DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi 

Tanzania inajulikana kuwa ni nchi ya wakulima na wafanyakazi. Alama katika bendera ya TANU na baadaye CCM ni jembe na nyundo. Alama ya jembe inawakilisha wakulima na nyundo inawakilisha kundi la wafanyakazi katika taasisi za umma na sekta binafsi.

Mbali na makundi hayo makubwa kuna kundi la wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo na wakubwa wa madini, wafanyabiashara na wajasiriamali.

Zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania hujishughulisha na kilimo. Idadi kubwa ya wakulima hapa nchini huishi vijijini mbali na kulima kundi hilo pia hujishughulisha na ufugaji na uvuvi kwa wale wanaoishi katika maeneo ya karibu na bahari, maziwa na mito.

Baada ya kupata Uhuru wetu mwaka 1961, Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere pamoja na mambo mengine ilitilia mkazo mkubwa katika sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyama vya ushirika katika kanda na mikoa mbalimbali hapa nchini.

Pia ikaanzisha ranchi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kufuga ng’ombe. Yote hayo yalikusudia kuongeza uzalishaji wa malighafi zitokanazo na kilimo na mifugo kwa ajili ya viwanda vya ndani na nje ya nchi. 

Sekta ya kilimo inaelezwa kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi. Katika hatua ya kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kilimo kwa uhai wa nchi, Nyerere alikuja na sera ya kilimo cha kufa au kupona.

Sera hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa wananchi kulima kwa bidii kwa malengo ya kupata chakula cha kutosha na kupata mazao ya biashara kwa ajili ya kujipatia kipato kwa njia ya kuyauza mazao na kuinua uchumi.

Kadiri miaka ilivyosonga mbele, kilimo kiliendelea kuwa ajenda ya kitaifa huku mazao ya biashara kama vile mkonge, kahawa, chai, tumbaku na pamba yalipewa kipaumbele kikubwa na yalilimwa katika mashamba makubwa ya umma na watu binafsi, lengo kubwa likiwa ni kukuza biashara ya ndani na nje ya nchi, hatua iliyosaidia kututangaza katika ulimwengu wa biashara.

Tanzania ilisifika kwa kilimo cha mkonge duniani huku ikiwa miongoni mwa nchi chache za Afrika maarufu kwa ufugaji wa ng’ombe. 

Uzalishaji wa mazao ya chakula, biashara na ufugaji ulitoa fursa kwa serikali kuanzisha viwanda vingi huku malighafi nyingi zikizalishwa hapa nchini.

Kila awamu ya uongozi imekuwa na jitihada mbalimbali katika kuleta mapinduzi ya kilimo. Jitihada zinazoelezwa kutofautiana nguvu katika kuhimiza na kuweka kipaumbele kwenye sekta muhimu ya kilimo kwa maendeleo ya nchi.

Serikali ya Nyerere ilianzisha Azimio la Iringa la Siasa ni Kilimo (mwaka 1972) huku lengo na madhumuni yake ilikuwa ni kupata wataalamu watakaotoa elimu juu ya kilimo bora, kutafuta masoko na kuboresha miundombinu kwa ajili ya wakulima nchini.

Serikali ya Rais Jakaya Kikwete ilikuja na kaulimbiu ya kilimo kwanza na kuibuka na sera ya utekelezaji wa maendeleo ya haraka kupitia mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika wizara sita ikiwamo Wizara ya Kilimo.

Sera hiyo ya kilimo kwanza ilileta msukumo katika sekta ya kilimo ingawa utekelezaji wake haukufikia malengo makubwa baada ya kuachwa njiani na Serikali ya Rais Dk. John Magufuli baada ya kuja na sera ya Tanzania ya viwanda na kuachana na BRN.

Wakati Serikali ya Magufuli ikitekeleza sera ya Tanzania ya viwanda kwa kujenga viwanda vipya na kufufua vya zamani, baadhi ya wakulima na wafanyabiashara wa mazao mbalimbali wamepata changamoto ya masoko kwa ajili ya mazao yao.

Sekta ya kilimo ni moyo wa uchumi wa Tanzania na takwimu zinaonyesha inachangia asilimia 26.6 katika pato la taifa na asilimia 24 katika bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi huku ikiajiri asilimia 66.3 ya nguvu kazi hapa nchini.

Pamoja na uchumi huo, sekta hiyo imeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo zana duni, uhaba wa masoko kwa ajili ya mazao, muundombinu, pembejeo, ufinyu wa bajeti inayotengwa kwa ajili ya Wizara ya Kilimo na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa hotuba za bajeti kuu na ya kilimo kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, bajeti ya kilimo bado iko chini ya asilimia moja katika bajeti kuu.

Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Wizara ya Kilimo ilitengewa kiasi cha Sh bilioni 267.87 sawa na asilimia 0.86 na kushuka katika mwaka wa fedha  2018/2019 kwa kupatiwa Sh bilioni 170.2 sawa na asilimia 0.52 ya bajeti yote. 

Bajeti ya kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 ilikuwa Sh bilioni 252.85 sawa na asilimia 0.77 huku  Sh bilioni 294.16 sawa na asilimia 0.81 zilitengwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Katika mijadala ya mapendekezo ya mwongozo wa Mpango wa Maendeleo wa Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 unaohusu kutenga bajeti ya Sh trilioni 39, baadhi ya wabunge na Spika wa Bunge, Job Ndugai, wamepaza sauti kutaka kilimo kipewe kipaumbele.

“Ilani ya uchaguzi inasema tunatakiwa hadi mwaka 2025 tuwe na hekta milioni 1.2 za umwagiliaji lakini hadi sasa tunazo 600,000 tu. Nilitarajia katika mpango kutakuwa na walau hekta 150,000 kama mradi wa kielelezo. Sipendi miradi hiyo lakini inawagusa wengi ambao ni maskini katika nchi hii? Hebu tubadilishe mwelekeo,” aamenukuliwa Nape Nnauye ambaye ni Mbunge wa Mtama (CCM).

Nape anapendekeza kuanzishwa kwa mfuko wa  ruzuku ya mazao utakaosaidia kuzikabili changamoto zinazojitokeza, mfano kupanda kwa bei ya mbolea hivi sasa na kuporomoka kwa bei ya mahindi.

“Kwa kuwasikiliza wabunge tangu wameanza kuchangia mpango huu, tunaomba mawaziri wahusika mwende mkaufumue kabisa, kipaumbele cha kwanza kiwe kilimo. Bunge letu la miaka hii mitano tulisema tunataka tufanye kitu katika kilimo. Tusipokuwa na mpango unaoshughulika na kilimo cha biashara  tutakuwa na tabu kidogo,” anasema Ndugai.

Kama hiyo haitoshi, Rais Samia Suluhu Hassan anasema hali ya kupanda kwa joto nchini imesababisha ukame unaoathiri sekta zinazotegemea maliasili  ambazo ni kilimo, uvuvi na misitu zinazochangia asilimia 30 ya Pato la Taifa na kuathiri asilimia 60 ya wananchi.

Samia ametoa kauli hiyo aliposhiriki mkutano uliojadili athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuza juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.

“Tupo katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni ugonjwa wa Uviko -19 ulioangusha uchumi na kufuta mafanikio  yaliyokwisha kufikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga  jamii zetu,” anasema Samia.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani, Joe Biden, anasema serikali yake itachangia dola 100 bilioni za Marekani katika mfuko wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa (UN) zitakazokwenda kusaidia nchi maskini zinazokabiliwa na tatizo hilo.

Pia hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa tahadhari kuhusu upungufu wa mvua za msimu unaoweza kujitokeza katika baadhi ya maeneo mbalimbali hapa nchini.

Tahadhari hiyo imekuja wakati wakulima wengi katika maeneo mengi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini wakiwa tayari wametayarisha mashamba yao kwa kuanza kwa msimu wa mvua.

Kutokana na utabiri huo ni vema kwa serikali na wakulima kuanza kujiandaa na athari zinazotokana na ukame huo ambao si tu utaathiri uzalishaji wa chakula  bali pia biashara na kuyumba kwa uchumi wa nchi. 

Wataalamu wa hali ya hewa  na wale wa kilimo wanapaswa kutoa elimu na ushauri kwa wakulima na wananchi kwa ujumla juu ya changamoto hiyo na kueleza aina ya mazao yanayopaswa kupandwa  kukabiliana na ukame na umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji.

Mabadiliko ya tabianchi yawekwe katika orodha ya  majanga ya kitaifa na kupewa uzito unaostahili na kamwe suala hili lisichanganywe na siasa.

0755-985966

220 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!