Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

SERIKALI mkoani hapa imewahamasisha Watanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kuchangia Mfuko wa Kusaidia Matibabu ya Figo na Uroto ulioanzishwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa lengo la kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa huduma za kibingwa.

Mfuko huo unalenga kukusanya Sh bilioni 7 ndani ya kipindi cha miaka miwili ili kuwezesha wagonjwa wengi zaidi kupata matibabu ya upandikizaji figo na uroto ambayo yamekuwa na gharama kubwa kwa wananchi wengi.

Akizungumza leo Mei 21,2026 jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema hatua ya kuanzishwa kwa mfuko huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa tangu kuanza kutoa huduma zake.

Amesema hospitali hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za afya za kibingwa nchini na kupunguza utegemezi wa wagonjwa kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu.

Kwa mujibu wa Senyamule, hadi sasa zaidi ya wagonjwa 55 wamefanyiwa upandikizaji figo huku watoto 28 wakifanikiwa kupata huduma ya upandikizaji uroto kupitia hospitali hiyo.

“Huduma hizi zimeleta matumaini makubwa kwa wananchi na zimeonesha uwezo wa Tanzania katika kutoa tiba za kibingwa ndani ya nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna wagonjwa wengi wanaohitaji msaada wa kifedha ili waweze kupata matibabu hayo muhimu.

Senyamule amesema mchango wa kila Mtanzania unaweza kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaosubiri huduma hizo, hivyo jamii inapaswa kuendelea kuiunga mkono BMH katika juhudi zake za kuboresha sekta ya afya.

Aidha, amesema uwekezaji unaofanywa na hospitali hiyo umeifanya Tanzania kuendelea kujijengea sifa kama kitovu cha huduma za afya za kibingwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo (BMH), Henry Humba, amesema maadhimisho ya miaka 10 yanalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha huduma muhimu za kibobezi nchini.

Amesema huduma za upandikizaji figo na uroto ni miongoni mwa huduma za gharama kubwa, hivyo mfuko huo umeanzishwa ili kusaidia wananchi wenye uhitaji kupata matibabu kwa urahisi zaidi.

“Maadhimisho haya ni sehemu ya kuunga mkono Serikali katika kuhakikisha huduma za kibingwa zinaimarishwa zaidi, na kupitia hatua hii tunataka kuendeleza jitihada zilizokwishaanzishwa,” alisema Dk. Humba.

Ameongeza kuwa hospitali hiyo imeamua kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya na maendeleo ili kuhakikisha mfuko huo unafanikiwa, huku akisisitiza kuwa changamoto zilizopo hazipaswi kuwa kikwazo kwa wananchi kupata huduma.

Amebainisha pia mchango wa awali wa Sh bilioni 1 uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha huduma hizo za kibingwa.