Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma

Baraza la Vyama vya siasa nchini limewataka viongozi wa Vyama vya Siasa kujiepusha kutumia lugha za matusi,ubaguzi,udhalilishaji,upotoshaji na kubeza maendeleo na badala yake katika kutimiza malengo yao ya kisiasa wajikite kunadi sera zao kwa kujenga hoja na kutumia lugha yenye staha.

Onyo hilo limetolewa leo Agosti 16,2023 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa nchini Juma Ali Khatibu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimio ya baraza hilo lenye lengo la kujenga utaifa.

Akizungumza kwenye kikao hicho amesema maendeleo ya nchi yana manufaa Kwa wananchi hivyo ni jukumu la watanzania Kwa ujumla wao kushirikiana na Serikali Katika juhudi hizo.

“Agizo hili ni sehemu ya maazimio ya kikao maalum cha baraza hili kilichofanyika Agosti Mosi mwaka huu Jijini Dar es salaam na kushirikisha taasisi za dini na asasi za kiraia,lengo letu ni kuimarisha amani miongoni mwa watanzania,”amesema

Mbali na hayo Baraza hilo ambalo lipo chini ya Ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini limetoa azimio lingine kwa viongozi wa vyama vya siasa kujiupusha kuanzisha vikundi vya ulinzi vyenye mavazi na matendo yanayofanana na majeshi ya nchi kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuhatarisha amani,utulivu na umoja wa Kitaifa.

“Baraza linashauri wizara inayohusika na suala la uwekezaji katika Bandari ya Dar es salaam kuandaa kikao na wajumbe wa baraza ili kuwapa fursa wajumbe kupata uelewa kuhusu uwekezaji huo,”amesisitiza.

Khatibu amesema,”Natoa wito kwa Viongozi wa vyama vya siasa ,viongozi wa dini na wananchi wote kwa ujumla kujitahidi kudumisha amani na utulivu uliopo sasa na kufuata sheria ziliopo,hakuna mwananchi anayehitaji vurugu, tunahitaji amani ili kuwe na utulivu,”amesisitiza

Pamoja na mambo mengine Baraza hilo pia limetumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya kuendesha shughuli za siasa ikiwemo kuliwezesha baraza kufanya kazi yake ipasavyo.

“Dk.Samia ameboresha mazingira ya kufanya shughuli za siasa na kitupatia ushirikiano mkubwa,hii inatufanya tuzidishe amani na kuwa na mapenzi makubwa na nchi yetu,”amesema Khatibu.

Baraza hilo linatarajia kufanya kikao maalum cha kujadili utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi cha Rais Samia na kujadili hali ya kisiasa nchini kitakachofanyika Jijini Dar es salaam Agosti 28,29 na 30 mwaka huu na kitawashirikisha wadau wa siasa wakiwemo viongozi wa dini ,asasi za kiraia na viongozi mashughuli.

By Jamhuri