Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

Ipo hofu ya kuzuka kwa vita ya tatu ya dunia, hali hiyo ikichochewa na matamshi ya Rais Joe Biden wa Marekani na matendo ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, hasa kuhusu vita ya Ukraine.

Vikwazo inavyowekewa Urusi vimeyageukia mataifa ya Magharibi na kuanza kutikisa uchumi wa nchi hizo, ambapo nchi hizo ikiwamo Marekani zimeanza kuhujumu mikakati ya Urusi nchini Ukraine ili kulinda sarafu yake isiporomoke.

Hatua mojawapo iliyofikiwa na mataifa hayo ni kuihakikishia Ukraine misaada ya kivita kama vile silaha za kivita na fedha kwa ajili ya kuendeleza vita hiyo.

Zipo tetesi za majeshi ya Urusi kumkamata ofisa wa juu wa jeshi la Marekani nchini Ukraine ambaye alikuwa akiongoza kikosi cha majeshi ya Ukraine cha Azov, hali inayozidisha hisia kwamba huenda Marekani inashiriki kwenye vita hiyo kwa kificho.

Hata hivyo taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo zimefichwa na Serikali ya Marekani kwa kuziondoa taarifa zote zinazomhusu kiongozi huyo na kuweka taarifa zinazoonyesha kuwa amefariki dunia Machi 28, mwaka huu. 

Pia upo mpango wa Marekani kutaka kuitumia Ukraine kujenga ngome kubwa karibu na mataifa ya Urusi na China kwa lengo la kuyadhibiti kinguvu, hali inayokoleza hofu ya kuzuka kwa vita ya tatu ya dunia.

Mpango huo unaelezwa kwa kuhakikisha vita inayoendelea nchini Ukraine inachukua muda mrefu kumalizika ili kuidhoofisha Urusi ndipo lengo hilo la kujenga ngome katika taifa hilo liweze kutekelezwa.

Rais Biden tayari ameomba bunge la bajeti la nchi hiyo kupitisha takriban dola bilioni 813 alizopendekeza ipewe Wizara ya Ulinzi, Pentagon, kwa mwaka wa fedha 2022/23 kutoka kwenye bajeti ya dola bilioni 773 iliyokuwa imeombwa awali.

Kitisho cha njaa Marekani, Ulaya 

Marekani inakabiliwa na mfumuko wa bei za vitu hasa vyakula, vikiwamo vya mifugo na katika baadhi ya maeneo maelfu ya mifugo imeanza kufa kwa kukosa chakula.

Baadhi ya wafugaji wanalazimika kuichinja mifugo yao na kusababisha nyama kuwa nyingi sokoni baada ya kushindwa kumudu gharama za kununua chakula cha kuilisha.

Hali ikiendelea hivyo nchini humo kwa siku za usoni, inatabiriwa kuwa bidhaa kama maziwa, siagi na Yogurt vitapatikana kwa bei kubwa kutokana na mifugo ambayo ndicho chanzo kikuu cha bidhaa hizo kupungua.

Wakati hali ikiwa hivyo nchini Marekani, Bara la Ulaya limo kwenye mgawo rasmi wa vyakula hasa ngano na mafuta ya kula, hasa alizeti, ambayo yameadimika kutokana na kushindwa kuyaagiza Urusi na Ukraine, ambao ndio wazalishaji wakubwa.

Baadhi ya ‘super market’ za vyakula barani humo inadaiwa zinafunguliwa kwa musimu na vyakula kuuzwa kwa bei kubwa.

Kupanda kwa bei duniani kumeanza kuchochea maandamano ya wananchi nchini Peru, Sri Lanka, Hispania na mataifa kadhaa ya Mashariki ya Kati.

COVID – 19 yahusishwa uhaba wa chakula duniani

Vita ya Urusi nchini Ukraine imekuwa kama sababu ya kuzidisha bei za vyakula duniani kote lakini kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo dunia imeshuhudia mfumko wa bei hizo ulioanza kuibuka baada ya kuibuka kwa mlipuko wa virusi vya corona.

Virusi vya corona vilianza kusambaa duniani tangu mwaka 2019, vikianzia katika mji wa Wuhan nchini China, ambapo vimesababisha vifo vya watu takriban milioni sita duniani kote na kuacha mamilioni ya watu wakijifungia ndani kwa miaka mitatu mfululizo bila kufanya kazi za uzalishaji.

Uwepo wa gonjwa hilo na hali ya vita nchini Ukraine kunaiweka dunia kwenye kipindi kigumu na usalama wa chakula duniani unatarajiwa kuwa mbaya mno siku za usoni.

Urusi yabadili mbinu kukwepa vikwazo

Kitendo cha mataifa ya Magharibi kuiondoa Urusi kwenye mfumo wa kimataifa wa malipo wa SWIFT na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi, vimesababisha imepoteza dola za Marekani bilioni 300 ambazo zimezuiliwa kwenye akaunti za benki zilizoko katika mataifa mbalimbali duniani.

Kitendo hicho kimechukuliwa na Urusi kama wizi wa wazi ambao umefanywa na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani.

Baada ya kujibu mapigo kwa kuyataka mataifa yasiyo rafiki kununua bidhaa zake kama mafuta, gesi, ngano na mbolea kwa sarafu ya Ruble na dhahabu sasa imepanga kudhibiti fedha zake kwa kufanya uwekezaji kwenye sarafumtandao, Cryptocurrencies.

Sarafumtandao ni kitu gani?

Cryptocurrency ni sarafu iliyogunduliwa na kikundi kinachojiita Satoshi Nakamoto mwaka 2008, ambacho kililenga kubadilishana fedha kwa njia ya kompyuta kwa kutumia mifumo ya kidijitali.

Hadi sasa nchi ambayo imekwisha kuhalalisha matumizi ya sarafu hiyo kama mfumo halali wa kubadilishana fedha ni El Salvador, taifa linalopakana na nchi ya Honduras kwa upande wa kaskazini mashariki na Guatemala kwa upande wa Kusini magharibi.

Sarafumtandao inatajwa kusafirisha taarifa za kifedha kwa kutumia teknolojia inayoitwa, ‘Cryptography’ ambayo huwawezesha watu kutumiana fedha katika mfumo wa kidijitali pasipo kuhitaji kuhusishwa kwa mifumo ya kibenki.

Namna ya kuweka na kuhesabu fedha katika mfumo huo inaitwa ‘mining’, ambapo kwa kutumia mfumo unaoitwa ‘block chain, ukiweka fedha zinakuwa salama zaidi.

Mfumo wa block chain umeimarishwa kiasi kwamba hakuna mtu anaweza kuuingilia, ‘hack’, kubadilisha wala kufanyiwa udanganyifu wa kimtandao.

Mitandao ya kimataifa ambayo imeanza kutumiwa kutoa huduma ya sarafumtandao ni Bitcoin, Ethereum na Litecoin.

Neno Cryptocurrency linatokana na neno lenye asili ya lugha ya Kigiriki, ‘Kryptos’ likimaanisha ‘kilichofichwa’.

Marekani kuja na Digital Dollar

Rais Biden Machi 9, mwaka huu alikaririwa akiwahimiza wataalamu wa masuala ya kifedha nchini humo kujifunza namna ya kufanya uwekezaji wa kifedha kwa kutumia sarafumtandao.

Biden aliwahimiza wataalamu hao kujifunza kwa kina mifumo yake inavyofanya kazi na kuweka wazi nia yake ya kuitambulisha sarafumtandao itakayojulikana kama Digital Dollar.

Hatua hiyo inatajwa kama njia ya kutaka kupambana na sarafu ya Ruble ya Urusi na Yuan ya China, ambazo mataifa hayo yamekubali uwekezaji wake kuwekwa kwenye sarafumtandao.

Kitendo cha China kuendelea kushirikina na Urusi kibiashara kimesababisha sarafu ya Ruble iliyokuwa imeanguka baada ya kuwekewa vikwazo kuanza kuimarika na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya dola ya Marekani na sarafu ya Euro inayotumika barani Ulaya.

China na Urusi zote zimefanikiwa kuunda mifumo yao ya kimataifa ya malipo ya fedha ambayo ni mbadala wa mifumo inayotumia dola kama Swift.

Urusi inatumia mfumo wa STFM kupokezana Ujumbe wa Kifedha katika benki zake zilizo nje ya mipaka, huku China yenyewe ikitumia mfumo wa CIPS.

Hatua hiyo inatoa changamoto kwa mfumo wa SWIFT unaotumia dola ya Marekani na kuzua hofu mgogoro wa Ukraine kutumiwa kama njia ya kuibuka kwa vita ya tatu ya dunia.

By Jamhuri