nyumba katika maghorofa hayo yaliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Machi mwaka huu, vijana wawili wanadaiwa kughushi hati ya kifo (death certificate) ya shangazi yao, Fatuma Omari (68), aliyekuwa mmiliki halali wa nyumba ya awali.

Akizungumza na JAMHURI, Arafa Almas, mtoto wa bibi Fatuma anayeishi naye katika chumba kimoja kilichopo nyumba Na. 256 B, Kiwanja Na. 1,000, Kitalu cha Pili, Magomeni, anasema chumba kingine ndani ya nyumba hiyo wanaishi Juma na mdogo wake Makalani; watoto wa mjomba wake, Said Mustafa, wanaodaiwa kughushi hati ya kifo.

Mustafa naye anamiliki nyumba Magomeni Kota akiwa amepewa na baba yake, huku dada yake, Fatuma, akirithishwa nyumba na baba yao.

“Hofu imemjaa mama yangu. Anadhani hawa vijana watamfanyia jambo baya ili kutimiza azima yao ya kumiliki nyumba.

“Haya yote yamesababishwa na TBA kwa kutokuwa makini. Wakati wa ugawaji nyumba, walikwenda Temeke alikokuwa amepanga, wakaiba nyaraka za umiliki wa ile nyumba ya awali, wakazipeleka TBA wakidai mama (shangazi yao) alikwisha kufariki dunia,” amesema Arafa.

Anadai kuwa vijana hao kwa kushirikiana na watu wengine walighushi hati ya kifo, na kwa kuwa mama yake alishindwa kufika Ofisi ya Manispaa ya Kinondoni siku ya uhakiki wa majina ya wamiliki wa nyumba kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya miguu, wakachukua nafasi hiyo kuwathibitishia wahakiki kuwa Fatuma amekwisha kufariki dunia wao ndio wamebaki wakisimamia umiliki.

Hata hivyo alipopata nafuu bibi Fatuma alikwenda manispaa kuulizia hatua za kupata funguo za nyumba mpya, hapo ndipo akabaini kuwa TBA wamewapa funguo watoto wa kaka yake.

“Tulikwenda hadi TBA kutafuta suluhu ya suala hili, tukaambiwa tukae kikao cha usuluhishi kama familia.

“Siku tulipokaa baadhi ya viongozi wa TBA walikuwapo, lakini Abel (Mwenyekiti wa Kamati), akaamuru tutoke nje. Akamlazimisha mama akubali kwa maandishi kuwa amehiari kuishi na vijana wa kaka yake,” amesema Arafa.

Baada ya Fatuma ‘kuhiari’ japo kwa shingo upande na kuanza kuishi na vijana hao, Arafa anasema kumekuwapo vurugu za mara kwa mara kati yake na binamu zake, akipinga kunyanyaswa mama yake.

Arafa anasema kinachomtia hofu yeye na mama yake ni kitendo cha mmoja kati ya vijana hao, Juma, kuwaingiza wageni wasioeleweka chumbani kwao nyakati za usiku.

“Kuna wanaume wawili wamewahi kuletwa na Juma usiku. Akawatambulisha kwa mama, akisema; ‘huyu ndiye yule shangazi yangu.’ Kwa kweli utambulisho huo unamtia hofu sana mama,” amesema.

JAMHURI lilitaka kufahamu ukweli kuhusu hali hiyo kutoka kwa Juma, pia kama ni kweli aliwasilisha TBA hati feki ya kifo cha shangazi yake na kupewa funguo za nyumba Magomeni Kota.

Juma anasema hakuna tatizo lolote kati yake na shangazi yake, bali anayeleta vurugu ni Arafa.

Kuhusu kudanganya kifo cha bibi Fatuma, Juma anasema: “Ni kilevi ndicho kilisababisha nidanganye kuwa shangazi amefariki dunia. Wao (TBA) wakakubali kunipa funguo.
“Lakini sioni kama kuna shida kwa sababu TBA na viongozi wa kamati walitukalisha chini tukaelewana.”
Juma hakukubali kumwonyesha mwandishi wa habari hizi nakala ya ‘death certificate’ ya Fatuma Omari.

Wengine pia hawajapewa nyumba

Kana kwamba haitoshi, mbali na Likule, familia nyingine 20 zimejikuta zikinyimwa funguo za nyumba mpya tofauti na kauli ya Rais Samia na mtangulizi wake, Dk. John Magufuli.

Viongozi hawa waliweka bayana kwamba umiliki wa nyumba hizo utatolewa kwa kuwapa kipaumbele wakazi asilia wa Magomeni, huku Rais Samia akiwataka wajiandae kuzinunua baadaye.

Kaya 21 ni sehemu ya 644 zilzokuwa zikiishi Magomeni Kota kabla ya kubomolewa, wameliambia JAMHURI kuwa kuna watu wanatengeneza mgogoro ili wapate namna nzuri ya kufanya utapeli.

“Tunanyimwa funguo za nyumba zetu bila sababu za msingi. TBA na viongozi wa kamati wamefanya makusudi wapate namna ya kuzigawa kwa watu wengine.

“TBA wanatudanganya kuwa taarifa za nyaraka zetu zinaonyesha wamiliki kuwa wawili wawili, lakini hawatuonyeshi majina waliyoyabaini ni ya akina nani. Wao wanasisitiza twende mahakamani tu,” amesema mmoja wa watu hao.

Nao pia wanamlaumu Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Majengo ya Magomeni Kota, George Abel, kuwa amehusika kuingiza majina ya watu wasiohusika katika orodha ya wanaotakiwa kupewa kipaumbele.

Alipotafutwa na JAMHURI, Abel amekataa kuzungumza lolote akidai kuwa wenye uwezo wa kutoa ufafanuzi kwa kina ni TBA.

Kwa upande mwingine, wawakilishi wa kaya hizo 21 wanasema serikali ilipozindua mradi Machi 23, mwaka huu na kuruhusu wakazi wote 644 waliohakikiwa kupewa nyumba baada ya utekelezaji wake kufanyika, ilibainika kuwa watu 44 hawana funguo, ingawa kiuhalisia walikuwa 61; ambapo baadaye walishughulikiwa, 40 wakapewa funguo, huku 21 wakisalia bila kupata nyumba.

“Kuna watu wameingizwa kwenye nyumba hizi hawana nyaraka zozote wala hawana historia ya kuishi Magomeni Kota.

“Hili tunahisi limeratibiwa na wenye mamlaka ya kugawa funguo. Vinginevyo isingekuwa rahisi,” amesema mlalamikaji mmoja.

Anawataja watumishi wa TBA wanaohisiwa kushirikiana na mwenyekiti wa kamati kuwanyima funguo kuwa ni Kaimu Meneja Miliki Majengo, Fredy Mangula na mmoja wa mabosi ndani ya TBA.

“Kuna shida kwa wasimamizi wa Magomeni Kota walioko TBA na viongozi wa kamati, tumeyafikisha malalamiko yetu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, ila hatudhani kama suala letu litashughulikiwa,” amesema.

Waliofikisha malalamiko kwa RC ni Zamzam Mwalimu Kambi ambaye nyumba yake ya zamani ilikuwa Na. 406, Calista Mfinanga (Na. 604), Cyprian Mahelo (Na. 625), Abbas Masoud (Na. 586), Issack Mgumba (Na. 112), Nana Mwapoka (Na. 567), Mwanaisha Kais (Na. 549) na Edward Kubebeka (Na. 362).

Wengine ni Irene Mayuni (Na. 615), Said Bungile (Na. 252), Pamela Mihenga (Na. 50), Athuman Ibrahim (Na. 642), Salum Hassan (Na. 40), Respia Salakana (Na. 339), Oswald Ramadhani (Na. 567), Gabriel Kilindo (Na. 83), Jamal Mkunguluka (Na. 130), Chiku Hamisi (Na. 360), Silvia Ntanga (Na. 494), Paul Lekule (Na. 460) na Charles Memba ambaye nyumba yake ilikuwa Na. 352.

Mwakilishi huyo ameliambia JAMHURI kuwa anatilia shaka nyaraka mojawapo iliyosomwa kwao kama majibu ya mgogoro, akidai huenda si halali kutokana na kukosa baadhi ya sifa zilizomo kwenye nyaraka zinazotolewa na serikali.

“Nyaraka gani ya serikali itatolewa kwenye jambo zito kama letu bila kuwa na nembo ya serikali, muhuri wala sahihi? Hili linatutia shaka, tunahisi tunatapeliwa,” amesema.
Kichwa cha habari cha waraka huo kinasomeka: ‘Majibu ya uhakiki wa kina wa nyumba sitini na moja (61) zilizokuwa na mgogoro wa umiliki katika eneo la Magomeni Kota’.

TBA wajibu

Baada ya jitihada za kukutana na Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi wa Ujenzi, Daud Kondoro, kukwama kutokana na maofisa wa chini wa taasisi hiyo kuliambia JAMHURI kuwa hoja zote zinaweza kujibiwa katika ngazi za chini, mwandishi amekutana na Mangula.

Akifafanua kuhusu lawama za wakazi wa Magomeni Kota, Mangula anasema TBA haina mamlaka tena ya kumaliza mgogoro wa wakazi hao kwa kuwa taarifa zao zilihakikiwa na taasisi zaidi ya nne za serikali zilizokuwa zimepewa kazi ya kuhakiki nyaraka na kubaini kuwapo kwa upungufu kwenye nyaraka zao.

“Hili suala limehusisha taasisi nyingi za seriali, TBA sisi tumesimamia ujenzi wa mradi, majina ya wanaotakiwa kupewa nyumba hata sisi tuliletewa baada ya kuwa yamehakikiwa kwa usahihi.

“Mradi mkubwa kama wa Magomeni Kota ni lazima ulete kelele na sisi tunaousimamia hatuwezi kukwepa lawama, lakini wanaotulaumu wasidhani mchakato wa kupewa nyumba Magomeni ni mwepesi kama wanavyofikiria,” amesema Mangula.

Anafafanua kuwa waraka wanaodai kuwa si halali ulitolewa na TBA kama muhtasari unaoonyesha juhudi ambazo wamefikia katika kutatua changamoto ya watu 61 kukosa funguo.
Kuhusu bibi Fatuma anayedaiwa kuzushiwa kifo na wapwa zake, Mangulla ameahidi kulifuatilia kwa kuwa hilo ni jipya mezani kwake sawa sawa na suala la Likule.

Naye Katibu Tawala (DAS) wa Manispaa ya Kinondoni, Stella Msofe, ambaye ni mlezi wa Magomeni Kota na kiongozi aliyesoma muhtasari huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, anasema muhtasari huo umebeba majibu ya taarifa iliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuhusu mgogoro uliokuwa umeibuliwa.

“Timu ilichunguza na kubaini migogoro mingi kuwa ya kifamilia, taarifa nyingi zilionyesha wanafamilia kukinzana, sasa huwezi kubaini haraka mmiliki halali ni yupi.

“Isitoshe nyumba zilizoko Magomeni kila mtu anazitolea macho. Pia kitendo cha kukaa bure kwa miaka mitano lazima kuwepo migogoro,” amesema Stella.

Kwa upande mwingine, amesema wanaolalamikia uongozi wa kamati ya Magomeni Kota kama hawaridhiki nao wanatakiwa kukaa vikao na kukubaliana kuendelea nao ama la!