Mfumo wa uchumi, dhana ya kukosekana kwa ajira 

KILIMANJARO

Na Nassoro Kitunda

Kumekuwa na mjadala kuhusu tatizo la ajira hapa nchini. Ni mjadala wenye sura nyingi namna unavyojadiliwa. Taarifa ya Uchumi ya Mwaka 2018 inasema kila mwaka wahitimu wanaomaliza elimu ya chuo kikuu ni zaidi ya laki nane katika ngazi mbalimbali za elimu nchini. 

Lakini uwezo wa kuajiriwa upo chini ya kiwango hicho. Huku utafiti wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) wa mwaka 2017 unaonyesha milioni 70 ya vijana duniani wanakosa ajira baada ya kuhitimu masomo yao. Hii inaonyesha kuwa tatizo ni kubwa katika nchi na kunahitajika suluhu ya haraka ya tatizo hili.

Baadhi ya wasomi na wachambuzi walinyooshea vidole taasisi za elimu na kusema kwamba haziandai wahitimu kwa ajili ya soko la ajira na kinachotolewa hakihitajiki katika soko la ajira. 

Lawama hizi au nadharia hii ilienda mbali zaidi na kuanza kupitia upya mitaala na kuifanya iendane na mahitaji ya soko la ajira. Kwa hiyo mitaala ilinyooshewa kidole na wadau wakaanza kuifanyia kazi. 

Kipindi hicho hicho tukaona sera mpya ya elimu ikaja ya mwaka 2014 inayosema kuwa itakuja na mfumo nyumbufu wa kusaidia wanafunzi katika maisha yao ya kawaida mara wanapohitimu masomo yao. Ibara ya 3.2.3 lengo la sera hii inasema: “Kuwa na mitaala yenye tija, iliyofanisi na inayokidhi mahitaji ya soko la ajira katika kuleta maendeleo ya taifa na kuhimili ushindani.” 

Hoja hii ya kulaumu elimu ya juu na mitaala yake ikaleta kitu kinachoitwa ujasiriamali. Ingawa hoja ya ujasiriamali ni hoja inayotoka kulaumu taasisi na kwenda kulaumu mhitimu binafsi, kuwa yeye mhitimu ndiye tatizo na anashindwa kufikiri nje ya boksi na kubadili mtazamo wake kuwa ukisoma si lazima uende ofisini. 

Wanasiasa wa vyama vyote nao sasa wamekuwa wakilisema hili kuwa wahitimu wanapaswa wajiajiri na wasitarajie ajira ya kuajiriwa na kukaa ofisini.

Hapo ndipo tunaona masomo ya ujasiriamali yakifundishwa si vyuoni tu hadi kwa makundi ya watu kupitia taasisi au hata wanaoitwa wahamasishaji (motivational speakers). Kuwa inawezekana mtu au jamii kupata maendeleo na kipato kwa kujiajiri. 

Tatizo la kutokuwa na ajira ni matokeo ya mfumo na hoja hizi hapo juu zinahama katika hoja ya msingi kuwa tatizo la ajira ni tatizo la mfumo wa uchumi unaotawala, yaani mfumo wa uchumi wa uzalishaji wa kibepari ambao kwa namna moja unafaidika na kinachoitwa ukosefu wa jira, kwa sababu kunakuwa na wimbi kubwa la watu walio katika ajira wanalipwa mishahara midogo na mazingira mabaya ya kazi, kwa kuwa ukiacha yupo wa kuziba hiyo nafasi.

Pia mfumo wa uchumi wa kibepari unaoratibiwa na soko huria unahamisha hoja ya msingi ya jamii katika namna inavyozalisha mali inapaswa kuzalisha na kinachoitwa ajira, kwa sababu dhana ya ajira ni dhana inayotokana na aina ya uchumi uliopo.

Ubepari haulengi kuajiri watu bali unalenga faida, kwa kuwa ndiyo kipaumbele. Kwa hiyo dhana ya ujasiriamali na kujiajiri ni dhana ya kuhamisha watu kutoona athari za ubepari na kuona ni haki yao kujiajiri na mfumo kutozalisha hizo ajira. 

Elimu imekuwa sehemu ya kuhalalisha na kuhamisha hiyo hoja na leo hii ujasiriamali unazungumzwa kama ndiyo suluhu pekee ya tatizo hili. Daktari Abunuwasi Mwami katika makala yake iliyochapishwa katika jarida la sosholojia Tanzania, anasema tatizo la elimu inayosukumwa na soko huria inafundisha watu kwa ajili ya soko badala ya kutatua matatizo katika jamii. 

Kimsingi, tatizo la ajira pia lina uhusiano katika uchumi wa kidunia, kati ya matabaka ya nchi tajiri na maskini. Tatizo la ajira limekithiri zaidi katika nchi maskini ukilinganisha na nchi tajiri, ingawa nchi hizo pia zimekumbwa na tatizo hilo la ajira. 

Gazeti la The Guardian la mwaka 2013 lilichapisha taarifa ya janga la ukosefu wa ajira barani Ulaya. 

Lakini nchi tajiri zinanufaika na mfumo wa uchumi wa ulimwengu na zimeweka mirija ya kuchukua rasilimali za nchi maskini. 

Kwa hiyo badala ya ajira kujengwa ndani, faida ya uwekezaji wa nchi tajiri kwa nchi maskini inakwenda kuwekezwa nje (exploitation by repatriation).  Kwa hiyo, sera hizi za uwekezaji katika uchumi wa kidunia wa soko huria, mtaji una hama, na faida inayojengwa haiwekezwi ndani ya nchi maskini bali inakwenda nje ya nchi hizo kujenga ajira nje. 

Je, ni kweli watu hawafanyi ujasiriamali? Leo hii tunaona namna ujasiriamali unavyotukuzwa kama vile watu hawa hawaufanyi wakati ukipita mitaani utaona wamachinga, mama lishe na baba lishe na wafanyabiashara wengine wapo. 

Lakini wanaoitwa wahamasishaji na wanasiasa wanalipigia debe suala hili kwa kiasi kikubwa. Lakini jamii inaonyesha kuwa wanajiajiri na si jambo jipya watu kujiajiri na ndiyo imekuwa historia ya binadamu kutafuta majawabu ya maisha yake. 

Ila linavyozungumzwa na kunadiwa kama ni kitu kipya kisichowahi kutokea wala kufanyika katika dunia hii. Hoja hii ya ujasiriamali haiondoi kuwa kuna haja ya kuwa na uchumi utakaozalisha ajira kwa wananchi wake na si ajira tu, bali ajira zenye kujenga taifa hilo. 

Kwa sababu suala si kuandaa watu waajiriwe katika soko, bali kuandaa wananchi wawe sehemu ya uzalishaji wa nchi yao.

Kwa hiyo hoja zilizopo ni za kubadili mitaala ili kuwafanya wahitimu waajiriwe na hoja ya kujiajiri wao wenyewe. Lakini tunapaswa kufanya ajira iwe matokeo ya uzalishaji wa kijamii. 

Yaani watu wanavyoshiriki katika uzalishaji wa nchi yao ndiyo ajira nayo inatengenezwa. Kumuandaa kijana katika soko aajiriwe ni dhana ya kibepari ya kumfanya binadamu kama bidhaa aweze kuuzwa na kununuliwa.

Dhana hii haifanyi ajira kuwa ni jambo la kijamii, bali mtu binafsi na ndiyo maana ubepari unatenganisha kati ya ajira na jamii. 

Napendekeza tuwe na uchumi wa kitaifa, uchumi utakaozingatia suala la uzalishaji wa ajira kwa wananchi wake kwa maana utajenga viwanda vya ndani, utatumia malighafi za ndani na utatumia teknolojia rahisi itakayozalisha ajira.

Mwandishi wa makala hii ni Mhadhiri Msaidizi wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).

0659-639808/0683-961891

[email protected]