*Ilikataa kumwongezea mshahara, akaomba kazi CRDB akapata

*Ilipobaini amepata kazi ikaahidi kumlipa mara mbili asihamie huko

*Alielekea kukubali, akabaini ni danganya toto, akathibitisha kuondoka

*Utawala wakafanya mbinu, wakamfukuza kazi kwa kosa la kusingiziwa

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Benki moja kubwa nchini imeingia katika mgogoro na mamia ya wafanyakazi wake baada ya kupata Mtendaji Mkuu mpya mwenye majivuno, asiyethamini wafanyakazi na anayeamini ipo siku atateuliwa kuwa Waziri wa Fedha, JAMHURI limebaini.

Katika hali ya kusikitisha, benki hiyo sasa ina migogoro mingi na wafanyakazi wake, ambapo kesi kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) zimezidi kuongezeka ndani ya miaka miwili iliyopita kwa kiwango ambacho wafanyakazi wote wanaoondolewa kwa fitina wana kila dalili ya kushinda kesi hizi, siku wakishinda benki itakuwa na wakati mgumu kulipa fidia.

Mtendaji huyo mwenye dharau, ameteuliwa katika moja ya kamati nyeti hapa nchini hivi karibuni, na amesikika akisema kuwa “yeye anaongoza benki kubwa, hivyo anastahili kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo na si kuwa chini ya mtendaji mkuu wa taasisi moja ya kiserikali.”

Mwenendo wa mtendaji mkuu huyu umepata kutiliwa shaka na Spika wa Bunge, Job Ndugai, katika moja ya vikao vya Bunge hivi karibuni aliposema: “[Jina la benki linahifadhiwa] tangu ameingia huyu [jina limehifadhiwa pia] hii benki imekuwa na uchoyo uliopitiliza na haieleweki.”

Kituko cha mwaka

Ukiacha vituko vya kutisha anavyowafanyia wafanyakazi kwa kuwasema hadharani na kutoa siri za watumishi mbele ya watu wasiohusika, huku akitumia mbinu za kuwatisha na kuwasukuma waache kazi wenyewe, zamu hii ametoa kali ya mwaka.

Mwakilishi wa benki hiyo kubwa Zanzibar, aliomba kuongezwa mshahara miaka mitano iliyopita, lakini alipuuzwa. Mwaka huu aliwaambia watu wa utawala kuwa kutokana na mwelekeo wa benki hiyo kutotaka kumwongeza mshahara ameamua aombe kazi sehemu nyingine.

Mfanyakazi huyu ambaye alikuwa kiungo kikuu kati ya benki hiyo kubwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa unyenyekevu mkubwa aliwasiliana na Afisa Utumishi Mkuu, akamjulisha kuwa kutokana na ukweli kuwa mwajiri wake hajaonyesha nia ya kumwongeza mshahara, ameamua kuomba kazi benki nyingine. 

“Walifikiri anatania. Wakamwambia awathibitishie kuwa amepata kazi benki nyingine. Yeye kwa unyenyekevu mkubwa akawapa barua ya offer. Wakamwambia asiende CRDB. Wakasema watamwongezea mshahara mara mbili. Tena wakamwandikia email kuwa watamlipa mara mbili ya offer aliyopewa (nakala tunayo), wakamwambia atulie tu, asiwe na hofu.

“Baada ya email yao, akaona muda unapita hakuna kinachotokea. Akajua ni danganya toto ileile ya mara zote. Akathibitisha kukubali offer ya CRDB”. Hapa ndipo roho mbaya ikadhihiri. Ghafla wakamletea mashitaka ya mwaka 2016, ambayo walifanya uchunguzi wakatoa taarifa kuwa hakuna kitu wakati huo. 

“Kuna mteja mmoja anafanya biashara na mke wa mfanyakazi huyu. Inaonekana walikuwa na visa au walivurugana na mke wa mfanyakazi huyu mwaka 2016. Mteja huyu alifika benki hapa Zanzibar kuomba mkopo wa Sh milioni 12. Katika hali ya kumchimba, akadai ameombwa rushwa ya Sh milioni 5 kupitisha mkopo wa Sh milioni 12.

“Benki ilifanya uchunguzi, ikabaini kuwa hakukuwapo kitu cha aina hiyo mwaka 2016 na ikafunga jalada. Kwa mshangao, mtu huyo huyo ambaye Afisa Utumishi Mkuu amemwandikia barua pepe akimbembeleza asiondoke wamwongeze mshahara (kipande cha barua hiyo tunakiweka gazetini) siku 12 baadaye Afisa Utumishi Mkuu huyo huyo, amemfungulia mashitaka kwa kasi ya upepo, kesi ambayo ilichunguzwa mwaka 2016 na kubainika haina mashiko. 

“Kwa masikitiko, Mzanzibari huyu amemfukuza kazi siku sita kabla muda wa notisi ya siku 30 aliyotoa kuacha kazi kuisha na kujiunga na CRDB Novemba 15, 2021. Hii ni fitina, ni majungu na inayumbisha Muungano. Ni moja ya kero za Muungano tunazosema. Kuna watu hawathamini Wazanzibari.

“Kwa kweli shida imekuwa kubwa mno tangu ameingia huyu mtendaji mkuu. CMA hadi wanauliza kuna shida gani katika benki hii ya [jina linahifadhiwa]. Mtendaji huyu anachofanya ni kujipendekeza na kumdanganya Rais Samia Suluhu Hassan. Amejionyesha kuwa ana uwezo mkubwa, kumbe hamna kitu. Waliomzunguka wamemteka.

“Bahati mbaya ni mshamba. Amechelewa kufika mjini. Wakurugenzi na watendaji wachache wanaofitini watumishi wenzao wanafaidika na ujinga wake. Wanamdanganya kuwa Rais Samia atamteua kuwa Waziri wa Fedha, anawaamini kama zuzu. Anagombana na kila awaye isipokuwa waliomzunguka. 

“Waliomzunguka wanatumia udhaifu wake wanajipatia mikopo mikubwa kupitia watoto wao au kampuni walizo na vinasaba nazo. Wakirudi kwake wanajichekesha na kumwambia yeye ndiye mwanzo na mwisho. Anasahau kuwa [jina linahifadhiwa] ina wafanya kazi wanne tu, ambao ndio walioanza nayo baada ya benki mama kuvunjwa na yeye ametoka sehemu nyingine ni wa kuja hapa,” kinasema chanzo chetu kwa masikitiko katika maelezo ambayo JAMHURI limeamua kuyachapisha neno kwa neno.

Mzanzibari aliyedhulumiwa anena

JAMHURI limewasiliana na mfanyakazi huyo aliyefanyiwa fitina, ambaye amesema: “Tarehe 13, Septemba nilifanyiwa upelelezi na Forensic Officer Zanzibar kwa ile issue ya 2016. Tarehe 16, Septemba nilipokea offer ya CRDB. Tarehe 26, Mzee [jina linahifadhiwa] aliniita na kunihakikishia nitulie menejimenti wamemtuma na kunihakikishia kijana wake aliyekuja kunipeleleza hakukuta kitu kibaya chochote.

“Tarehe 28 Septemba nilishare offer Kwa CHRO na reply yake ya tarehe 4, October ni kuwa wataicounter offer. Email ninayo. Tarehe 15 October baada kuona wana-delay nikatoa 30 days Resignation notice (taarifa ya siku 30 ya kujiuzulu). Tarehe 21 October (siku 6 baada ya taarifa ya kuacha kazi) wakatoa charge sheet (mashitaka) na nika-reply the same day (nikajibu siku hiyo hiyo).

“Tarehe 28 October waka-issue hearing notice (taarifa ya kusikilizwa) ambayo ifanyike tarehe 2 Nov. Na tarehe 8 Novemba ndiyo wameni-terminate… (wamenifukuza kazi). Kitu ambacho tarehe 14 ilikuwa ndiyo my last day with [jina linahifadhiwa], na tarehe 15 Novemba naripoti CRDB.

 “Inaonekana wamefanya uamuzi tarehe 7, wao wakanifukuza tarehe 8, naona waliona hii inawalinda kwa roho mbaya nikose kila kitu. Interview [ya CRDB] ilikuwa Agosti mwanzoni, na Agosti 19 CRDB wakanipa negotiable offer na nikaanza submission of some documents while them preparing the employee documentations… (kuwasilisha vielelezo ilhali wao wakiandaa masharti ya ajira). Agosti nikakamilisha kila kitu… inathibitisha roho mbaya ya vitu nilivyokuwa ninasikia tangu ameingia huyu mtendaji mkuu.

 “Nimeambiwa anasumbua kila anayeona anaweza kuonekana mbele ya Rais Samia na anakanyaga haki za watu kama hana akili nzuri. Amenifanyia hivyo kunifukuza kazi akiamini Kanuni ya sasa ya Benki Kuu (BoT) inayosema mtumishi wa benki akifukuzwa benki moja hataajiriwa benki nyingine itatumika kunikosesha kazi.

“Lakini najiuliza, hii ni roho mbaya ya namna gani? Sisi huku Zanzibar tunamwogopa Mungu. Hatufitiniani kwa kiwango hichi. Sisi fitina ziko katika siasa ila si maisha ya watu. Mtendaji huyu ana roho mbaya usipime. Ataiangusha hii benki si muda. Siku hizi anatumia wafanyakazi wenye nyadhifa za chini kuchokonoa mabosi wao. Ajabu kweli. Inabidi afungwe gavana huyu.

“Mimi naomba Benki Kuu iingilie kati, ifanye uchunguzi kubaini uonevu huu. Wapo wengi sana walioonewa. Wengine wanaishi kama watumwa. Heri mkoloni kuliko huyu mtendaji mkuu aliyeendekeza majungu na watu wachache wenye kujikomba, anayeharibu maisha ya watu mchana kweupe,” amesema Mzanzibari huyo aliyefanyiwa fitina.

Kesi za watumishi

JAMHURI limepitia majalada kadhaa pale CMB na kubaini kuwa mamia ya wafanyakazi wanaacha kazi katika benki hii kubwa inayowaambia kuwa hawana mahala pa kwenda. Gazeti hili limekutana na kesi zilizoko Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na CMA ambazo watumishi wanadai fedha za kutisha. Mtumishi mmoja katika Mahakama ya Rufaa anadai Sh 550,000,000, mwingine anadai Sh 500,000,000, mwingine anadai Sh 366,677,195, mwingine anadai Sh 112,000,000, mwingine Sh 80,000,000, mwingine Sh 55,000,000, mwingine Sh 52,000,000 na orodha ni ndefu.

Baadhi ya wafanyakazi wanaosukwasukwa ndani ya benki hii na wengine ambao tayari wamefukuzwa kazi kibabe baada ya Afisa Mtendaji Mkuu kuingia akaungana na wakuu wa idara wanaojikomba akiwamo Mkuu wa Idara ya Utumishi miaka miwili iliyopita, wameipatia JAMHURI nakala ya watumishi 286 ambao wamefungua kesi au wanasumbuliwa na mtendaji mkuu huyu anayeamini anastahili kuwa Waziri wa Fedha.

JAMHURI limepata taarifa kuwa mmoja wa wakuu wa mikoa Zanzibar amempigia simu mtendaji mkuu wa benki hii kumuuliza juu ya kadhia hii, akasema: “Mimi niko lilizo Singida, sina taarifa hizo.” 

JAMHURI limewatafuta watendaji wakuu wa benki hii bila mafanikio, na sasa kupitia wakili wake linakamilisha taratibu za kisheria kupata ruhusa ya Mahakama kuchapisha orodha ya kesi zinazoikabili benki hii chini ya mtendaji mkuu anayetaka kuiangusha benki hii katika soko.

Mmoja wa wafanyakazi amelieleza JAMHURI: “Mwenzetu huyu anayefanyiwa fitina, ni mmoja kati ya wengi. Watu wanaishi kama vile wapo jehanamu. Kila mara tumelalamika Benki Kuu haitusikilizi. Tunaomba BoT iingilie kati. Huyu mtendaji mkuu ameigeuza benki hii kubwa kuwa kama nyumbani kwake. Anagombana na kila mtumishi isipokuwa hao wachache wanaompa majungu. Angalia benki kama CRDB wafanyakazi wana raha sana. Mtendaji Mkuu wa CRDB, Majid, anasaidia wafanyakazi, ila huyu wetu, anataka kudidimiza wafanyakazi.

“Tunaomba Rais Samia aingilie kati. Huyu mtendaji wetu amemdanganya Rais Samia kwa kujipendekeza akadhani ana maana kumbe ni mtu wa hovyo sana. Hafai kuongoza hata mtaa, achilia mbali benki kubwa kama hii. Anaendekeza majungu usiku na mchana. Anajifanya ni mtu wa Mungu kumbe anashinda kwa ‘sangoma’ Bagamoyo. Tunamwomba Rais Samia atunusuru dhidi ya huyu mtendaji mkuu.”

JAMHURI linaendelea kufuatilia utendaji wa benki hii na litaendelea kutoa taarifa kadiri zinavyopatikana. Je, wewe ni mmoja wa walioonewa na benki hii? Wasiliana nasi kupitia namba zilizopo gazetini, nasi tutachapisha taarifa zako bila woga, wala uonevu.

By Jamhuri