Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha mchakato wa kufanya maboresho ya Sheria ya Elimu unakamilika ifikapo mwaka 2027 ili kuifanya iendane na mahitaji na mabadiliko ya sasa katika sekta ya elimu nchini.

Kauli hiyo imetolewa Leo Mei 21,2026 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya awali ya Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 kwa wadau mbalimbali wa elimu.

Profesa Mkenda amesema serikali inaendelea kutekeleza maboresho makubwa katika sekta ya elimu kupitia sera, mitaala, ongezeko la walimu, uboreshaji wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa vitendea kazi kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.

Amesema baada ya kuzinduliwa kwa sera mpya ya elimu, hatua inayofuata ni kuhakikisha sheria ya elimu inafanyiwa maboresho ili kuendana na mwelekeo mpya wa mfumo wa elimu nchini.

“Lengo la kikao hiki ni kupata maoni ya wadau kuhusu mapendekezo yaliyofanyiwa kazi. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 imepitia marekebisho mbalimbali, lakini sasa tunahitaji maoni yatakayosaidia kuamua kama tuwe na sheria mpya au kuendelea kuiboresha iliyopo,” amesema Profesa Mkenda.

Ameongeza kuwa maoni yatakayopatikana kutoka kwa wadau yatawasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kwa hatua zaidi za uamuzi.

Waziri huyo pia aliwapongeza wadau wa elimu kwa kuendelea kushiriki katika mchakato wa kutoa maoni yenye lengo la kuimarisha mfumo wa elimu na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Caroline Nombo amesema wizara ipo tayari kuyapokea, kuyachambua na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayowasilishwa na washiriki.

Amewahimiza wadau kutumia nafasi hiyo kutoa maoni kwa uwazi na weledi ili kusaidia kupatikana kwa sheria bora yenye tija kwa taifa.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema ucheleweshaji wa mchakato huo umetokana na nia ya kuhakikisha sheria itakayopatikana inazingatia maoni ya wananchi na wadau wengi zaidi.

Amesema kutokana na Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kudumu kwa muda mrefu, ipo haja ya kupata maoni yatakayosaidia kuandaliwa kwa sheria imara na endelevu itakayolinda maslahi ya taifa kwa vizazi vijavyo.