Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),unatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 20 kuwalipa watumishi wa Umma waliondolewa kazini kwa kosa la kughushi vyeti

Hayo yameelezwa leo Novemba 9,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa hifadhi ya jamii (PSSSF),CPA Hosea Kashimba, wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/2023 .

CPA Kashimba amesema kuwa wanakadilia kulipa watu zaidi ya 9,000 na kiasi cha Sh. bilioni 20 kitatumika kama malipo ya fedha za michango walizozichangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii katika kipindi chao cha utumishi wa umma.

“Rais alielekeza watumishi hawa waliobainika kuwa na vyeti feki waanze kulipwa fedha zao za michango kuanzia Novemba mosi mwaka huu lakini kinachotakiwa hivi sasa kwa watu wote ambao walikutwa na sakata hili ni kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu ambazo zitaletwa kwetu kwa ajili ya malipo hayo.

“Badala ya kuja PSSSF, wanapaswa sasa kwenda kwa waajiri wao wa mwisho ili kujaziwa fomu hizo na kuzilileta kwetu na sisi tutatoa kipaumbele kwao kwa kulipa ndani ya siku 60 tangu kuletwa kwa madai hayo”amesema CPA Kishimba

CPA Kashimba amesema gharama za uendeshaji wa mfuko huo zimepungua kwa mwaka kutoka Shilingi bilioni 128.93 mwaka 2018 hadi shilingi bilioni 68.83 sawa na kushuka kwa asilimia 46.61 kutokana na uunganishwaji wa mifuko minne.

Amesema uunganishwaji wa mifuko hiyo minne imeleta uendelevu wa mifuko kwani umenusuru udororaji wa mifuko na kuanzishwa kwa mfuko wa PSSSF ambao umeongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Amesema kuwa uunganishwaji huo umeondoa ushindani usio na tija kwani kumekuwepo na mifuko ya pensheni miwili yenye majukumu tofauti ya mmoja kuhudumia sekta binafsi na mwingine sekta ya umma.

“Uunganishwaji huu umewezesha kuwianisha mafao yatolewayo na mifuko ya pensheni ambapo kuanzia Julai 1,mwaka huu wanachama wote wa mifuko ya pensheni wanalipwa mafao ya uzee kwa kutumia kanuni zinazofanana ambazo zinalipa mafao bora na kuwezesha mifuko,”amesema CPA Kashimba

Aidha CPA Kashimba ameeleza kuwa Mfuko huo unatambua Moja ya changamoto kubwa kwenye jamii ni uelewa mdogo kuhusu sekta ya hifadhi ya jamii hivyo PSSSF imejipanga kuendelea kutoa elimu kwa wanachama wake ili kuhakikisha sekta hiyo inafanikiwa .

Amesema kuwa ili jitihada za kuhakikisha lengo la kutoa huduma bora linatimia,Mfuko unaendelea kutekeleza mambo mbalimbali yanayolenga kurahisisha utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na mtandao wa Ofisi za Mfuko ambapo una Ofisi Kila Mkoa na baadhi ya Wilaya Kwa lengo la kuwa karibu na wanachama.

“Mfuko una kituo cha kupiga simu bure kwa ajiri ya wanachama ambapo huduma hutolewa hadi saa mbili usiku ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji wa masuala ya yanayohusu huduma mbalimbali za uanachama,”amesema CPA Kashimba.

Akieleza matarajio ya baadae,amesema wanatarajia kuongeza vituo vya uhakiki Katika halmashauri mbalimbali na kuanzisha utaratibu wa kujihakiki kupitia simu janja na kusaidia Kila taarifa ya mwanachama iwe kwenye mfumo.

“Matarajio mengine ni kuhakikisha mifumo ya PSSSF inasomana na mifumo mingine kutoka Taasisi za Umma zinazotoa huduma,kurahisisha uandikishaji wanachama na uletaji wa madai kupitia mtandao na kutumia mifumo mipya ya Tehama kulingana na mahitaji ya Mfuko,”amesema.

CPA Hosea ametaja matarajio mengine kuwa ni kubuni mifumo mipya na salama ya TEHAMA kulingana na mahitaji ya mfuko pamoja na kutumia mifumo ya TEHAMA kwa asilimia 85 huku lengo likiwa ni kutumia kwa asilimia 100 ifikapo 2023 katika shughuli za Mfuko hivyo kuboresha utoaji huduma.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa idara ya Habari -MAELEZO Gerson Msigwa, amewataka watumishi wa umma kuhakikisha kuwa wanafuatilia mara kwa mara waajiri wao kama wanawasailisha michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Wafanyakazi ni jukumu lenu kuhakikisha kuwa mnafuatilia kama waajiri wenu wanapeleka michango yenu katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili kusiwe na shida pale ambapo mtumishi akifika wakati wa kustaafu”amesema Msigwa.