Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha

Mabalozi wamehimizwa kutumia taaluma, uzoefu na ujuzi tofauti waliokuwa nao kuharakisha mabadiliko ya kimfumo yanayoendelea ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili, 23, 2024 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka wakati anaongea na Mabalozi katika warsha ya siku 4 ya kutathimini utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayofanyika mjini Kibaha tokea tarehe 21 Aprili 2024.

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mmebarikiwa kuwa na watu wenye taaluma tofauti na wenye historia ya sekta tofauti, tumieni fursa yenu hii kumsadia Mwanadiplomasia namba moja, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewarahisishia kazi yenu kwa kuitekeleza diplomasia kivitendo”, Balozi kusiluka alisema.

Amesema Serikali inazitambua changamoto wanazokabiliana nazo na inazifanyia kazi lakini kutokana na Wizara kuwa na watu wenye uzoefu wa kutoka sekta tofauti, wakishirikiana wanaweza kuzitatua na kuifikisha nchi katika hatua nzuri.

Balozi kusiluka alimazia kwa kuwapongeza Mabalozi kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwaahidi kuwa Serikali itapokea mawazo yote mazuri na ya kibunifu na kuyafanyia kazi.

By Jamhuri