Bwawa Nyumba ya Mungu kufungwa Machi 2023

Na Kija Elias,JamhuriMedia,Mwanga

Wadau wanaoshughulika na uvuvi katika Bwawa la Nyumba ya Mungu wa wilaya za Simanjiro, Moshi Vijijini na Mwanga, wamependekeza kufungwa kwa Bwawa hilo kwa kipindi cha miezi mitatu kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu.

Uamuzi wa kufungwa kwa bwawa hilo ulitolewa jana mbele ya kikao cha Ujirani mwema kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TRC Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, na kuwashirikisha viongozi mbalimbali.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau hao, wameiomba Serikali kupitia Wizara husika kulifunga Bwawa hilo la Nyumba ya Mungu kwa kipindi cha miezi mitatu ili kutoa fursa ya samaki waweze kuzaliana na kukua.

“Tunaiomba Serikali kulifunga bwawa hili ili kuruhusu samaki wakue na kuzaliana, kwani wako baadhi ya watu wachache ambao wamekosa uaminifu wamekuwa wakifanya uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zisizo rasmi na kuvua samaki wadogo katika bwawa hili,”alisema Afisa Uvuvi Wilaya ya Mwanga Said Msemo.

Akifungua kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Moshi Abbas Kayanda, ambaye alikua Mwenyekiti wa kikao hicho, alisema kutokana na kukuithiri kwa uvuvi haramu kwenye bwawa hilo, wamelazimika kukutana wilaya tatu zinazozunguka ili kuweza kuzungumzia suala zima linalohusiana uvuvi haramu unaofanyika katika Bwawa la Nyumba ya Mungu

“Tumeona tukutane kama viongozi wa wilaya hizi tatu zinazozunguka Bwawa la Nyumba ya Mungu ili tuweze kutoka na mikakati ya pamoja itakayosaidia kulinusuru bwawa hili, ambalo limeonekana kukithiri kwa uvuvi haramu,”alisema DC Kayanda.

Alisema “Changamoto kubwa ambayo imetolewa na wadau ni uvuvi haramu ambao unafanywa kwa kutumia nyavu zisizokubalika kwa mujibu wa maelekeazo ya Wizara jambo ambalo limekuwa likichangia sana kuharibu mazalia ya samaki,”alisema.

Awali akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Abdallah Mwaipaya, alisema asilimia 70 ya Bwawa la Nyumba ya Mungu liko wilaya ya Mwanga, katika mapato yake ya ndani halmashauri ya Mwanga inategemea zaidi, lakini kutokana na uwepo wa uvuvi haramu halmashauri imekuwa haipata mapato hayo kutokana na wavuvi kukimbilia wilaya ya Simanjiro.

Akifunga kikao hicho Mwenyekiti mwenza wa Kikao hicho, ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara Dkt. Suleiman Serera alisema Serikali inao wajibu wa kuhakikisha Bwawa la Nyumba ya Mungu, linatumika kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa wakati wote, hivyo kufungwa kwa bwawa hilo ni kutoa fursa ya samaki waweze kuzaliana na kuwa wakubwa.

“Kikao cha ujirani mwema kimependekeza Bwawa la Nyumba ya Mungu tulifunge kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Machi 2023 hadi Juni 2023,”alisema Dk. Serera.

Alisema pamoja na kulifunga bwawa hilo Serikali itaangalia maslahi mapana ya wananchi wa maeneo yanayozunguka bwawa hilo ili kuweza kuwaruhusu kupata kitoweo kutoka katika bawa hilo.

Kikao cha ujirani mwema kiliwakutanisha viongozi kutoka Wizara ya Uvuvi, maafisa uvuvi kutoka kila wilaya zinazozunguka Bwawa la Nyumba ya Mungu, Watendaji wa vijiji na Kata, Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya pamoja na Sektarieti za Mikoa ya Manyara na Kilimanjaro.