BALOZI wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro ametembelea kambi ya wanamichezo wa Tanzania wataoshiriki kwenye Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola iliyopangwa kuanza Julai 28, 2022, na kuwatakia kila la heri kwenye michuano hiyo inayoshirikisha jumla ya nchi 72.

Dkt. Migiro, ambaye amemuwakilisha kiongozi wa msafara Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa katika hafla ya kukaribisha rasmi nchi zinazoshiriki, alitoa pia salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa wanamichezo hao, akisema kiongozi huyo wa nchi na Watanzania wote kwa ujumla wana imani kubwa na wanamichezo hao kwamba watafanya vizuri kwenye mashindano.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro akikaribishwa na Bw. Henry Tandau, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania na Kiongozi wa Msafarta wa wanamichezo wa Tanzania kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola alipowatembelea katika kijiji cha wanamichezo katika Chuo Kikuu cha Birmingham Jumatatu Julai 25, 2022

“Macho na masikio ya Rais na ya Watanzania wote yako hapa Birmingham na wote wanawategemea kwamba mtafanya vyema kwenye michezo hiyo hivyo mjitume na kupigania heshima ya nchi kwa nguvu zote, huku mkidumisha amani, nidhamu na furaha wakati wote mtaokuwa hapa”, amesema.

Kwenye michezo hiyo Tanzania inawakilishwa na wanariadha tisa, mabondia watatu, wacheza judo wawili na waogeleaji wawili. Wachezaji wote wameshawasili Birmingham isipokuwa wanariadha wa marathon ambao walikuwa kambini Arusha na wanatarajiwa kuwasili siku tatu kabla ya michuano kuanza.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro akifurahia zawadi zilizoandaliwa na wanamichezo wa Tanzania kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola alipowatembelea katika kijiji cha wanamichezo katika Chuo Kikuu cha Birmingham Jumatatu Julai 25, 2022
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha-Rose Migiro akiongea na wanamichezo wa Tanzania kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola alipowatembelea katika kijiji cha wanamichezo katika Chuo Kikuu cha Birmingham.

By Jamhuri