Na Mwandishi Wetu , JamhuriMedia

Benki ya NMB na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamezindua ushirikiano wa kibiashara wa mifumo ya malipo ya tiketi za ndege ‘Anga Rafiki – Tiketi Yako Imebima,’ unaowapa fursa wasafiri wa kulipia tiketi kupitia matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi App, ambazo zitakuwa zimekatiwa Bima ya Safari moja kwa moja.

Ushirikiano huo umezinduliwa Makao Makuu ya NMB jijini Dar es Salaam leo Jumatano Agosti 16, 2023 ambako msafiri atakayelipia tiketi za safari za ndani ya nchi kupitia NMB, atakatiwa bima ya maisha, ulemavu ama upotevu wa mizigo safarini, ambapo atalipwa hadi Sh. Mil. 5 za Kitanzania itapotokea mteja kufariki dunia.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ruth Zaipuna, amesema kwamba, kupitia matawi 229 na mawakala zaidi ya 21,000, wasafiri nchini wanaenda kufikiwa kirahisi kuwezesha upataji tiketi na kwa wateja wa benki hiyo wanazo njia za ziada za kulipia tiketi hizo kwa simu ya mkononi kupitia USSD na NMB App.

“Ni imani yetu sisi NMB kwamba, huduma hii sio tu inaenda kumpa urahisi na wepesi msafiri wa kulipia tiketi yake, bali kumkinga pia na majanga yatokanayo na safari kama ulemavu, kifo na upotevu wa mizigo. “

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi (wa pili kushoto), wakionyesha mfano wa ndege kuashiria uzinduzi wa mfumo wa malipo ya tiketi za ndege kupitia matawi, mawakala wa NMB katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 16, 2023. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa ATCL, Jamal Kiggundu na kulia ni Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi. (Na Mpiga Picha Wetu).

“Mteja akilipia tiketi ya ATCL kupitia NMB, ikatokea akafariki – ingawa hatuliombei hilo, ama kupata ulemavu akiwa safarini, yeye ama wategemezi wake watalipwa hadi Sh. Milioni 5.”

“Na iwapo mzigo (checked in Baggage) wa msafiri utapotea, mteja wetu atalipwa Shilingi 300,000, lakini pia ikiwa safari itasogezwa ama kuahirishwa, atalipwa Shilingi 150,000. Bima hizi tutazilipa kupitia washirika wetu Kampuni ya Reliance Insurance,” amefafanua Zaipuna.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi, aliipongeza NMB sio tu kwa ushirikiano wao huo, bali kuweka ziada ya Bima ya Safari kwa wateja wao, huku akibainisha kwamba hakuna tena sababu ya Watanzania kusafiri kwa hofu wakati kuna ATCL na NMB.

“ATCL kila siku tumejikita katika kuboresha utoaji huduma zetu, kuanzia tiketi inapokatwa, mteja anapokuwa safarini hadi kufika, hivyo tunajivunia ushirikiano wetu na NMB, ambao unaenda kututofautisha na watoa huduma za usafiri wa anga wengine waliopo sokoni.”

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi (wa pili kushoto), wakionyesha mfano wa ndege kuashiria uzinduzi wa mfumo wa malipo ya tiketi za ndege kupitia matawi, mawakala wa NMB katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 16, 2023. (Na Mpiga Picha Wetu).

“Ni ushirikiano unaoenda kumaliza kabisa hofu ya upatikanaji tiketi za safari na usalama wa abiria wetu na mali zao wawapo safarini, hii ni kutokana na ziada zilizowekwa na NMB kwa abiria watakaolipia kupitia mtandao wao mpana wa matawi, mawakala na huduma za NMB Mkononi kama alivyotangulia kusema CEO Zaipuna,” ameongeza Matindi.

Matindi ameenda mbali zaidi na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kila aina ya uwezeshaji inaowapa katika kutoa huduma kwenye Sekta ya Usafiri wa Anga kitaifa na kimataifa, ambako kufikia mapema mwakani watatanua mtandao wa ndege zao kufikia 16.

Ameitaka NMB kujiweka tayari kuhudumia wateja wa ndege zao hizo, ikiwamo kujenga mazingira ya kuongeza chachu ya usafirishaji wa mazao na bidhaa za ndani kwenda nje ya nchi, huku akimaliza kwa kuhoji kwanini abiria wasafiri kwa hofu wakati kuna ushirikiano chanya mfano wa huo wa Shirika lake na benki hiyo.

By Jamhuri