KIBAHA

Na Costantine Muganyizi

Baada ya kuimarika na kufikia wastani wa zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.5 mwanzoni mwa muongo huu, kiasi cha biashara kati ya Tanzania na India kimeshuka sana miaka ya hivi karibuni.

Kiasi hicho cha thamani ya biashara kwa mwaka kati ya mataifa haya rafiki ni sawa na Sh trilioni 5.75 kwa viwango vya soko vya ubadilishaji wa shilingi dhidi ya dola vya sasa. 

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, hali hasi ya biashara imeanza mwaka 2018 na kuwa mbaya zaidi mwaka 2020, hasa kutokana na changamoto za janga la Uviko-19 ambalo linaendelea kuuvuruga uchumi wa dunia.

Wakati thamani ya biashara kati ya India na Tanzania ilikuwa dola za Marekani bilioni 3.76 (Sh trilioni 8.65) mwaka 2014, mwaka jana ilikuwa takriban dola za Marekani bilioni 1.61. 

Hili ni sawa na anguko la asilimia 57.1, kiwango ambacho ni dhahili kinaashiria kudorora kwa biashara.

Ili kukabiliana na changamoto hii, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na pande zote mbili ili kuweka mambo sawa na tayari kuna dalili za kufanikiwa. 

Hatua hizi ni pamoja na kufanyika kwa mkutano wa biashara na uwekezaji kati ya India na Tanzania jijini New Delhi, India muda si mrefu. 

Takwimu zilizowasilishwa wakati wa mkutano huo zinaonyesha kuwa kiasi cha biashara kati ya Januari na Juni mwaka huu cha dola milioni 918.19 kilikuwa asilimia 57 ya thamani yote ya biashara ya mwaka 2020. 

Washiriki wa mkutano huo akiwamo Balozi wa Tanzania nchini India, Baraka Luvanda, wanapendekeza ifanyike ziara ya ujumbe wa wafanyabiashara wa India nchini mwezi huu kama moja ya hatua za kurekebisha mambo.

“Karibuni Tanzania tuna fursa nyingi za biashara na uwekezaji pamoja na mazingira salama, thabiti na yanayofaa kwa mitaji yenu yanayowahakikishia usalama wa uwekezaji na faida zenu,” Balozi Luvanda anawaambia zaidi ya washiriki 50 wa mkutano huo uliofanyika Septemba mwaka huu.

Wajumbe wa mkutano huo pia wamefahamishwa kuhusu hali ya sasa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi pamoja na mwelekeo wa maendeleo nchini, hasa wakati huu wa janga la Uviko-19.

Vilevile, washiriki walipewa taarifa kuhusu mwenendo mzuri wa miaka mingi wa biashara baina ya nchi hizi ambao ni kielelezo halisi cha ushirikiano wa jadi, historia na urafiki kati ya India na Tanzania.

India ni mshirika namba moja wa biashara wa Tanzania, ikiwa na asilimia 16 ya biashara zote za nje na ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa uwekezaji nchini. 

Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC), uwekezaji wa India ni zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.2, sawa na Sh trilioni 5.06.

Kwa mujibu wa Ubalozi wa India nchini, Tanzania hununua kwa wingi mafuta, dawa, sukari, vifaa vya umeme, pikipiki na spea zake kutoka India. 

Kwa upande mwingine, Tanzania huiuzia India mazao ya jamii ya mbaazi, korosho, dhahabu, karafuu na mbao ambavyo kwa mwaka jana; pamoja na bidhaa nyingine, vililiingizia taifa dola za Marekani milioni 525.95.

Mwaka 2019, 2018 na 2017 mapato hayo yalikuwa dola milioni 866.68, milioni 739.03 na milioni 977.55 mtawalia, wakati mwaka 2016 kiasi kilichopatikana kilikuwa dola milioni 706.2.

Mwaka 2020 India iliiuzia Tanzania bidhaa zenye thamani ya dola milioni 1,087.09 ukilinganisha na dola milioni 1,126.82 mwaka uliotangulia. 

Mauzo yake ya mwaka 2018, 2017 na 2016 yalikuwa dola milioni 1,218.7, milioni 1,165 na milioni 1,421.46 mtawalia.

Thamani ya biashara baina ya nchi hizi mbili ilikuwa dola milioni 1,993,5 mwaka 2019 na dola milioni 1,957.1, milioni 2,142.55 na milioni 2,127.66 mwaka 2018, 2017 na 2016 mtawalia.

Tanzania ilifanya mauzo ya dola milioni 346.77 kati ya Januari na Juni mwaka 2021, India iliingiza dola milioni 571.42.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), thamani ya biashara kati ya India na Tanzania ilikuwa dola milioni 2,127.66 mwaka 2016 na milioni 2,408 mwaka 2015. Mwaka 2013 nchi hizi mbili zilifanya biashara yenye thamani ya dola milioni 3,060.88 ukilinganisha na milioni 1,360.73 mwaka 2012.

Dhahabu ndiyo iliyoiingizia Tanzania fedha nyingi kutoka India mwaka jana (dola milioni 149.38). Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na dola milioni 226.01 zilizotokana na mauzo ya dhahabu kati ya Januari na Juni mwaka 2021.

Mauzo ya dhahabu mwaka 2019 yalikuwa dola milioni 602.13 wakati mwaka uliotangulia zilipatikana dola milioni 547.9 na mwaka 2017 na 2016 mauzo ya dhahabu India yaliingiza dola milioni 596.66 na milioni 282.79 mtawalia.

Aidha, India huiuzia Tanzania dawa nyingi za kutibu magonjwa ya binadamu.

Kwa mujibu wa Balozi wa India nchini, Binaya Pradhan, miongoni mwa kampuni kubwa za India zilizowekeza nchini ni Benki ya Baroda, Benki ya India, Benki ya Canara, Tata International Limited, Bharti Airtel, Kamal Group of Industries, Escorts, Ashok Leyland, Eicher, Bajaj, TVS, Kirloskar, Shapoorji Pallonji, Larsen & Toubro na Godrej.

329 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!