ARUSHA

NA MWANDISHI WETU

Kampuni za bilionea raia wa Marekani, Dan Friedkin, zinazotikiswa na ukwepaji kodi, rushwa na uhujumu uchumi, zimekiri kuwa zinachunguzwa.
Hayo yakiendelea, imebainika kuwa kwa miaka 30 kampuni hizo hazijawahi kutangaza kupata faida; jambo linalotia shaka na kuibua maswali ya kwanini hazijafunga kazi zake kama miaka yote imekuwa ya hasara tu kwao.
Hata hivyo, imebainika kuwa mbinu hiyo inatumiwa kuhalalisha malipo ya mishahara minono wanayolipana kwa kificho kwenye benki za ughaibuni, pia kama mwanya wa kupata unafuu wa kodi nchini Marekani.
Uongozi wa kampuni hizo kupitia kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari umethibitisha kuwapo kwa ukaguzi unaofanywa na Kikosi Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hadi wiki iliyopita, kiasi cha fedha kinachodaiwa kutoka kwa kampuni hizo kimefikia dola milioni 36 za Marekani ambazo ni wastani wa Sh bilioni 82.
Kiwango hicho kinahusisha ukwepaji kodi kupitia mishahara minono wanayolipana wafanyakazi Wazungu kupitia akaunti mahususi zilizo nje ya nchi, ununuzi wa mali bila kulipa kodi stahiki, udanganyifu kwenye mikataba ya kazi na kadhalika.
Kampuni hizo zimetumia mamilioni ya fedha kujaribu kujisafisha kupitia vyombo vya habari zikitaka kuaminisha umma na ulimwengu yanayoandikwa juu yake ni ya kuzusha. JAMHURI lina vielelezo muhimu vinavyoonyesha namna kampuni za Friedkin zilivyoiumiza nchi kwa ukwepaji kodi kwa miaka zaidi ya 30.
Hivi karibuni kampuni hizo ziliweka Sh bilioni 5 kwenye akaunti maalumu ya Serikali ya Tanzania wakati majadiliano ya kiasi hali wanachopaswa kulipa yakiendelea.
Kashfa ya ukwepaji kodi nchini Tanzania imeitikisa Friedkin kwenye masoko ya hisa, na hata kwenye mpango wake wa kutaka kuinunua Klabu ya soka ya As Roma ya nchini Italia kwa dola bilioni 1 za Marekani (takriban Sh trilioni 2.2).
Kulipwa kwa Sh bilioni 5 ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Friedkin, Jean-Claude McManaman, kwa Kikosi Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kinachochunguza kashfa ya ukwepaji kodi.
Katika barua hiyo ya Novemba 8, mwaka huu, McManaman alisema Sh bilioni 5 zinawekwa kwenye akaunti hiyo wakati ambao bado mjadala wa uchunguzi kuhusu kiwango halisi cha kodi wanachodaiwa Friedkin ukiendelea.
Anaihakikishia serikali kuwa kampuni za Friedkin zitaendelea kutii sheria za nchi, na kwamba kukubali kwao kuweka kwenye akaunti kiasi hicho cha fedha kunathibitisha dhamira hiyo.
Kwenye barua anaeleza matumaini yake ya kuona wakurugenzi waliopokwa hati za kusafiria wanarejeshewa na wanaondolewa zuio la kusafiri nje ya Tanzania.
Msemaji wa kampuni za Friedkin, McManaman, mara zote amegoma kuzungumza na JAMHURI hata baada ya kuandikiwa maswali.
Wakurugenzi kadhaa walipokwa hati za kusafiria kama sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa hawakimbii wakati huu ambao serikali inafanya uchunguzi wa tuhuma za ukwepaji kodi kwa kampuni hizo.
Mbinu za ukwepaji kodi unavyofanywa na kampuni za bilionea Mmarekani, Friedkin, zimefichuka baada ya kubainika kuwa kwa miaka zaidi ya 30 serikali imekoseshwa mabilioni ya shilingi kupitia udanganyifu kwenye mishahara, uuzaji na ununuzi wa mali zikiwamo hoteli.
Nchini Tanzania, baadhi ya kampuni za Friedkin ni Tanzania Game Tracker Safaris Ltd (uwindaji wa kitalii), Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Ltd (uwindaji wa kitalii), Ker & Downey Safaris (Tanzania) Ltd (utalii wa picha), Northern Air Ltd (usafiri wa anga), Mwiba Holding Ltd (ranchi ya wanyamapori na utalii), na The Friedkin Conservation Fund (uhifadhi na maendeleo ya jamii).
Kikosi Kazi kilichoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kimebaini mwanya wa ukwepaji kodi ambao ni kupitia malipo ya mishahara na marupurupu manono wanayolipana wawekezaji hao.
Kwa kutumia akaunti zilizofunguliwa nje ya nchi (offshore accounts), Friedkin wanatuhumiwa kutumia kigezo cha kuajiri wataalamu wa kigeni ili kukwepa kodi. Mwaka 2008 fedha zilizowekwa kwenye akaunti hizo ni dola 963,879 za Marekani. Kwa kiwango cha sasa cha kubadilishia fedha cha wastani wa dola moja ya Marekani kwa Sh 2,300; hiyo ina maana mwaka huo fedha zilizohamishwa kwa mbinu hiyo ni Sh bilioni 2.216.
Mwaka 2009 dola 849,109 za Marekani (Sh bilioni 1.952) za mishahara ziliingizwa kwenye akaunti hizo; na mwaka 2010 kiwango hicho kilikuwa dola 578,798 za Marekani (Sh bilioni 1.331). Hii ina maana kwa miaka mitatu pekee kiwango cha fedha kilichohamishwa bila kukatwa Kodi ya Ajira (PAYE) na Kodi ya Uendelezaji Ufundi Stadi (SDL) ni Sh bilioni 5.499 ambazo kwa miaka 33 ni Sh bilioni 181.467.
Akaunti hizo zimefunguliwa katika Visiwa vya Cayman, Cyprus, Mauritius na Uswisi. Kampuni ya Kitanzania (jina tunalo) imekuwa ikishirikiana na kampuni nyingine za kimataifa kufungua akaunti mbalimbali za wafanyakazi wa kampuni za Friedkin. Baadhi ya washirika hao ni CIM Corporate Services iliyopo Mauritius.
Mambo mengine yaliyodaiwa kufanywa na kampuni za Friedkin ni ubaguzi wa mishahara kati ya wafanyakazi wageni na wenyeji bila kujali uwezo wao kitaaluma. Wafanyakazi wageni wanalipwa kiasi kidogo cha fedha hapa nchini, ilhali kiwango kikubwa kikiwekwa kwenye akaunti zao zilizofunguliwa ughaibuni.
Mkurugenzi Mkuu McManaman anapokea mshahara wa Sh 50,922,000 kwa mwezi. Mkurugenzi wa Operesheni wa Mwiba Holdings Limited, Russel Hastings analipwa mshahara wa Sh milioni 49 kwa mwezi. Sehemu kubwa ya mshahara huo haikatwi kodi kwa kuwa huingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zilizoko ughaibuni. Ofisa Mkuu wa masuala ya Fedha wa Kerr & Downey Limited, Nick Stubbs mshahara wake ni Sh milioni 43.
“Jambo la kusikitisha ni kuwa sehemu kubwa ya mishahara hii inalipwa offshore kwa hiyo haikatwi kodi wala tozo, lakini kwa wafanyakazi Watanzania ambao wanalipwa kidogo, kodi zote wanakatwa,” kimesema chanzo chetu.
Mchanganuo unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 hadi mwaka huu (2019), Hasting pekee amekwepa kodi ya wastani wa Sh milioni 840; na Stubbs ameikosesha serikali Sh milioni 744 kama kodi na tozo kutoka kwenye mshahara wake pekee.
Wakati wageni hao wakilipwa hivyo, kwa Watanzania walio kwenye ngazi ya umeneja mshahara wa kila mmoja ni wastani wa Sh milioni 9 pekee kwa mwezi; na baada ya makato hubaki na wastani wa Sh milioni 5.
Wafanyakazi wa ngazi ya chini kama vile wahudumu wanalipwa mshahara wa wastani wa Sh 400,000 hadi Sh 800,000 kwa mwezi na wanakatwa kodi zote za PAYE, SDL, WCF na NSSF. Pia imebainika kuwa kwa miaka yote 30 hakuna Mtanzania aliteuliwa kushika nafasi ya juu kwenye menejimenti ya kampuni za Friedkin hapa nchini.
Wawindaji Bingwa (PH) raia wa kigeni wanalipwa dola 12,000 za Marekani (Sh milioni 27.6) kwa mwezi; lakini waswahili wanaambulia dola 1,000 za Marekani (Sh milioni 2.3) tu kwa muda kama huo.
Kwa miaka yote hiyo, wafanyakazi wataalamu kutoka nje walioajiriwa na kampuni za Friedkin wamekuwa wakilipwa sehemu kubwa ya mishahara yao kwenye benki zilizo ughaibuni ili pamoja na mambo mengine, wasilipe kodi na tozo mbalimbali za kisheria hapa nchini.
Sehemu zinazotajwa kupelekwa fedha hizo ni katika Visiwa vya Bahamas kwenye taasisi za fedha za Adventure Services na AHIL Trust. Hayo yakiendelea, uchunguzi umeanza kwenye akaunti za Friedkin zilizoko Uswisi na Visiwa vya Cayman.
Wanaotajwa kuwa wanahusika kuidhinishaji fedha kutoka ofisi kuu za Friedkin zilizoko Houston Texas, Marekani ni Rais wa kampuni za Friedkin, Dan Friedkin; Mtendaji Mkuu, Marcus Watts; na Mwanasheria Mkuu, Kimberly Jacobson.
Kampuni za Friedkin zinatuhumiwa ukwepaji kodi kupitia malipo ya wakurugenzi; na ukwepaji kodi kwenye mikopo na uhamishaji fedha ndani ya kampuni.
Makosa mengine ni kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi wanaofanya kazi kama washauri, lakini wakiwa hawana vibali na  wala sifa za kitaaluma; na imebainishwa kuwa baadhi ya wafanyakazi — wamekutwa wakiwa na mishahara zaidi ya mmoja na kwa viwango tofauti. Pia hakuna makato kwa ajili ya mifuko ya hifadhi ya jamii.
Jingine ni mikataba kwa wataalamu kutoka nje ya nchi, hasa kwa Jean-Claude ambaye amekutwa akiwa na barua ya ajira, lakini ana mkataba mwingine kama mshauri.
Uchunguzi unaoendelea umefichua kuwapo kwa ubaguzi mkubwa kati ya wafanyakazi wa Friedkin kutokana na misingi ya rangi.
Wafanyakazi weupe wanalipwa vizuri zaidi kuliko wenzao weusi hata kama wanawazidi uwezo kitaaluma. Mishahara hiyo ya kibaguzi inalipwa kwenye akaunti za Wazungu zilizofunguliwa ughaibuni. Imebainika kuwa baadhi ya wageni hao hulipwa dola 18,000 kila mmoja kwa mwezi na bonasi. Fedha hizo huwa hazitolewi taarifa zake kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wakaguzi wa ndani ya Friedkin mara zote wamewaficha wanahisa na wakurugenzi wenzao Watanzania, lengo likiwa ni kutotaka kujulikana kwa mpango huo wa kibaguzi.
Wanahisa Watanzania waliothubutu kuhoji masuala mbalimbali ya utendaji wamekuwa wakiondolewa bila kulipwa stahiki zao. Kwa miaka 30, kampuni za Friedkin zimekuwa zikitangaza kupata hasara. Mwanasheri wa kampuni za Friedkin ni Lemmy Bartholomew wa Kampuni ya Mawalla Associates.
Kwa miaka 30, Friedkin wamekuwa wakitangaza kupata hasara inayofikia dola milioni 10 za Marekani kwa kila mwaka; ilhali ukweli ukiwa kwamba hasara inayotangazwa ndiyo hutumika kuwalipa wawekezaji hao mamilioni ya fedha kupitia akaunti zao zilizoko ughaibuni.
Marc Watts ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Friedkin na Kimberley Jacobson ambaye ni Mwanasheria, ndio wakurugenzi wa AHIL Bahamas – ambayo ni kampuni ya Friedkin ya offshore inayotumika kupeleka malipo kwenye akaunti za wawekezaji hao, hivyo kukwepa kodi; na kuwaacha Watanzania wakilipwa kiasi kidogo cha fedha na kukatwa makato yote ya kodi kisheria.
Watts ambaye ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Harvard, ni mjumbe wa bodi ya Dallas Federal Reserve Bank, taasisi ya kifedha ambayo hutaka wajumbe wake wawe watu waadilifu. Lakini ni yeye huyo huyo anayetuhumiwa kama kiongozi wa kampuni za Friedkin, kuendesha akaunti za fedha katika Visiwa vya Bahamas na Cayman, zinazotumika kuingiza fedha zisizolipiwa kodi nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wafanyakazi wa Friedkin jijini Arusha wamekieleza Kikosi Kazi kuwa wanazuiwa kuzungumza Kiswahili — lugha ambayo ni ya taifa. Pia kuna madai kuwa wafanyakazi wasiomudu kuzungumza Kiingereza vizuri wamekuwa wakifukuzwa au kuhamishwa.
Malalamiko mengine ni kuwa licha ya kuwapo nchini kwa muda wa miaka zaidi ya 30, Friedkin haijawahi kumwekeza mswahili kwenye menejimenti, badala yake nafasi hizo zimekuwa zikishikwa na weupe tu, hali inayotafsiriwa kuwa ni ubaguzi wa rangi.
“Tunashangaa kuona watu wasiokuwa na sifa wakipewa nafasi za ukurugenzi. Watu kama Alex Rechsteiner, Fabia Bausch, Nicolas Negre na Jean-Claude McManaman hawana ujuzi wowote wa kuwazidi waswahili lakini ndio wanaopewa nafasi za kuongoza,” anasema mmoja wa wafanyakazi.
Watu hao wanne wakitambuliwa kama “washauri”, pamoja na Russel Hastings, ndio wanaoongoza kampuni zote za Friedkin hapa nchini wakiwa wanawajibika moja kwa moja kwa Dan Friedkin na Marc Watts nchini Marekani.
 
.tamati…

By Jamhuri