•Asilimia 41 hutumia huduma za kifedha kwa mtandao

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Matarajio ya Tanzania kujenga uchumi jumuishi yanaonyesha nuru baada ya takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuonyesha ongezeko kubwa la watumiaji wa huduma za kifedha mtandaoni.

Kwam mujibu wa takwimu za sekta ya Mawasiliano zilizotolewa na mamlaka hiyo zinaonyesha mwezi Juni 2022 watumiaji wa huduma za kifedha mtandaoni waliongezeka hadi kufikia watu milioni 37.4.

Idadi ya akaunti za fedha kwa njia ya mtandao, miamala na thamani ya miamala imeongezeka kwa kiasi kikubwa. Inakadiriwa kuwa zaidi ya theluthi moja (asilimia 41) ya Watanzania wanatumia huduma za ki-fedha kwa njia ya simu.

Takwimu zinaonyesha kuwa akaunti za fedha kwa simu zipatazo milioni 37.4 zilikuwa hai katika matumizi nchini Tanzania hadi kufikia Juni 2022. Zilifanya jumla ya miamala milioni 343.6; yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 11.6. Miamala hiyo inahusisha shughuli za kutuma na kupokea pesa na kulipia huduma na bidhaa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Dkt. Jabiri Bakari. Picha na TCRA

Takwimu zinaonyesha mwelekeo wa matumizi ya data na viwango vya malipo; huku huduma za data zilizounganishwa na zisizounganishwa kwenye vifurushi zikiwa za bei nafuu zaidi ikilinganishwa na huduma za sauti na ujumbe mfupi (SMS).

Viwango vya malipo ya data hupimwa kwa megabytes, au MB. MB moja ambayo haijaunganishwa kwenye kifurushi iliuzwa kwa shilingi Nane (8) (TZS) ikilinganishwa na shilingi 32 kwa simu za sauti kwenye mtandao wa mtumiaji (on-net) na mtandao mwingine (off-net). SMS za ndani ya nchi zilitozwa shilingi kumi na moja. Dakika moja ya sauti ni ghali zaidi kuliko gharama ya SMS na data.

Simu za kimataifa ziliendelea kugharimu zaidi katika Robo ya Mwisho ya mwaka wa fedha wa 2021/21. Dakika moja ilikuwa TZS 1,888 ikilinganishwa na TZS 1,601 ya awali; likiwa ni ongezeko la asilimia 18.

Kupigia simu nchi jirani (Afrika Mashariki) kuligharimu TZS 1,151 kwa dakika; ikiwa ni gharama nafuu kidogo kuliko katika robo ya pili ya 2021/21 wakati iligharimu 960 TZS.

Takwimu zinaonyesha kuwa watumiaji wengi huzungumza na kutuma SMS kwenye mitandao mingine zaidi (off-net) kuliko ndani ya mitandao yao (on-net).

Imani kwamba watu huzungumza zaidi ndani ya mitandao yao husika kwa sababu ya viwango vya bei nafuu imeondolewa na takwimu hizi. Uchaguzi wa laini ya simu miongoni mwa watumiaji sasa unaweza usijikite kwenye kigezo cha unafuu wa kuwasiliana bali utategemea bei ya huduma ndani au nje ya mtandao. Nafuu hii imepatikana kutokana na unafuu wa muunganisho baina ya mitandao na ndani ya mtandao husika ambao mtumiaji amechagua kuutumia.

Takwimu zinaonyesha kuwa kufikia Juni 2022, kulikuwa na laini za simu amilifu milioni 56.2; ambapo asilimia 52 zinatumika. Idadi ya laini za simu zilizosajiliwa iliongezeka kwa asilimia mbili (2); kutoka milioni 55.4 Machi 2022 hadi milioni 56.2 Juni. Katika ufikiwaji wa Mawasiliano ya simu na intaneti – wastani wa waliojisajili ikilinganishwa na idadi ya watu nchini – ilikuwa asilimia 92 na 48 mtawalia.

Kwenye sekta ya posta, takwimu zinaonyesha kuwa, licha ya maendeleo makubwa kuonekana katika mawasiliano ya kielektroniki, mawasiliano ya posta na usafirishaji vipeto bado yana sehemu kubwa katika sekta Mawasiliano nchini. Wastani wa vipeto na vifurushi 783 kila siku nchini. Kimataifa hutumwa vifurushi 144 na Afrika Mashariki hutumwa vifurushi 1,216 kila siku.

TCRA hukusanya takwimu za mawasiliano kutoka kwa Watoa-Huduma zote za Mawasiliano; yaani, mawasiliano ya simu, intaneti, huduma za fedha-kwenye mtandao, na utangazaji, na kuzichapisha kupitia vyombo vya Habari na tovuti ya Mamlaka kila Robo ya mwaka wa fedha.

By Jamhuri