Bibi afariki baada ya kuruka kutoka ghorofani

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Unguja

Rehema Chande (70),ambaye ni mkazi wa Unguja, Zanzibar, amefariki dunia baada ya kuruka kutoka ghorofa ya pili nyumba anayoishi wakati akijiokoa dhidi ya moto uliowaka ndani ya nyumba hiyo.

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Zanzibar, Rashid Mzee Abdallah amethibitisha tukio hilo lililotokea leo Agosti 29, 2022 saa 3.30 asubuhi katika Shehia ya Kiponda Wadi ya Malindi, Mji Mkongwe ambapo bibi huyo aliruka na mjukuu wake Nabili Issa Ramadhani (5) ambaye amejeruhiwa na kulazwa Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Kamanda amesema kwamba walipofika eneo la tukio walimkuta bibi huyo na mjukuu wake lakini walipofikishwa hospitalini daktari alisema tayari Rehema ameshafariki dunia.

“Rehema aliruka kujiokoa na moto baada ya kutanda na kushindwa kutoka ndani, kwa hiyo aliporuka yeye kapoteza maisha lakini mjukuu wake amejeruhiwa na anaendelea na matibabu,” emesema Abdallah.

Kuhusu athari zingine, Mkuu huyo wa Kikosi cha Zimamoto, amesema bado wanaendelea na kazi ya kuuzima moto huo kutokana mazingira ya eneo hilo kutokuwa rafiki.

Sheha wa Shehia hiyo, Juma Khamis Makame amesema bibi huyo alikuwa anaishi na mjukuu wake na watoto wengine lakini kwa wakati huo hawakuwa ndani