Na Jumanne Magazi, JamhuriMedia, Dar es Saalam

Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kupitia kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imetangaza kupanda kwa Riba mpya ya Benki Kuu yaani (Central Bank Rate-CBR) kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi asilimia 6.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania ( BoT) Emmanuel Tutuba amesema mamati imeona umuhimu wa kuongeza Riba ya Benki Kuu hadi asilimia 6, itakayokuwa na wigo wa asilimia 2 juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia.

Vilevile Tutuba amesema riba hiyo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024, yaani mwezi Aprili hadi Juni 2024.

Aidha amesema kutokana na tathmini ya mwenendo wa uchumi wa dunia, Kamati imebaini kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ukuaji wa uchumi uliimarika katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi.

“Mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sambamba na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha.

“Bei za bidhaa katika soko la dunia imebaki tulivu. Mathalan, bei ya mafuta ghafi ilikuwa wastani wa dola 80 kwa pipa, wakati bei ya dhahabu imeendelea kubaki juu, ikiuzwa kwa wastani wa dola za Marekani 2,071 kwa wakia moja”alifafanua Gavana Tutuba.

Amesema ,Hali hii inatarajiwa kuendelea katika kipindi kijacho cha mwaka 2024.

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania ,Gavana Tutuba alibainisha kuwa Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi, licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa dunia.

“Hali hii ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, hususan robo ya pili ya mwaka 2024.

Kwa upande Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania,Theobald Sabi amesema wao kama wadau wa kuu wa BOT,wamefurahi kuona uchumi wa nchi umezidi kukuwa kwa kipindi Cha robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Amesema kutokana na ongezeko hilo tayari mabenki nchini wameendelea kutumia ongezeko Hilo ili kusaidia kufikia riba ya mikopo kwa mabenki na wataja wao.

Vilevile Sabi amesema wao wamefarijika kusikia uchumi wa nchi umeongezeka kwa asilimia 5.1 na uchumi ukiendelea kwa kipindi cha robo ya kwanza na pia amesema Gavana hadi kumalizika kwa robo ijao uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukuwa hadi kufikia asilimia 6.2.

Katika hatua nyingine Gavana Tutuba amesema “Ukuaji wa uchumi unakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2023, kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022.

Aidha amesisitiza kuwa ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.” alisisitiza Gavana Tutuba.

By Jamhuri