Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia

Wakazi wa kijiji cha Pande plot wilayani Kilwa mkoani Lindi wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan
kuwatatulia kero ya barabara kama alivyo ahidiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake Mahamudi Mandodo amesema wakazi wa eneo hilo,wamekuwa na kero ya barabara kwa muda mrefu kwani wamekuwa wakilazimika kutembea kwa miguu,pikipiki kwa zaidi ya umbali wa kilometa 32 kufika barabara kubwa.

Mandondo amesema barabara hiyo imekuwa changamoto kwa wakulima na wagonjwa kwa sababu wamekuwa wakipata shida sana wakati wa dharula na kusafirisha mazao yao kipindi chote.

“Mtu akitaka kusafiri kutoka kijijini nyakati za kiangazi lazima atumie pikipiki au usafiri wa kibasi kidogo kwa gharamna kubwa ambayo wananchi wanashindwa kuimudu,” amesema.

Amesema wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kwenda kwenye eneo hilo na kuwaahidi wananchi wa eneo hilo, kwamba barabara yao itajengwa kwa lami lakini mpaka sasa haijajengwa na wananchi wanaendelea kuteseka.

Mohamedi Soli amesema kuwa kijiji cha Pande wamekuwa wakiishi kama wapo kisiwani ,kwani ubovu wa barabara hiyo umewafanya kurudi nyuma kiuchumi kutokana na adha ya usafiri.

“Usafirishaji wa mazao kutoka pande kwenda barabara kuu au wilayani ni gharama kubwa kwani gunia moja unaweza kusafirisha kwa gharama ya sh. 6000 na kuendela sasa mkulima na mlalahoi akitaka kwenda kuuza mazao yake hawezi ukichukulia kipato chao ni duni.

“Japokuwa thamani ya wakazi haionekani lakini kijiji hiki kimekuwa kikilima mazao ya biashara kama korosho ,ufuta na mazao ya bahari ili kujikwamua lakini wamekuwa hawawezi kusonga mbele kutokana na hali ya barabara kuwa mbaya na hivyo kuwawia vigumu kuinuka kiuchumi,” amesema.

Soli amedai kipindi cha Rais Kikwete alikwenda kwenye maziko ya mwanazuoni mkubwa marehemu Sheikh Nurdin Hussein, alitoa ahadi ya kabla hajaondoka maradakani ,barabara hiyo angehakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami.

.

“Ukifika hapa hotel tatu kuna kibao kimeandikwa barabara yetu imepandishwa hadhi sasa itasimamiwa na mkoa kwa maana ya TANROADS na inatakiwa kutengenezwa kwa kiwango cha changarawe mpaka kwenye bandari ya mtandula lakini kilichofanyika hakuna mpaka leo tunaabika tu”amesema Soli.

Mkuu wa wilaya hiyo Christopher Ngubiagai amesema barabara ni ya muda mrefu inachangamoto kubwa, lakini iko chini ya TARURA kwa taarifa alizokuwa nazo wanataka kuitoa kwenye kiwango cha vumbi kwenda kwenye changarawe.

“Sasa kila mwaka TARURA wamekuwa wakitenga bajeti zao kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kwa awamu kutoka hoteli tatu mpaka sasa wameshafikia kijiji cha Mkazambo”anasema Ngubiagai.

Sasa tumewaomba TARURA wakaangalie changamoto zake ,kwa sababu barabara hiyo imekuwa na changamoto kubwa wakati wa mvua,” amesema.

By Jamhuri