Barua ya wazi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani

Kwako Mheshimiwa Hamad Yusuf Masauni (MB) Waziri wa Mambo ya Ndani. Pole kwa kazi na ninakusalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Kwanza ninakupongeza kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kukuamini na kukuteua kuwa msaidizi wake kuongoza wizara hii nyeti.

Ninaandika barua hii kuhusu dhamira ya serikali kutaka Jeshi la Magereza kujitegemea.

Kwa hakika dhamira hii inasababisha maumivu makali kwa mahabusu hasa wa Gereza la Keko, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Waziri, naomba ufahamu kwanza kwamba ninayeandika barua ya mkasa huu kwa sasa ni raia mwema.

Ni mwezi mmoja tu uliopita nilikuwa Gereza la Keko nikituhumiwa kwa kesi ya jinai. Imekwisha na nimeachiwa huru baada ya kuwekwa hapo miaka mitatu!

Kwa muda niliokuwa katika gereza hilo, nimeyaona mengi, lakini kuna mengine yamenifanya kushindwa kunyamaza. Hakika ungejua yanayoendelea Keko, ungeyatafutia ufumbuzi haraka.

Ninasema hivyo kwa kufahamu kwamba uamuzi kutaka Jeshi la Magereza kujitegemea bila kupewa fungu kutoka serikalini, ni mwiba kwa wakuu wa magereza na mahabusu wa mijini, mfano Keko.

Mheshimiwa, ninasema hivyo kwa kuwa ninafahamu na mahabusu wanaumia sana hadi ninatoka hakuna dalili ya kutatuliwa shida mbalimbali kwa kuwa taarifa hazikufikii.

Hakika zingekufikia, ungetafuta muafaka.

Keko kuna tatizo la usafiri wa kuwapeleka mahabusu mahakamani. Hili ni tatizo kubwa ingawa uongozi wa gereza ukiulizwa hauwezi kukiri kwa hofu ya kuonekana wameshindwa kujitegemea.

Ukimya huu wa uongozi wa Gereza la Keko unawaumiza mahabusu wanaohitaji kufikishwa mahakamani mapema lakini badala yake huwa wanafika saa tano na si saa mbili na kukuta kesi zao zote zimeahirishwa bila wao kuwapo!

Mheshimiwa Masauni, hilo lipo pia kwa mahabusu wa Ukonga na Segerea na wanaotaabika zaidi ni wanaopaswa kwenda kusikiliza kesi zao Mahakama ya Kinondoni.

Hali hii, mheshimiwa, wala si siri! Haihitaji utafiti wa fedha nyingi! Ipo tu na ukiamua hata leo utapata majibu na ukweli wenyewe.

Wengine wanaoumizwa na ugumu wa usafiri wa mahabusu unaosababishwa na magereza kutakiwa kujitegemea ni ndugu wanaofuatilia kesi.

Hawa wanakuwapo mahakamani mapema, wanasikia kesi ikiitwa saa tatu asubuhi lakini mahabusu hawajafika. Wanakuwapo hata saa tano wakati kesi zikiahirishwa bila ndugu zao kuwapo! Inaumiza sana.

Kwa mtindo huo kuna mahabusu wameshakaa zaidi ya miaka mitatu kusubiri vikao, halafu wanakuja kupata tarehe ya kwenda kusikiliza kesi, kisha zinaahirishwa, makarani wa mahakama wanawaambia kuwa jaji amekwishaita kesi tangu saa tatu, hivyo ameahirisha mpaka siku nyingine.

Mheshimiwa, hebu jiulize, kama binadamu, inapotokea hali kama hii utajisikiaje?

Mkuu wa gereza analiona tatizo, lakini amekaa kimya. Hata wenzake wa mikoani pia wamekaa kimya, wanashindwa hata kumwambia Kamishna Mkuu wa Magereza.

Kuna nyakati ni basi moja tu hutumika kuchukua mahabusu wa Ukonga na kupita mahabusu zote ndipo safari kuwapeleka mahakamani ianze. 

Mheshimiwa, ofisa mmoja wa magereza Mkoa wa Dar es Salaam, tangu ateuliwe asikilize changamoto zilizopo hajafanya hivyo!

Ninaamini hata ukimpigia simu kumuuliza hatakuwa na majibu ya kukupa. 

Mheshimiwa, lipo tatizo jingine Keko linalohuzunisha sana mahabusu waliopo ndani na ndugu wanaokwenda kuwatembelea siku za wikiendi na sikukuu. 

Katika siku hizo ndugu huwatembelea mahabusu kuwaona na kuwapelekea chakula kama ilivyo utamaduni.

Lakini tangu Desemba 8, 2021, Gereza la Keko, lilizuia ndugu kuwapeleka huduma hizo wapendwa wao kwa madai ya sababu za kiusalama.

Watu wanajiuliza, usalama huo ni upi ikiwa chakula hakimfikii mlengwa mpaka kwanza kikaguliwe na maofisa wa magereza?

Mtu anayepeleka chakula naye huwa na kibali maalumu kinachosainiwa na Mkuu wa Gereza. Swali, ni kwa nini hali hii ipo Keko pekee?

Keko ina tofauti gani na magereza mengine? Uongozi wake unafuata sheria tofauti na magereza mengine?

Tangu zamani hakujawahi kuwekwa zuio kama hili. Likawekwa mwisho wa mwaka hadi leo bado haijaruhusu ndugu kupeleka chakula kwa wapendwa wao.

Meshimiwa Waziri, naomba kufahamu, utaratibu na utamaduni wa mahabusu kupelekewa chakula magerezani siku za wikiendi na sikukuu, upo katika sheria za nchi au ni utaratibu tu waliojiwekea jeshi la magereza?

Wakati nikiwamo Keko, mimi na wenzangu tulijitahidi sana kuomba utaratibu wa kuletewa chakula urejeshwe, lakini hatukufanikiwa. Uongozi uligoma kabisa!

Kwa ukweli tatizo la uongozi wa Gereza la Keko unawaumiza sana ndugu wa mahabusu na familia zao kwa kuvunja utamaduni mzuri wa Kitanzania.

Mheshimiwa, hata ninyi kwenye chama chenu, CCM, kuna utamaduni na utaratibu ambao si sheria. Rais anayepatikana kwenye kinyang’anyiro ndani ya chama chenu ni kawaida kuongoza vipindi viwili. Ni utamaduni mliojiwekea. 

Hakika, Mheshimiwa, ninaomba, kwa niaba ya ndugu zangu mahabusu, ulitazame kwa jicho la tatu na kumsaidia Rais Samia katika hili kwa kuwa ni mpenda haki na ana wapenda wananchi wake wote hata walioko jela.

Changmoto ya mwisho niliyoishuhudia katika Gereza la Keko ni bei ya vitu wanavyouza katika duka lao.

Bei ya hapo ni mara mbili ya bei za kawaida. Hili nalo nadhani ni kwa sababu Magereza wameambiwa wajitegemee.

Nimewahi kuwasikia maofisa wakisema wanategemea wauze maandazi na sukari kwa mahabusu ndipo wanunue dizeli kwa ajili ya kupeleka mahakamani na LUKU kwa ajili ya umeme wa kupandishia maji.

Kisima cha magereza kimefungiwa LUKU! Hili suala la kujitegemea ni mwiba kwa wakuu wa magereza na kwa watuhumiwa hali ni mbaya sana. 

Ni mimi raia mwema, mpenda haki kwa taifa langu, Said Hamis Lubuva.