DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

‘Nusu mtu, nusu chuma’ ni jina la utani analoitwa mlinzi wa kati wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Joash Onyango, ambaye ni raia wa Kenya. 

Onyango amepewa jina hili kutokana na kazi zake za nguvu na za kuvutia anazozifanya na kuzionyesha awapo uwanjani. 

Wiki iliyopita katika Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro baada ya mechi ya Mtibwa Sugar na Yanga kumalizika, wachezaji wa Yanga pamoja na mashabiki wao jukwaani walilipuka kwa furaha kwa ushindi wa mabao 2-0.

Yalikuwa mabao yaliyowekwa kimiani na nyota kutoka Burundi anayeichezea Yanga; Saido Ntibazonkiza na mwenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Fiston Mayele. 

Wachezaji hawa wa kimatifa ndio waliopeleka kilio kwenye mashamba ya miwa yanayomilikiwa na Mtibwa Sugar huko huko nyumbani kwao Turiani. 

Baada ya filimbi ya kuashiria kumalizika kwa mchezo huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, mashabiki wengi na wachezaji walimfuata Saido kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoionyesha; wengi miongoni mwao wakikubaliana hata bila kujadiliana kuwa huyu ndiye aliyecheza vizuri zaidi katika mechi ile; kwa Kiingereza ‘Man of the Match’. 

Hili kwa uhakika lilikuwa ni sahihi kabisa, kwani siku ile ‘Godfather wa Bujumbura’ aliupiga mwingi sana uwanjani. Saido akiwa uwanjani huwa ana utulivu wa hali ya juu sana. 

Hali haikuwa hivyo kwa upande mwingine, kwa kuwa golikipa wa Yanga, Djigui Diarra, alikuwa na mawazo tofauti na wengi waliolishuhudia pambano hilo.

Badala ya kumfuata Saido, kipa huyo raia wa Mali akaamua kumfuata Yanick Bangala, beki wake wa kati ambaye ni raia wa Congo. Hakuona haja ya kwenda kwa mchezaji mwingine yeyote!

Naam! Kipa huyo na nahodha wake, Bakari Mwamnyeto, walimfuata Bangala na kumkumbatia huku Diarra akionekana kumnong’oneza jambo moja au mawili sikioni. 

Sawa, huenda si Diarra peke yake aliyedhani kuwa Bangala ndiye ‘Man of the Match’ kwa mechi ile kwani mbali na yeye, pia Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, naye alimkimbilia Yanick na kumpa mkono. 

Unahisi ni kwa nini watu wote wawataje Ntibazonkiza na Mayele, kisha Kaze na Diarra peke yao ndio wamuone Bangala? 

Hii ni kwa sababu Bangala ni mwamba. Kwa muda sasa huyu jamaa amekuwa nguzo imara ya Yanga katika mifumo yote miwili ya uchezaji; yaani kujilinda na kushambulia. 

Amekuwa akicheza nafasi ya ulinzi wa kati na muda mwingine akionekana kucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi. 

Golikipa Diarra alikuwa au alifanya makosa ya hatari langoni mwake, jambo ambalo Yanick alilifahamu na kuanza kufanya ‘marking’ za kiufundi zaidi kiasi kwamba muda mwingi washambuliaji wa Mtibwa walijikuta waathirika katika mitego yake akishirikiana na Mwamnyeto.

Katika muda wote wa mchezo Bangala pia alitoa msaada mkubwa kwa viungo wa kati kusukuma mbele mipira langoni mwa Mtibwa Sugar, hali iliyowapa uhuru akina Khalid Aucho, Salum Abuubakar ‘Sure Boy’ na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kufanya watakalo katikati ya uwanja.

Ukimtazama kwa macho na hata mwonekano wake Bangala ni ‘tozi’. Lakini kwa hakika ana moyo mgumu ‘wa Kijerumani’. 

Ili ujue huyu mwamba ana mchango gani mchezoni, itazame Yanga vema hasa wakati yeye akiwa uwanjani.

Usajili wa Bangala unaweza kufananishwa na usajili wa nyota wa zamani wa Yanga, Constantine Kimanda. Huyu ni Kimanda kabisa! Kuanzia akili ya mpira hadi nguvu. Bangala anafanana vitu vingi na Kimanda.

By Jamhuri