DAR ES SALAAM

NA MWANDISHI WETU

Biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani imeanza kuimarika baada ya miaka mitatu ya mdororo kutokana na
kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uagizaji wa bidhaa na huduma mbalimbali kutoka nje, JAMHURI limebaini.
Kuimarika huko ambako ni moja ya viashiria vya uchumi kufanya vizuri, kumechangiwa sana na kuongezeka kwa mauzo ya nje ambayo sasa yanakaribia kufika dola bilioni 10 za Marekani kwa mwaka na kuboresha upatikanaji wa fedha za kigeni.
Hali ikiendelea hivyo, itasaidia kuimarisha thamani ya shilingi ambayo mwaka huu imekuwa na utulivu mkubwa dhidi ya fedha nyingi za kigeni, ikiwamo dola ya Marekani.
Vyanzo vingine vikubwa vya fedha za kigeni ni misaada na mikopo ya nje, pamoja na mitaji kutoka mataifa mengine ambavyo vimepungua sana miaka ya hivi karibuni.
Takwimu rasmi zinaonyesha kwamba kwa mwaka ulioishia Oktoba 2019, Tanzania iliuza na kununua nje ya nchi bidhaa
na huduma zenye thamani ya dola bilioni 20.4 za Marekani ukilinganisha na dola bilioni 18.7 kipindi kama hicho mwaka jana.
Katika kipindi hicho, mauzo ya nje yaliliingizia taifa fedha za kigeni zenye thamani ya dola bilioni 9.5, ongezeko la zaidi
ya asilimia 10 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 5.2 kati ya Septemba 2018 na Septemba 2019. Kiwango hiki cha mapato ni kikubwa zaidi ya hali ilivyokuwa miaka miwili iliyopita na ni karibu sawa na mauzo ya nje ya miaka mitatu
ya 2016, 2015 na 2014.
“Thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi zilikua kwa asilimia 10.3 na kufikia dola milioni 9,472.3 za Marekani mwaka ulioishia Oktoba 2019 kutokana na kiasi kikubwa na mapato ya huduma mbalimbali na bidhaa zisizo asilia,” Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema katika Tathmini ya Hali ya Uchumi kwa Mwezi (MER) ya hivi karibuni.
Utalii ndiyo sekta iliyoongoza kuzalisha fedha nyingi za kigeni huku dhahabu ikichangia asilimia 50.4 ya bidhaa asilia
kwa asilimia 39.3 ya mauzo ya bidhaa zote kwa ujumla.
MER hiyo mpya ya Novemba inayotathmini hali ya uchumi wa nchi kwa mwezi Oktoba inasema dhahabu ilifanya vizuri
kutokana na hatua za serikali kudhibiti kwa karibu shughuli za uchimbaji na mauzo ya madini nchini.
Mauzo ya nje mwaka wote wa 2018 yalikuwa dola milioni 8,386.2 baada ya kushuka kwa asilimia 3.2 kutoka dola milioni 8,664 zilizopatikana mwaka 2017. Mwaka 2015 na 2016, mapato ya fedha za kigeni yalikuwa dola milioni 8,921.9 na 9,381.6 mtawalia.
Thamani ya manunuzi kutoka nje ilikuwa dola milioni 10,338.2 mwaka 2018 na dola milioni 9,591.6 mwaka uliotangulia na taifa lilitumia dola milioni 10,797.4 mwaka 2016 na milioni 12,512.8 mwaka 2015 kwa ajili ya kununua bidhaa na huduma nje ya nchi.
Jumla ya biashara ya nje kwa mwaka ulioishia Oktoba 2017 ilikuwa dola bilioni 18.2, ikipungua kwa karibu asilimia 10
kutoka dola bilioni 20.2 mwaka 2016. Katika kipindi kama hicho mwaka 2015, mauzo na manunuzi nje ya nchi yalikuwa dola bilioni 22.1, kiasi ambacho kilikuwa karibu sawa na thamani ya biashara yote ya nje mwaka 2014.
“Gharama ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi ilikua kwa asilimia 7.3 hadi dola milioni 10,895.8 mwaka ulioishia
Oktoba 2019, hasa kutokana na uagizaji kwa wingi wa bidhaa,” Benki Kuu inasema kwenye ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, bidhaa zilizoagizwa kwa wingi kati ya Oktoba 2018 na Oktoba mwaka huu zilikuwa zile za
kukuza mitaji kama vile vifaa vya usafiri na ujenzi pamoja na mitambo. Bidhaa hizi na mafuta viliagizwa kwa wingi
kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkatati kama ujenzi wa Bwawa la Umeme la Nyerere na reli ya
kisasa (SGR).
Ripoti za BoT zinaonyesha kwamba thamani ya bidhaa na huduma zilizonunuliwa nje ya nchi ilishuka kutoka dola
milioni 13,487.5 mwaka ulioishia Oktoba 2014 hadi dola milioni 13,231.1 kipindi kama hicho mwaka uliofuata.
Mwaka ulioshia Oktoba 2016, manunuzi hayo yalishuka kwa kiasi kikubwa na kufika dola milioni 10,692.3 kabla ya
kupungua sana hadi dola milioni 9,516.6 kipindi hicho mwaka 2017

521 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!