DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Watu wengi husita au hushindwa kuingia katika biashara wakitishwa na hatua zinazofahamika katika kuanzisha biashara husika, mbali na hofu iliyozuka kwa sasa ya vita kati ya Urusi na Ukraine.

Hatua hizo ambazo ni sawa na ‘amri za uanzishaji biashara’ huanza na kwanza kupata eneo sahihi la kufanyia shughuli na kutafuta leseni.

“Yaani uwe na chumba maarufu kama ‘fremu’. Hiki ni kikwazo kwa wengi, kwa kuwa mbali na ulazima wa kuwa na mtaji, mwekezaji mpya atapaswa kuwa na fedha za kulipia fremu kwa miezi mitatu, sita wakati mwingine hata mwaka mmoja!

“Unalipiaje sehemu tena kwa fedha nyingi bila hata kujua mwenendo wa biashara unayotaka kuianzisha?” Huwa ni swali ambalo wengi hujiuliza.

Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Daud Mbaga, anasema katika kampuni hiyo ya serikali inayojihusisha na uwekezaji, hatua hizo za uanzishwaji biashara si kikwazo kwa mwekezaji mpya na anaweza kuanzisha biashara hata sasa bila hofu iliyoikumba dunia ya vita kati ya Urusi na Ukraine; janga lililokuja duniani baada ya corona.

“Ukiwa na mtaji, hata wa Sh 10,000 tu unaweza kuanza uwekezaji. Nimesema Sh 10,000 lakini hata mtaji ukiwa mkubwa zaidi, tuseme Sh 500,000, unaweza kuwekeza bila kuwa na fremu,” anasema na kuendelea:

“Kupitia uwekezaji wa pamoja huhitaji fremu, leseni ya biashara au hata kijana wa kukusaidia kuuza duka au genge. Wa kazi gani? Uwekezaji kupitia kwetu ni ule usio na hofu wala ‘stress’.

“Unawekeza fedha zako na kuendelea na shughuli nyingine zenye tija kwako na kwa taifa zima,” anasema.

Huu ndio uwekezaji wa pamoja unaosimamiwa na UTT AMIS kupitia mifuko yake, ambao kwa miaka mingi umewavutia Watanzania wengi na kuwasaidia kuinua uchumi wao na kuwa na uhakika wa maisha bora.

Mifuko hii ni chombo cha uwekezaji kinachokusanya fedha kutoka kwa watu na kampuni mbalimbali ili kupata mtaji mkubwa ambao aghalabu huwekezwa kwenye kampuni zilizo chini ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

“Maeneo mengine ya uwekezaji ni akaunti za muda maalumu za benki, hati fungani – mkataba maalumu wa mkopo wa serikali au kampuni binafsi. Hati fungani zipo za muda mfupi na za muda mrefu.

“Ukiondoa hisa, fedha nyingi za uwekezaji huwekezwa kwenye mikopo yenye mkataba maalumu na ambapo hatari ya kupotea ni ndogo sana. Mfano mikopo kwa serikali ambayo kwa kawaida haina hatari au kama zipo ni kidogo na mara nyingi ni zilizo nje ya uwezo wa binadamu.

“Kila mfuko una kanuni zilizoainishwa kwenye waraka wa makubaliano, ni wajibu wa mwekezaji kuzisoma na kuzielewa ili ajue haki zake, na ni tahadhari gani achukue kabla ya kuwekeza,” anasema Mbaga.

Anasema fedha zinazowekwa kwenye mifuko ya kampuni hii husimamiwa na meneja mwenye utaalamu wa uwekezaji; hivyo: “Kuwapa nafasi waliokusanya kuendelea na shughuli zao nyingine.”

Meneja huyo hufanya uwekezaji kwa niaba yao chini ya masharti waliyojiwekea kwenye Mkataba wa Makubaliano (Memorandum of Understanding) na Mbaga anasema:

“Meneja huzitawanya fedha kitaalamu; ananunua hisa, hati fungani na anakopesha benki mbalimbali. Faida inayopatikana ni ya wawekezaji, yeye anatoza tozo ya usimamizi tu.”

Fedha hizo hugawiwa katika vipande (hisa) ambapo anayetaka kukuza uwekezaji hununua vipande zaidi na akizitaka fedha zake, anaviuza.

Faida zake

Kutawanywa kwa mtaji uliokusanywa na meneja katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji husababisha sehemu moja kama hailipi, kufidiwa na sehemu nyingine zinazolipa.

“Kidole kimoja hakivunji chawa. Mkikusanya fedha pamoja mnakusanya mtaji mkubwa unaowawezesha kufanya biashara ambayo ungekuwa peke yako usingeiweza. Pia wingi wa fedha huongeza nguvu ya majadiliano sokoni. Mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama,” anasema.

Mbaga anasema mfuko unapokuwa na fedha nyingi huleta unafuu katika gharama.

“Yaani inakuwa kama vile ununuzi kwenye duka la jumla. Kawaida duka la jumla bei huwa ni tofauti na la rejereja. Kwa sababu wawekezaji ni wengi, ina maana gharama kwa kichwa zinapungua pia, yaani gharama zinabebwa kwa umoja, tofauti na mwekezaji kama angekwenda mwenyewe,” anasema.

Anasema meneja huwa na wataalamu waliobobea ambao kila siku hufuatilia taarifa za soko.

“Wataalamu hawa huangalia mambo mengine mbalimbali. Hufanya upembuzi yakinifu kabla ya kuwekeza popote. Mfano, kabla ya kununua hisa kwenye kampuni fulani, huangalia historia ya kampuni hiyo, uwezo wa kifedha, ushindani, uongozi, uchumi, masoko kiujumla, matarajio ya baadaye na mambo mengine kadhaa,” anasema.

Ofisa huyo anasema pamoja na faida nyingi, uwekezaji huu sawa na mwingine wowote hukumbwa na changamoto, ikiwamo kutoweza kumhakikishia mwekezaji kupata asilimia fulani kila mwaka.

“Hii ni kwa sababu faida hutegemea rejesho la kule meneja alikowekeza. Kama ni kwenye hisa, mwaka huu zinaweza kulipa tofauti na mwaka ujao.

“Pia zipo tofauti za riba kati ya benki na benki ambazo huathiri rejesho kwa meneja,” anasema.

Anazitaja changamoto nyingine kuwa husababishwa na ‘MoU’ ambapo kwa namna yoyote ile, meneja hatakiwi kuwekeza maeneo nje ya yale yaliyomo kwenye mkataba huo.

“Meneja anakosa uhuru! Hata akiona fursa ya kupata faida eneo fulani, hana cha kufanya,” anasema na kusisitiza kuwa kutokana na ukweli kuwa meneja ni binadamu, pia anatakiwa kusimamiwa vema asiingize matakwa binafsi kwenye biashara.

Hapa anataja uwepo wa usimamizi wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji Tanzania (CMSA).

Masoko haya ya fedha pia hukumbwa na majanga na kuathiri mtiririko wake kama ilivyo sasa ambapo dunia imekumbwa na janga la vita ya Urusi na Ukraine.

“Mafuriko, matetemeko ya ardhi, mfumuko wa bei, kupungua kwa thamani ya fedha na mambo mengine mengi tu. Katika hali kama hii, mwekezaji anashauriwa kuwa na subira.

“Majanga huwa hayadumu, hupita kadiri muda unavyokwenda. Juhudi za meneja na jitihada za wadau, huyarekebisha na hali hurejea kuwa shwari,” anasema Mbaga.

Riba inaweza kuwa changamoto kwani kuna nyakati hupanda au kushuka na kwa kuwa riba ni gharama ya mkopo, ikiwa juu wakopaji hupungua na ikishuka huongezeka.

Hatari nyingine inayotajwa kuwapo kwenye uwekezaji huu ni pale ambapo kutokana na meneja kukosa uangalifu, hutokea akawa hana fedha za kutosha kuwalipa wawekezaji wanapozihitaji.

“Kukabiliana na hili, utaalamu wa hali ya juu hutumika kuhakikisha fedha zinawekezwa sehemu zinakoiva mara kwa mara na ndani ya muda mfupi.

“Pia kuwapo pembeni fungu ambalo malipo yakihitajika, meneja anachukua fedha ndani ya muda mfupi na kulipa mara moja kwa mujibu wa misingi husika,” anasisitiza.

Kama alivyosema awali, kiasi kidogo huwekezwa kwa kampuni binafsi ambazo zimefanyiwa upembuzi wa kutosha tena kampuni anuai.

Zipo pia hatari za kisiasa na kiuchumi, mfano mapinduzi ya kijeshi na kuyumba kwa uchumi.

Uwekezaji unaovuka mipaka nao ni hatari, kwani thamani ya fedha ya nchi moja inaweza kuwa kikwazo hasa katika kupanda na kushuka kwa kiwango cha kubadili fedha.

Mwanga anazungumzia mabadiliko ya kodi akisema yanaweza ama kuufanya uwekezaji uvutie na kuwa rahisi au wenye kukatisha tamaa na mgumu.

“Kodi ni gharama kwenye uwekezaji, zikiwa ndogo zinavutia wawekezaji na zinafanya mazingira yawe rafiki,” anasema.

UTT AMIS husimamia mifuko sita ya uwekezaji wa pamoja, ambayo ni mfuko wa umoja, watoto, wekeza maisha, jikimu, ukwasi na hati fungani.

Historia ya mifuko yote ni hadithi nzuri kwa wawekezaji wote wa kipindi cha kati na kirefu. Hayupo hata mmoja aliyepata hasara na leo hii mifuko hii imekuwa chaguo na kimbilio la Watanzania wengi. 

Kumbuka kuna namna tatu za kupata pesa kwenye uwekezaji wa pamoja, kwanza kabisa unaweza kuchagua kupata gawio ambalo litatokana na faida itokayo kule meneja anakowekeza.

Pili, ni kuwa na faida inayoongeza thamani ya mtaji na mtaji utaongezeka kwa kasi kama huchukuwi gawio, kwa sababu gawio nalo linakuwa sehemu ya uwekezaji. 

Kama unachukua gawio bado mtaji utaongezeka lakini kwa kiasi kidogo. Na mwisho, faida inatokana na ongezeko la thamani ya vipande, thamani inaongezeka kutokana na mchango wa faida inayotokana na uwekezaji.

0712 625 310

By Jamhuri